Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo itajikita katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia. Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo itajikita katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia. 

Tafakari Ya Njia Ya Msalaba Kuzunguka Magofu Ya Colosseo: FAMILIA

Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo itajikita katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Furaha ya Upendo ndani ya familia sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia. Huu ni mwaka utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

IJUMAA KUU: Kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Aprili 2022 anatarajiwa kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 4:15 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki ataongoza Njia ya Msalaba, mwishoni atatoa neno na kuwapatia waamini baraka yake ya kitume. Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo itajikita katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia.” Huu ni mwaka utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”.  Furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1.

Hizi ni tafakari ambazo zimeandaliwa na Utume wa Familia. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Kanisa linatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbalimbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa.

Njia ya Msalaba: Maisha ya Ndoa na Familia Katika Ulimwengu mamboleo
Njia ya Msalaba: Maisha ya Ndoa na Familia Katika Ulimwengu mamboleo

Familia katika ulimwengu mamboleo zinakabiliwa na fursa, matatizo na changamoto nyingi. Ukweli huu unafumbatwa katika tafakari ya Njia ya Msalaba kwa Mwaka 2022 kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma. Ni changamoto zinazofumbatwa katika maisha ya wanandoa vijana; utume wa maisha ya ndoa na familia; wanandoa ambao hawakubahatika kupata watoto katika maisha yao. Hizi ni changamoto za familia zenye watoto wengi; familia zenye watoto walemavu; familia inayotunzwa na mzazi mmoja peke yake. Wazee nao wamechangia katika tafakari hizi. Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama, changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Kuna tafakari za wajane wanaoendelea kuwatunza watoto wao. Familia zenye watoto waliowekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa Mungu, Kanisa na jirani. Kuna tafakari ya familia ambayo imempoteza mtoto wao wa pekee. Katika vita mipasuko ya kijamii, kuna shuhuda kutoka kwa familia nchini Ukraine na Urussi na hatimaye ni tafakari kutoka kwa familia ya wakimbizi na wahamiaji.

Katika Sala ya Mwanzo wa Njia ya Msalaba, Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Njia hii ya Msalaba ni sehemu ya maisha na utume wa maisha ya ndoa na familia, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya Injili ya uhai, hekima, faraja na matumaini. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuzitegemeza familia zinazoogelea kwenye mashaka, familia zenye madonda ya maisha ili zipate ujasiri wa kupenda, neema ya kusamehe pamoja na ujasiri wa kuwasaidia wengine, ili hatimaye, kujenga familia kubwa ya binadamu inayosimikwa katika fadhila ya upendo, amani na msamaha. Katika Kituo cha Kwanza Yesu anahukumiwa afe! Hapa wanandoa wapya wametimiza punde tu miaka miwili, tangu waliponfunga ndoa yao ambayo imejaribiwa sana kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Katika maisha yao ya kila siku, wanaonja madhara makubwa ya UVIKO-19. Vifo, mafarakano na hata ndoa nyingi kuvunjika, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Wanakabiliana na hali ngumu ya maisha kutokana na mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma, kiasi cha kujikuta wakiwa kama watoto yatima, Bustanini Gethmane.

Katika Kituo cha Pili, Yesu anasalitiwa na Yuda Iskarioti na anakimbiwa na Mitume wake. Familia hii, inasema kwamba, imedumu katika ndoa kwa kipindi cha miaka 10, wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa; Katika malezi na makuzi ya watoto wao. Kufumba na kufumbua, vita ikavuruga mtindo wa maisha na utume wao; imani na upendo, vikaanza kupungua taratibu; mateso na machungu ya maisha yakaingia na kuanza kusimika mizizi yake, kiasi cha kuona uchungu wa usaliti kwa ndugu zao maskini kutokana na vita. Wanamwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie waamini waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa amani na upatanisho. Kituo cha Tatu, Kristo Yesu anahukumiwa afe. Hii ni tafakari ambayo imeandikwa na wachumba walioamua kufunga pingu za maisha hivi karibuni, ili kuunda familia, Kanisa dogo la nyumbani. Katika safari ya maisha yao, wamejikuta wakiwa ni wagumba, hawawezi kupata mtoto, ambaye alikuwa ni ndoto kubwa katika maisha yao. Lakini, wamepiga moyo konde na wanaendelea kuimarika katika imani, faraja na mapendo, huku wakisaidiana na wanachama wa Utume wa Familia, ambao kwa hakika wamewasaidia kupita kipindi kigumu cha historia na maisha yao! Wanamwomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kuishi kikamilifu Sakramenti ya Ndoa Takatifu, licha ya mapungufu wanayokabiliana nayo siku kwa siku.

