Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani. Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani.  

Wamisionari Wa Huruma Ya Mungu: Ishara Hai Ya Huruma Na Msamaha Wa Mungu

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani. Ni Mapadre ambao wamepewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kwa kawaida zilikuwa zinaondolewa tu na Kiti cha Kitume, ishara hai ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwetu sote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake Kitume wa “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba. Katika neno hili upo ufupisho sahihi wa fumbo zima la Imani ya Kikristo. Huruma imepata kuwa hai na yenye kuonekana katika Yesu Mnazareti, na hata ikafikia kilele chake katika Yeye. Baba “aliye mwingi wa rehema” (Efe 2:4), baada ya kumfunulia Musa jina lake kuwa ni “Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli” (Kut 34:6), hakuwahi kuacha hata mara moja kuonesha hali yake ya kimungu katika nafasi zote za historia ya mwanadamu. “Ulipowadia utimilifu wa wakati” (Gal 4:4), kila kitu kilipokuwa kimepangwa kadiri ya utaratibu wake wa ukombozi, alimtuma duniani Mwanae pekee ili kuwafunulia watu wa Mataifa huruma na upendo wake katika ukamilifu wake. Aliyemwona Kristo Yesu, amemwona Baba wa milele (Rej. Yn 14:9). Kristo Yesu, kwa neno, matendo na kwa nafsi yake yote anaifunua huruma ya Mungu.

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma na msamaha.
Wamisionari wa huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma na msamaha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, “tunahitaji kulitafakari tena na tena fumbo la huruma. Ni chemchemi ya furaha, ya utulivu na ya amani. Ni sharti la wokovu wetu. Huruma ni neno linalotufunulia Utatu Mtakatifu wenyewe. Huruma ni tendo la juu na kuu kabisa ambalo kwa njia yake Mungu anatujia sisi. Huruma ni sheria ya msingi ambayo ipo katika moyo wa kila mtu anayemwangalia kwa unyofu wa macho ndugu anayemkuta katika safari ya maisha. Huruma ni njia inayowaunganisha Mungu na binadamu, na kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya hali yetu ya dhambi.” Rej. Misericordiae vultus 1-2. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” aliwathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anafafanua kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani.

Huruma inamuunganisha Mungu na binadamu.
Huruma inamuunganisha Mungu na binadamu.

Hawa ni Mapadre ambao wamepewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kwa kawaida zilikuwa zinaondolewa tu na Kiti cha Kitume. Mapadre hawa hasa ni ishara hai ya namna Baba mwenye huruma anavyowapokea wale wanaotafuta huruma na msamaha wake. Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo, tayari kutweka hadi kilindini ili kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Wamisionari hawa katika utume wao wanaongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rej. Rom. 11: 32). Rej. Misericordiae vultus 18-19. Ni katika muktadha huu, Wamisionari wa huruma ya Mungu 400 kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuanzia tarehe 23 Aprili hadi tarehe 25 Aprili 2022 wanakutana mjini Vatican kama sehemu ya III ya Mkutano wao wa Kimataifa. Hii ni fursa ya kubadilishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi yaliyojitokeza wakati wa maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika maisha na utume wao kama mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Kati ya wawezeshaji wakuu ni pamoja na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa pamoja na Padre Damiàn Guillermo, Profesa Kitivo cha Sheria za Kanisa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Wamisionari Huruma
23 April 2022, 15:16