Papa: Ulinzi Wa Watoto Wadogo Dhidi ya Nyanyaso Ni Wajibu Wa Wote
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 29 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM. Amekazia umuhimu wa Kanisa kulinda utu, heshima na haki msingi za watoto; shuhuda zilizotolewa na wahanga wa nyanyaso za kijinsia; kwa kukutana na kuwasikiliza kama kielelezo makini cha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiuu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba Mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” Katiba itakayoanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste anasema, Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM sasa itakuwa ni sehemu ya shughuli za kila siku za Sekretarieti kuu ya Vatican. Tume itakuwa chini Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kuonesha umuhimu wa Kanisa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Tume itaendelea kuwa huru kutoa maoni sanjari na kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya Kanisa zima. Kumekuwepo na mafanikio makubwa, lakini bado kuna mambo mengi yanapaswa kutendwa, kwa ajili ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Ushirikiano wa Tume na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ni kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo: Ulinzi, uponyaji na haki kutendeka kadiri ya taratibu, kanuni na sheria za Kanisa.
Kila mwaka, Tume itamwandalia Papa taarifa kuhusu harakati za Makanisa mahalia katika ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa kujikita katika: ukweli, uwazi na uwajibikaji, ili kuliwezesha Kanisa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, vinginevyo, waamini watakosa imani na Kanisa na hivyo kugumisha mchakato wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kutendwa dhidi ya watoto wadogo. Mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni mrefu na tete; unahitaji matumaini, kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu na kuomba nguvu ya Roho Mtakatifu, hali inayohitaji imani thabiti kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kosa kubwa kwa sababu zinaacha madonda ambayo wakati mwingine si rahisi kufutika hata kidogo, kiasi hata cha kutishia usalama na maisha ya wahanga, wanaopekenywa na upweke hasi. Kila mwamini kadiri ya wito na dhamana yake ndani ya Kanisa anaalikwa kusimama kidete kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa kwa kujielekeza katika haki na uponyaji. Ni wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia kuanzisha vituo, mahali pa kuwasikilizia wahanga wa nyanyaso za kijinsia, kama sehemu ya mchakato wa kuganga, kuponya na haki kutendeka.