Tafuta

Nia za sala ya Papa kwa mwezi Mei 2022:kwa ajili ya vijana wenye imani

Katika ujumbe kwa njia ya video wa nia za sala ya Papa kwa mwezi Mei amebainisha kwamba:“Tuwaombee vijana wanaoitwa katika maisha ya utimilifu,waweze kugundua kutoka kwake Bikira Maria mtindo wa usikivu,wa mang’amuzi ya kina,wa ujasiri wa imani na kujitoa katika huduma".

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika nia za sala kwa mwezi Mei 2022, zimejikita kutazama vijana wa kike na kiume ulimwenguni kote ambao Papa Francisko anawaomba wawe na ujasiri na kusikiliza. Anawashauri waishi maisha kamili ambapo kwa hakika ni tunda la kijitoa kabisa katika huduma kwa ajili ya wengine. Na zaidi ni mwaliko wa Papa ili kuzungumza na wazee. Kwa sababu hekima yao inapita zaidi ya shida za wakati huu. Video ya mwezi huu inaonesha watu walio mstari wa mbele ambao ni vijana, familia na wazee. Kwa maana hiyo Papa Francisko anatoa chachu ya kuwa na ubunifu na shauku kwa vizazi vipya katika nia za sala. Na  ambapo kwa hakika imani kuu kwa ajili ya vijana ndiyo kiini ili waweze kweli kutengeneza mustakabali mpya tofauti na wa sasa ulio na majanga mbalimbali, hasa ya kivita. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu anahimiza mazungumzo na wazee na kutoa wito wa kuwepo kwa uongozi ulio bora zaidi wa vijana katika maeneo ya umma. Papa Francisko anawasihi kusikiliza na kutoa huduma hasa kuwa na ujasiri kwa sababu amesema ikiwa wanataka kujenga kitu chochote kipya na ili dunia iweze kuwa bora ni lazima wathubutu!

Vijana, familia na wazee

Matashi na mapendekezo hayo  katika ujumbe wake unakumbusha  Wosia wa Kitume wa Chritus vivit, uliochapishwa baada ya Sinodi iliyokuwa inawahusu vijana, ambapo Papa Fransisko alithibitisha kwamba: “Tunahitaji kujenga nafasi zaidi ambapo sauti ya vijana inasikika”. Ombi hilo lilikuwa tayari limependekezwa  mnamo mwaka 2019 na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, ambalo lilianzisha hata chombo cha kimataifa cha uwakilishi wa vijana ili kusaidia  ushiriki wao na uwajibikaji wao katika Makanisa mahalia. Kwa hakika katika ushirikiano wao na Baraza hilo la kipapa limewezesha kutengeneza video ya Papa kwa mwezi Mei iliyotolewa tarehe 3 Mei na Mtandao wa Sala ya Papa Ulimwenguni kote, ambayo inawakilisha sehemu ya kwanza kati ya  nia tatu za sala  kwa kuwaona wahusika wakuu Vijana, mwezi Mei, Familia kwa mwezi Juni na wazee mwezi julai.

Filamu hiyo imetafsiriwa kwa lugha 23 ambapo zinafunika nchi 114 na Papa anaelekeza Mama Maria kama mfano na kiongozi kwa vizazi vipya. Papa Francisko anasema: “Ninapofikiria mwanamitindo ambaye nyinyi vijana mnaweza kujifananisha naye, daima ninaijiwa akilini mwangu na Mama yetu, Bikira Maria, ujasiri wake, uwezo wake wa kusikiliza na kujitoa kwake katika huduma.”

Thubutu

“Maria alikuwa jasiri na akaamua kusema: ‘Tazama mimi hapa Bwana. Katika wakati ule kwakwe ilikuwa hatari. Na ninyi vijana ambao mnataka kujenga kitu kipya, ulimwengu ulio bora, fuateni mfano wake, mthubutu”, amesisitiza Papa Francisko huku picha ya msichana mdogo inaonesha akijaribu kuchora  uso wa Mama Maria. Papa amesema: “Msisahau kwamba  ili kumfuata Maria ni lazima mtambue kufanya mang’amuzi na kugundua kile ambacho Yesu anataka kutoka kwenu, sio kile mnachofikiria akilini kuweza  kufanya”.

Kuzungumza na babu na bibi

Papa Francisko ameendelea: “Katika kufanya mang’amuzi hayo, msaada mkubwa ni  kusikiliza maneno ya babu na bibi. Kwa sababu katika maneno ya bibi na babu mtapata hekima ambayo itawapeleka zaidi ya matatizo ya sasa. Itataweka katika matarajio mapana zaidi ya wasiwasi wenu”. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu tunaona anavyozindua mwaliko wa kufanya muungano wa vizazi ambao ni msingi wa jamii nzima. Katika hitimisho la filamu hiyo, Papa anasali ili vijana wa kikie na kiume wanaoitwa kwenye maisha kamili, wanaweza kugundua mtindo wa kusikiliza, wa kufanya mang’amuzi ya kina, kwa ujasiri wa imani na kujitoa katika huduma”. Na wanaweza kufanya hivyo kwa kumtazama Bikira Maria.

Uhusiano na Siku ya vijana (WYD)huko Lisbon, Ureno

Katika kurejea suala la mama Yetu Maria linahusisha sala ya Papa katika matarajio ya Siku ya Vijana Duniani ijayo (WYD) itakayoadhimishwa huko Lisbon nchini Ureno mwaka 2023, ambayo inaongozwa na mada kuu ya Maria,  kutoka katika Injili ya Luka: “Maria alisimama na kwenda kwa haraka (Lk 1:39 ). Kwa maana hiyo: “Mchakato mzima wa maandalizi wa tukio hilo ni mwaliko kwa vijana kuamka na kusaidia ulimwengu kufanya hivyo”. Amesema hayo Padre João Chagas, Mkuu wa Ofisi ya Vijana ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Akiendelea na ufafanuzi huo amesema: “Katika ujumbe wake wa mwisho kwa vijana, Baba Mtakatifu aliwaalika vijana wasaidiane kuamka pamoja, katika wakati huu mgumu wa kihistoria ambao utakuwa na manabii wa nyakati mpya, na wenye matumaini! Na Bikira Maria atuombee”.

Wazee kusaidia vijana

Kwa upande wake Padre Frédéric Fornos S.J., ambaye ni mkurugenzi wa kimataifa wa Mtandao wa sala  Papa Ulimwenguni kote, shughuli ya  kipapa inayojali sehemu ya vijana (Harakati ya Ekaristi ya Vijana), amesema  kwa nia ya sala ya mwezi huu, katika muktadha wa mchakato wa sinodi, Papa Francisko anataka kusisitiza umuhimu wa malezi ya vijana katika kufanya mang’amuzi. Ni jinsi gani inawezekana kusaidia vijana wakifuata mtindo wa Maria, kusikiliza, kung’amua, ili kuweza kutambua wito wa Bwana na kutoa huduma katika ulimwengu wa leo? Hapa kwa hakika ndipo linaingia jukumu la wazee, kwa sababu wanaweza kuwasaidia katika zoezi hilo”.

WAZEE KUSAIDIA VIJANA
03 Mei 2022, 16:19