Tafuta

. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumtumia Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima ujumbe na matashi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022. . Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumtumia Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima ujumbe na matashi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022.  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox

Waamini wa Makanisa ya Mashariki, tarehe 24 Aprili 2022 wameadhimisha Pasaka ya Bwana. Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima ujumbe wa Pasaka, Sherehe ya kutoka katika giza na uvuli wa mauti na kuanza maisha mapya; mapambazuko yanayofukuzia mbali usiku wa vita kwa watu wa Mungu nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ni imani iliyotangazwa na kushuhudiwa kwanza kabisa na wanawake jasiri wa imani, Mitume wa Yesu na hatimaye waamini wa Kanisa la Mwanzo. Ni imani ambayo imethibitishwa kwa njia ya Agano Jipya, wakaitangaza na kuihubiri kwa ari na moyo mkuu kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka pamoja na Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu amefufuka kutoka wafu, kwa kifo chake alishinda mauti. Wafu amewapa uzima. Rej KKK 638. Sherehe ya Pasaka ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Waamini wa Makanisa ya Mashariki, tarehe 24 Aprili 2022 wameadhimisha Pasaka ya Bwana. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumtumia Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima ujumbe na matashi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022.

Pasaka ya Bwana Ni Sherehe ya Upendo na mwanzo wa maisha mapya.
Pasaka ya Bwana Ni Sherehe ya Upendo na mwanzo wa maisha mapya.

Hii ni Sherehe kutoka katika giza na uvuli wa mauti na kuanza maisha mapya; mapambazuko ya siku mpya inayofukuzia mbali usiku wa vita kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Watu wote wa Mungu wanasikia na kuelemewa na uzito wa mateso na mahangaiko ya watu kutokana na madhara ya vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwangalia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu na kwa mateso yake, amebeba ndani mwake mateso na mahangaiko ya walimwengu wote. Fumbo la Pasaka ni mwanzo wa maisha mapya na ukombozi kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Mwaliko ni kusali na kuombeana, ili kweli kama viongozi wa Makanisa waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda amini wa ujumbe wa Injili ya Kristo Mfufuka na Kanisa kama Sakramenti ya Wokovu. Lengo ni kuwawezesha watu wote wa Mungu kuingia katika Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani.

Baba Mtakatifu Francisko alikua anatarajia kukutana na kuzungumza na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima mwezi Juni 2022 huko mjini Yerusalemu, lakini kutokana na diplomasia ya Vatican mkutano huu umesogezwa mbele hadi wakati mwingine, hali na mazingira yatakaporuhusu. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, Jumatano jioni tarehe 16 Machi 2022 alipata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima. Patriaki Cyril alikuwa ameambatana pia na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk ambaye pia ni Mjumbe wa Sinodi Takatifu na Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya nje ya Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow nzima. Kiini cha mazungumzo haya ni uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Kirussi nchini Ukraine, dhamana na wajibu wa Wakristo na viongozi wao katika kuhamasisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili haki, amani na maridhiano viweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima kwa kushiriki katika mazungumzo haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Viongozi wa Makanisa wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki na amani
Viongozi wa Makanisa wawe ni mashuhuda na vyombo vya haki na amani

Kama viongozi wa Makanisa wanasukumwa kuonesha dira na mwongozo unaopaswa kufuatwa na waamini wao, katika mchakato wa kutafuta amani; huku wakiendelea kujikita katika kusali na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili hatimaye, vita iweze kukoma na amani kutamalaki. Kanisa linapaswa kutumia lugha ya Kristo Yesu, yaani upendo na wala si lugha ya wanasiasa. Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, wao ni viongozi wa watu wanaomwamini Mungu, Fumbo la Utatu Mtakatifu na Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Ni katika muktadha huu, viongozi wa Makanisa hawana budi kushikamana na kuungana kwa pamoja ili kutafuta amani, kuwasaidia wale wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kuongeza juhudi za kusitisha vita. Viongozi hawa wakuu wa Makanisa wamekazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya kufikia amani ya kweli na ya kudumu. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanaoathirika na mashambulizi haya ya kivita ni watu wa kawaida na wanajeshi wa Urussi wanaojikuta wakipoteza maisha yao kutokana na vita.

Viongozi wa Makanisa washikamane katika haki, amani, utu na heshima ya binadamu
Viongozi wa Makanisa washikamane katika haki, amani, utu na heshima ya binadamu

Makanisa hayana budi kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa sasa kuna uelewa na kiu kubwa ya kutaka amani na watu wamekwisha kujifunza madhara ya vita. Makanisa yanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kuna watoto, wanawake na wazee wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na uvamizi wa kivita nchini Ukraine. Roho Mtakatifu anayewaunganisha katika huduma kama viongozi wakuu wa Makanisa anawataka wawasaidie waathirika wa vita.

Papa Ujumbe wa Pasaka
25 April 2022, 16:38