Familia zinakabiliana na fursa, matatizo na changamoto mbalimbali za maisha.
Familia zinakabiliana na fursa, matatizo na changamoto mbalimbali za maisha.

Kituo cha Nne Mtume Petro anamkana Kristo Yesu. Wanandoa hawa wanasema, tangu mwanzo hawakuwa na haraka ya kutaka kupata watoto, huku wakitamani kuendelea “kula kuku kwa mrija. Lakini, pole pole, wakapata mtoto wa kwanza na baadaye wa pili, hali ambayo ilianza kuwaletea wasi wasi katika maisha na taaluma zao. Wakajikuta wakiwa wanaelemewa na matatizo na changamoto za ukuaji wa watoto wao! Wakazipokea kwa imani na matumaini, leo hii wanaendelea kufurahia maisha. Wanamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwa ni faraja kwa familia zilizobahatika kuwa na watoto wengi, wawe na ujasiri wa kusimama na kuendelea na safari ya ndoa na familia. Kituo cha Tano, Yesu Anahukumiwa na Pilato ili Afe. Tangu mtoto wao wa kwanza akiwa tumboni, alihukumiwa afe na madaktari, wakamtoa angali tumboni. Leo hii wanateseka sana kutokana na maamuzi mbele, kiasi cha kukosa huruma na mapendo; hata kudiriki kuukimbia Msalaba alama ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Ulemavu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Wanamwomba Mwenyezi Mungu awafundishe waamini kupenda, kuthamini, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kituo cha Sita, Kristo Yesu anachapwa kwa mijeledi na kuvikwa taji la miiba kichwani. Huu ni ushuhuda wa familia yenye watoto wengi waliobahatika kupata baraka ya wingi wa wajukuu. Ni familia ambayo imeasili watoto watano wenye ulemavu wa akili. Wameonja na kuguswa na mateso ya watoto hawa, ambayo yamewaletea toba na wongofu wa ndani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya uhai; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika Njia ya Msalaba, kuna watu wengi ambao wanaendelea kupigwa kwa mijeledi, kuelemewa na uzito wa Msalaba. Furaha ya kweli inabubujika kwa wale wanaojitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Wanamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie waamini kuwa ni Wasamaria wema, ili waweze kuwafariji wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili.

Kituo cha Saba, Kristo Yesu Anasulubiwa Msalabani. Hii ni tafakari ambayo imetolewa na Baba wa familia ambaye alijikuta amepigwa na bumbuwazi, baada ya mke wake kuanguka na kupoteza fahamu na hatimaye, kukimbizwa hospitalini ili kuokoa maisha yake. Akabaki hivi hivi katika maisha yake, lakini hata leo hii, anasema huyu Baba wa familia, mbele ya macho yake bado anaendelea kuwa ni Mama wa watoto wake na mke wake mpendwa, licha ya Msalaba mkubwa uliosimikwa ndani ya familia yao. Mama huyu hata katika mateso yake, amekuwa ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani kutokana na ucheshi wake. Anatambua na kuonja furaha ya familia kwa jicho lake pendelevu na angavu. Huu ni mwaliko kwa watoto kuwalinda na kuwatunza wazazi wao, kama alama ya shukrani, chemchemi ya furaha ya kweli na umuhimu wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa moyo wa upendo na ukarimu.

