Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo. Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo. 

Wamisionari wa Huruma ya Mungu: Funikeni Utu wa Wadhambi Kwa Huruma ya Mungu

Uinjilishaji ni utume unaotekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu. Wamisionari wa huruma ya Mungu wanayo dhamana na utume maalum kwenye Makanisa mahalia. Ni matumaini kwamba Wamisionari hawa wataendelea kuongezeka kwa Maaskofu kuteuwa Mapadre watakatifu na wenye huruma, watakaotoa msamaha wa dhambi na hivyo kutambuliwa rasmi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” aliwathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anafafanua kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani. Hawa ni Mapadre ambao wamepewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kwa kawaida zilikuwa zinaondolewa tu na Kiti cha Kitume. Mapadre hawa hasa ni ishara hai ya namna Baba mwenye huruma anavyowapokea wale wanaotafuta huruma na msamaha wake. Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo, tayari kutweka hadi kilindini ili kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Wamisionari hawa katika utume wao wanaongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rej. Rom. 11: 32) na Rej. Misericordiae vultus 18-19.

Wamisionari wa huruma ya Mungu wawafunike wadhambi kwa huruma na upendo
Wamisionari wa huruma ya Mungu wawafunike wadhambi kwa huruma na upendo

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na Wamisionari wa huruma ya Mungu, wakati huu wanapoadhimisha Mkutano wa tatu wa Wamisionari wa huruma ya Mungu Kimataifa. Hawa ni vyombo madhubuti wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, idadi yao, inaendelea kuongezeka kila mwaka, kielelezo cha umuhimu wa dhamana na utume wao maalum kwa Makanisa mahalia. Uinjilishaji ni utume unaotekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu na kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu wanayo dhamana na utume maalum kwenye Makanisa mahalia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu wataendelea kuongezeka maradufu kwa Maaskofu mahalia kuteuwa Mapadre watakatifu na wenye huruma, watakaotoa msamaha wa dhambi na hivyo kutambuliwa rasmi na Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amejikita kwa baadhi ya wahusika kwenye Maandiko Matakatifu: Nuhu na Gharika kuu; Ruthu katika historia ya wokovu sanjari na huruma na ushiriki. Katika mazungumzo yake na Wamisionari wa huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu amekwisha kukazia umuhimu wa Wamisionari wa huruma ya Mungu kulinda utu, heshima na haki msingi za wadhambi, kwa kuwafunika na huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kuonja utu na furaha ya kuwa wana wapendwa wa Mungu.

Ruthu ameingizwa moja kwa moja katika historia ya wokovu kutokana na: mazingira na hali yake kijamii na hasa kwa sababu alikuwa ni mjane, kiasi cha kudhani kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa amemgeuzia kisogo katika maisha yake na hata kutamani kuyatoa maisha yake kuwa ni sadaka kwa Mama mkwe wake Naomi, hadi akifa afe na kuzikwa pamoja naye na kwamba, ni kifo tu kitaweza kuwatenganisha. Akajiaminisha kwa huruma na neema ya Mungu, aliyemkirimia zawadi nyingi na hatimaye kuuona wema wa Mungu. Maneno ya utenzi wa Bikira Maria yanasikika kinywani mwa Ruthu akisema, amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Rej. Lk 1: 52-53. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Ruthu kwa hakika ni uso wa huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika huruma na ushiriki. Kitabu cha Ruthu kinachosimikwa katika Sura IV kimesheheni amana na utajiri mkubwa imani kwa upendo wa Mungu unaowaambata watu wote. Ni kitabu kinachoonesha ufunuo wa Mungu anayetambua undani wa maisha ya mwanadamu katika uaminifu wake, ukweli wa maisha unaomzunguka, ukarimu na matumaini yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake anapokabiliana na majaribu magumu ya maisha. Ukarimu ni kielelezo cha haki na ujasiri unaopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Mapadre.

Wamisionari wa huruma ya Mungu wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu
Wamisionari wa huruma ya Mungu wawe ni mashuhuda wa huruma ya Mungu

Katika Kitabu cha Ruthu, Mwenyezi Mungu hazungumzi kamwe, lakini anamgusa Naomi kwa matendo makuu, kielelezo cha uwepo wake wa daima. Huu ni mwaliko wa kutambua na kukiri uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Hii ni hija yenye ugumu na changamoto nyingi, lakini ni katika safari hii ya maisha, Mwenyezi Mungu anafunua upendo wake wa daima. Ni dhamana ya Mapadre katika maisha na utume wao, kuwa ni sauti ya Mungu, kwa kuwafunulia watu Uso wa huruma ya Mungu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda kazi kati pamoja na waja wake katika furaha na kimya kikuu; katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwa njia ya watu mbalimbali, hao wanageuka na kuwa ni Sakramenti ya uwepo wake angavu! Wamisionari wa huruma ya Mungu, wawe mbali sana na maamuzi mbele ili kujikita zaidi katika ujumla wa maisha ya mdhambi anayekimbilia huruma ya Mungu. Wanaweza kuthubu kuhukumu kwa kutumia kipimo cha huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Wamisionari wa huruma ya Mungu kuwafunika wadhambi kwa blanketi la huruma ya Mungu, ili kulinda utu, heshima na haki zao msingi. Wawe ni vyombo vya huruma na faraja ya Mungu kwa wale wanaoteseka na kusetwa kwa machungu; waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na upweke hasi kama ilivyokuwa kwa Ruthu. Wawe wapole na wakarimu kama alivyokuwa Ruthu. Na kwa njia hii, watu wa Mungu wataweza kuwatambua kuwa kweli ni watumishi waaminifu wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho. Itakumbukwa kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu 400 kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuanzia tarehe 23 Aprili hadi tarehe 25 Aprili 2022 wamekuwa wakikutana mjini Vatican kama sehemu ya III ya Mkutano wao wa Kimataifa. Hii ni fursa ya kubadilishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi yaliyojitokeza wakati wa maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 katika maisha na utume wao kama mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Kati ya wawezeshaji wakuu ni pamoja na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa pamoja na Padre Damiàn Guillermo, Profesa Kitivo cha Sheria za Kanisa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian.

Wamisionari Huruma
25 April 2022, 16:05