Papa Francisko:Kusali Rosari kwa ajili ya amani na dhidi ya ukatili wa vita
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mbele ya wehu wa vita ni kuendelea kusali kila siku Rosari kwa ajili ya amani. Ni maombi ya Baba Mtakatifu Francisko aliporudi kuzungumzia watu ambao kwa hakika wanaishi katika balaa la vita na ambapo ametazama picha ya Bikira Maria inayoheshimiwa kwa Ibada katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei nchini Italia. Ameeleza hayo mara baada ya tafakari na sala ya Malkiwa wa Mbingu tarehe 8 Mei 2022 kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro.
“Katika masaa haya waamini wengi wamekusanyika kwa pamoja katika picha ya Bikira Maria inayoheshimiwa katika Madhabahu ya Pompei, kwa sala ambayo ilitungwa kutoka katika moyo wa Mwenyeheri Bartolo Longo. Kwa kupiga magoti kiroho kwa Bikira Maria, ninakabidhi mawazo ya shauku ya amani kwa watu ambao katika pande za ulimwengu wanateseka na vita visivyo na maana”, amesema Papa Francsiko.
Baba Mtakatifu amewakabidhi kwa Bikira Maria kwa namna ya pekee mateso na machozi ya watu wa Ukraine. Mbele ya uwazimu wa vita vinavyoendelea, Papa ameomba kuendelea kusali kila siku Rosari takatifu kwa ajili ya amani. Na amesali ili wahusika wa Mataifa wasipoteze wakati kwa ajili ya watu ambao wanataka amani na wanajua vema kuwa vita kamwe havileti amani.