Kituo cha Nane, Simoni wa Kirene anamsaidia Kristo Yesu Kubeba Msalaba. Hii ni tafakari inayotolewa na wazee wa familia ambao hivi karibuni wamestahafu kazi, lakini mbele yao wakakutana na Ugonjwa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ndoa ya mtoto wao ikaingia mchanga, wajukuu ikawalazimu warudi nyumbani kwa Babu na Bibi yao. Ugumu wa ukosefu wa fursa ya kazi na ajira vikagusa na kutikisa msingi wa maisha ya ndoa na familia yao. Wakajikuta daima wakiwa na hofu ya kifo mbele ya macho yao. Baada ya tafakari ya kina, wakajikuta wakiwa ni watu wenye furaha, kwa kuweza kuwasaidia wajukuu wao, zawadi kubwa ambayo wanaendelea kuitunza moyoni mwao na kwamba, malezi ya watoto hayana ukomo hadi kieleweke! Wanamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie waamini waweze kujenga umoja na mshikamano wa udugu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kituo cha Tisa, Kristo Yesu anakutana na Wanawake wa Yerusalemu. Huu ni ushuhuda wa familia ambayo kwa muda mrefu imejikuta ikielemewa na upweke hasi, lakini tangu walipopata fursa ya kuasili Watoto wawili na hivyo kuwa watu wanne ndani ya familia, wamekuwa ni chemchemi ya furaha na upendo. Watoto hawa wamekuwa ni siri ya furaha yao ya ndani. Wanamwomba Mwenyezi Mungu awakirimie waamini ujasiri wa kujenga familia zinazosimikwa katika ukarimu na upendo kwa jirani.

Kituo cha Kumi, Kristo Yesu Anahukumiwa Afe. Hii ni tafakari ya Mama mjane, ambaye analazimika kuwatunza watoto wake wawili, lakini wamefarijika daima kwa uwepo wa Kristo Yesu katika maisha yao, wanapouangalia Msalaba, Kwa upande wao, Kanisa licha ya mapungufu yake, limekuwa msaada mkubwa katika maisha yao, kama Sakramenti ya wokovu. Katika mahangaiko yao, hawakuweza kuokoa maisha ya Baba wa familia. Lakini, Msalaba umekuwa ni urithi na amana ya maisha yao ya kiroho; kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu ambao daima umeendelea kuwaandama na kuwaambata licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Anawaombea waamini wote waweze kujenga mshikamano wa udugu, katika raha na machungu ya maisha. Kituo cha Kumi na Moja: Kristo Yesu anampatia msamaha mhalifu na kumwahidia mbingu. Sehemu hii ya tafakari imeandikwa na familia iliyojiamini, iliyowekeza vyema kwa malezi na makuzi ya mtoto wao, ili aweze kuwa na maisha bora zaidi. Kufumba na kufumbua, Mtoto akapoteza dira na mwelekeo wa maisha na kutaka kuwekwa wakfu kwa ajili ya Mungu, Kanisa na jirani zake. Wazazi nao wakamwonjesha ubaridi na kuanza kumtenga, ili kufundisha adabu kwamba, alikuwa anakosea. Wanasema, walitaka kumwadhibu kama wale wahalifu wawili. Lakini, hatimaye, kama ilivyokuwa kwa yule mhalifu, waliishia kuomba msamaha na huruma ya Mungu, wakimsihi awakumbuke na kuwaombea mbele ya Mwenyezi Mungu. Familia hii inawaombea wazazi wote waweze kuwa makini katika kufuatilia na hatimaye, kulea miito ya watoto wao, waweze kuwa wafuasi waaminifu wa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni muhimu sana.
Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni muhimu sana.

Kituo cha Kumi na Mbili: Kristo Yesu Anamkabidhi Bikira Maria Kwa Mwanafunzi Aliyempenda. Hii ni tafakari kutoka katika familia inayoundwa na watu watano. Miaka mitano iliyopita, Saratani iliingia ndani ya familia na kumwathiri mtoto mdogo waliyemhudumia hadi dakika ya mwisho wa maisha yake, miaka miwili iliyopita. Haikuwa rahisi kukubali na kupokea ugonjwa wa Saratani ndani ya familia, lakini Mwenyezi Mungu akawakirimia neema na baraka ya kuweza kupokea Msalaba huu mzito ndani ya familia yao. Wakati wa matibabu, wazazi hawa walihisi kwamba, wako chini ya Msalaba kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria pale Mlimani Kalvari. Wanamwomba, Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia Roho Mtakatifu Mfariji, ili waamini waweze kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao.

