Slovakia Mashuhuda wa Imani Katika Huruma na Upendo Kwa Maskini Na Wahitaji Zaidi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Slovakia kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Septemba 2021 ilinogeshwa na kauli mbiu “Pamoja na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu Njia ya Kwenda kwa Yesu”. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Septemba 2021, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mateso Saba, aliungana pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Slokavia kusali kwenye Madhahabu ya Bikira Maria wa Mateso Saba huko mjini Šaštín. Bikira Maria wa Mateso saba, anaheshimiwa sana nchini Slovakia. Kwa namna ya pekee kabisa, tarehe 15 Septemba 2021 Mama Kanisa aliadhimisha Kumbukumbu ya Bikira Maria, Mama wa Mateso saba. Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu hii kitaifa, iliadhimishwa kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Hii ni Sikukuu ambayo imepata chimbuko lake kunako Karne ya kumi na nne. Kunako Mwaka 1727 Papa Benedikto XIII akaiingiza rasmi kwenye Kalenda ya Kanisa. Mwaka 1913 Papa Pio X akatangaza rasmi kwamba, itakuwa inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 15 Septemba baada ya Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba. Ilikuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kushuhudia amana na utajiri wa Kanisa nchini Slovakia unaofumbatwa katika madhehebu na mapokeo yanayounganisha wakristo kutoka Mashariki na Magharibi.
Hiki kilikuwa ni kipindi cha janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, hija hii ya kitume, itazaa matunda kwa wakati wake. Watu wa Mungu kutoka Slovakia mara kwa mara wanaonekana kwenye katekesi za Baba Mtakatifu Francisko na wakati wa Sala kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kielelezo kwamba, ni watu ambao wanapenda kujenga mahusiano na mafungamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022 kwa mahujaji kutoka Slovakia waliofika mjini Roma kumshukuru Baba Mtakatifu kwa hija yake ya Kitume mwezi Septemba 2021. Amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu kutoka Slovakia. Pamoja na mambo mengine, amekazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu; wawe ni mashuhuda wa Injili ya ukarimu na mapendo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mchakato wa utamadunisho na uinjilishaji. Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Slovakia kujenga utamaduni wa kukutana katika umoja na utofauti wao, kwa kujikita katika fadhila ya ukarimu, uwazi na kipaji cha ubunifu; mambo msingi yanayopata asili yake kutoka kwa Roho Mtakatifu, anayewasafisha na kuwatakasa na dhambi zao; anayeganga na kuponya madonda na machungu ya ndani, ili hatimaye, kuwakirimia amani na utulivu wa ndani.
Watambue kwamba, wao ni chumvi ya dunia kwa njia ya ukarimu na nuru ya ulimwengu katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika amani. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa waathirika wa vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine. Wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo kwa wale wanakimbilia usalama na hifadhi nchini mwao, ili kuwaonjesha moyo wa mshikamano kama ilivyo pia kwa ndugu zao ambao wako mbali kama ilivyo kwa wale walioko nchini Cuba. Watakatifu Cyril na Method, Wasimamizi wa Bara la Ulaya, wanaheshimiwa sana na familia ya Mungu huko Czech na Slovakia, kutokana na mchango wao katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho, amana na utajiri mkubwa ulioachwa na ndugu hawa pacha katika maisha na utume wa Kanisa! Ni ndugu ambao wameacha urithi mkubwa wa tunu msingi za maadili, kiasi kwamba, Ukristo umekuwa ni chemchemi ya matumaini hasa wakati wa giza na mahangaiko ya watu! Walichangia kutafsiri Biblia ambayo ni msingi wa maisha ya kiroho na maendeleo ya kitamaduni; rejea ya sheria katika nchi mbalimbali duniani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, watakatifu hawa wawasaidie kujenga madaraja ya udugu wa kibinadamu tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuheshimu na kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Stanislav Zvolenský, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Slovakia katika salam zake kwa Baba Mtakatifu Francisko, amemshukuru na kumpongeza kwa hija yake ya kitume nchini Slovakia, fursa ambayo imewasaidia kukiri, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mahujaji waliofika mjini Vatican ni ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene kama njia ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo. Ni mashuhuda wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa waathirika wa vita kati ya Urussi na Ukraine, lakini kwa namna ya pekee, ni kielelezo muhimu cha mshikamano na familia ya Mungu nchini Cuba. Pamoja na mambo mengine, wanataka kuwawezesha kiroho na kimwili ili kupata mahitaji yao msingi.