Papa,Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji 2022:Kujenga mustakabali&bila kutenga
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Si wavamizi, si waharibifu, si wanyang'anyi, bali wafanyakazi wenye hiari, zana za kuijua dunia na uzuri wa utofauti wake vyema zaidi, wabeba mienendo ya kuhuisha na wahuishaji wa sherehe za kusisimua kwa upande wa Wakatoliki. Ni wito mpya wa dhati wa kubadili mtazamo na mawazo kwa ndugu wahamiaji ambao unaonekan katika Ujumbe wa Baba Mtakatifu Franncisko wa Siku ya 108 ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, itakayoadhimishwa Dominika tarehe 25 Septemba 2022.
Wahamiaji na wakimbizi, kujenga mustakabali ambapo hakuna mtu atengwe
‘Kujenga mustakabali na wahamiaji na wakimbizi’ ndiyo kauli mbiu inayoongozwa Ujumbe huo muhimu wa Baba Mtakatifu uliotiwa saini huko Mtakatifu Yohane Laterano tarehe 9 Mei na kuchapishwa Alhamisi,tarehe 12 Mei 2022. Katika ujumbe huo Papa anaweka uchunguzi wake katika suala la kuhama ambalo bado ni la sasa na limekuwa la dharura zaidi na vita vya Ukraine , ukiwa unasindikizwa pamoja na vifungu vya Biblia kutoka kwa Manabii na Injili. Maono msingi ni mwisho wa ulimwengu, Ufalme wa Mungu, Yerusalemu Mpya, makao ya Mungu na lengo la wanadamu. Mtazamo huo ni juu ya matukio ya sasa, dhiki za nyakati za mwisho ambazo zinatuita kupyaisha ahadi yetu za kujenga dunia ambapo kila mtu anaweza kuishi kwa amani na hadhi.
Lazima tukaribishe wokovu wa Kristo
Kwa ajili ya kutawala maelewano haya ya ajabu, Papa anaandika, ni lazima tuukaribishe wokovu wa Kristo, Injili yake ya upendo, ili kuthibiti kutokuwepo kwa usawa na ubaguzi wa ulimwengu wa sasa. Hakuna anayepaswa kutengwa, Papa Francisko anasisitiza waziwazi katika Ujumbe huo. Mpango wa Mungu kwa hakika unajumuisha na unaweka wakazi wote wa pembezoni kuwa katikati, kwa maana hiyo ni wahamiaji, wakimbizi, watu waliohamishwa, waathirika wa biashara haramu ya binadamu. “Ujenzi wa Ufalme wa Mungu uko pamoja nao, kwa sababu bila wao haungekuwa Ufalme ambao Mungu anataka. Kujumuishwa kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi ni hali msingi wa kupata uraia kamili. Papa Francisko amesema kuwatendea wahamiaji na ubinadamu, haki zao wakati mwingine zilikiukwa na mamlaka ngumu. Hivyo kujenga mustakabali na wahamiaji na wakimbizi pia kunamaanisha kutambua na kuthamini kile ambacho kila mmoja wao anaweza kuleta katika mchakato wa ujenzi. Papa Fransisko anakumbuka unabii wa Isaya, ambamo “wageni hawaonekani kama wavamizi na waharibifu, bali kama watenda kazi walio tayari kujenga upya kuta za Yerusalemu mpya”. Kwa hiyo kufika kwa wageni kunawasilishwa kama chanzo cha utajiri.
Mipango inayolengwa
Kwa upande mwingine, Papa amebainisha kuwa ni historia yenyewe inayotufundisha kwamba mchango wa wahamiaji na wakimbizi umekuwa msingi kwa ukuaji wa kijamii na kiuchumi wa jamii zetu. Na ndivyo ilivyo leo hii. Kazi yao, uwezo wao wa kujitolea, ujana wao na shauku yao huboresha jamii zinazowakaribisha. Lakini mchango huu unaweza kuwa mkubwa zaidi ukithaminiwa na kuungwa mkono kupitia mipango inayolengwa. Huu ni uwezo mkubwa, tayari wa kujieleza, ikiwa tu watapewa nafasi.
Nguvu mpya ya maisha ya kikanisa
Kwa hakika, Papa anabainisha, uwepo wa wahamiaji na wakimbizi wakati mwingine unawakilisha changamoto kubwa, lakini zaidi ya yote ni fursa ya ukuaji wa kiutamaduni na kiroho kwa wote. Shukrani kwao, tunaweza kukomaa katika ubinadamu na kwa pamoja kujijenga sisi zaidi, amesema Papa Francisko. Hivyo nafasi za mapambano yenye kuzaa matunda kati ya maono na mapokeo mbalimbali ambayo yanazalishwa na utajiri uliomo katika dini na hali ya kiroho isiyojulikana kwetu na ambayo kiukweli hugunduliwa. Hakika, kufika kwa wahamiaji na wakimbizi wakatoliki kunatoa nguvu mpya kwa ajili ya maisha ya kikanisa ya jumuiya zinazowakaribisha, amesisitiza Papa.
Ushirikishishana maonesho na vielelezo vya imani
Kushirikishana maonesho na vielelezo mbalimbali vya imani na ibada kunawakilisha fursa adhimu ya kuishi kikamilifu zaidi ukatoliki wa Watu wa Mungu, amebainisha. Kwa kuongeza ametoa wito kwa waamini wote, hasa vijana kuwa: “Ikiwa tunataka kushirikiana na Baba yetu wa mbinguni katika kujenga wakati ujao, na tufanye hivyo pamoja na ndugu na dada zetu ambao ni wahamiaji na wakimbizi. Kwa maana hiyo tuijenge leo hii! Kwa sababu siku zijazo huanza leo hii na huanza na kila mmoja wetu. Hatuwezi kuwaachia vizazi vijavyo jukumu la maamuzi yanayopaswa kufanywa sasa, ili mpango wa Mungu katika ulimwengu utimie na Ufalme wake wa haki, udugu na amani ufike. Hatimaye katika Ujumbe wa Papa, kuna sala iliyotungwa maalumu ambapo Papa Fransisko anamwomba Mungu kwamba palipo na kutengwa, udugu ustawi na kwamba sote tunaweza kuwa wajenzi wa Ufalme wako, pamoja na wakazi wote wa vitongoji vya Ufalme wake.