Kituo cha Kumi na Tatu, Kristo Yesu Anakufa Msalabani. Kifo katika maisha ya mwanadamu kinaleta mabadiliko ya ghafla na hasa kikiwa kinasababishwa na vita. Kila kitu kinapoteza maana na thamani yake, kiasi cha kuanza kujiuliza, Je, Mungu yuko wapi? Je, kwani nini ametelekeza na kuwafanya kusambaratika na hivyo kupoteza ndoto ya kuendelea kuishi? Hawa ni waamini walioguswa na kupapaswa na vita, wanasema, wamelia kiasi kwamba, kwa sasa hawana tena machozi na wameshindwa kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Lakini hata katika kimya kikuu na mtutu wa bunduki, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuzungumza. Katika vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, Mwenyezi Mungu aendelee kuwafundisha waja wake umuhimu wa kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani; watambue kwamba, licha ya tofauti zao msingi, lakini wao ni ndugu wamoja; mambo ambayo kamwe hayawezi kubomolewa na mlipuko wa mabomu. Awasaidie waamini kujikita katika nguvu ya msamaha, ili wajenge amani na maridhiano. Kituo cha Kumi na Nne: Kristo Yesu Anashushwa Msalabani. Vita imefisha historia ya maisha yao ya huko nyuma. Wameshuhudia watu wengi wakipoteza maisha na wengine kugeuka kuwa walemavu. Wao kwa huruma ya Mungu wameponyoka. Utu, heshima na haki zao msingi zimepotea. Ni wakimbizi na wahamiaji wanao tamani siku moja, kuona jiwe la kaburi la Yesu likiwa limeondolewa, ili kuendelea kuishi pasi na vitisho vya mabomu, nyanyaso na dhuluma. Mwenyezi Mungu awasaidie watu kutambuana na kuthaminiana kama ndugu wamoja!

Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu 15 Aprili 2022 Colosseo Mjini Roma.
Njia ya Msalaba Ijumaa Kuu 15 Aprili 2022 Colosseo Mjini Roma.

SALA YA MWISHO:

Baba mwenye huruma, unaliangazia jua lako juu ya wema na wabaya, usiiache kazi ya mikono yako, ambayo hukusita kumkabidhi Mwanao wa pekee, mzaliwa wa Bikira Maria aliyesulubishwa kwa Mamlaka ya Pontio Pilato, amekufa na kuzikwa ndani ya tumbo la nchi; Akafufuka kwa wafu siku ya tatu, akamtokea Mariamu Magdalena, Mtakatatifu Petro, kwa Mitume wengine na wanafunzi, na yuko hai daima katika Kanisa takatifu, Fumbo la Mwili wake hai duniani. Endelea kuwasha katika familia zetu taa ya Injili, ambayo huangaza furaha na huzuni, juhudi na matumaini: kila nyumba inaakisi sura ya Kanisa, ambaye sheria yake kuu ni upendo. Kwa kumiminiwa kwa Roho wako Mtakatifu, tusaidie kuuvua utu wa kale ulioharibiwa na tamaa danganyifu, na kutuvika utu mpya, ulioumbwa kwa haki na utakatifu.

Utushike mkono kama Baba, tusiende mbali na Wewe; ugeuze mioyo yetu yenye uasi kwa moyo wako Mtakatifu, ili tuweze kujifunza kufuata miradi ya amani; wawezeshe wapinzani kushikana mikono, ili wapate kusameheana; Ondoa mkono wa vita dhidi ya ndugu wamoja, ili palipo na chuki maridhiano yaweze kustawi. Kamwe tusiwe adui wa Msalaba wa Kristo, ili hatimaye, tuweze kushiriki katika utukufu wa ufufuo wake. Anayeishi na kutawala pamoja nawe, katika umoja wa Roho Mtakatifu, Milele yote.

R/. Amina.

Njia ya Msalaba 2022
11 April 2022, 15:58