Sikukuu ya Wafanyakazi 2022: Usalama Na Afya za Wafanyakazi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mei Mosi ya kila mwaka ni Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Maadhimisho ya Mei Mosi 2022 yanafanyika wakati ambapo kuna changamoto kubwa za usalama kazini, hali ambayo imepelekea wafanyakazi wengi kupoteza maisha katika maeneo ya kazi. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa usalama kazini. Jambo hili linawezekana ikiwa kama kuna ushirikiano wa dhati kati ya waajiri, waajiriwa na serikali husika. Kuna idadi kubwa ya wafanyakazi waliopoteza maisha kutokana na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na wengine wengi kukosa fursa za ajira. Kumbe, kuna haja pia kusimama kidete kuhakikisha kwamba, afya za wafanyakazi zinalindwa na kuendelezwa, ili kupunguza na kama si kufuta kabisa vifo na ajali kazini ambazo zinawaacha mamilioni ya watu wakiwa na ulemavu. Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linasema, maeneo ya kazi ni sehemu muhimu sana ya kujitakatifuza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni mahali pa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo na sehemu muhimu sana ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Maeneo ya kazi yanapaswa kuwa ni sehemu ya kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kutambua haki na wajibu; upendo na uhuru wa watoto wa Mungu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kwa upande wake linakazia kwa kusema kwamba, utajiri wa kweli ni rasilimali watu katika kazi, changamoto ni kujenga utamaduni wa huduma ya usalama na ulinzi wa afya za wafanyakazi. Kuna haja ya kuwepo na uhusiano mzuri kati ya nguvu kazi na mtaji. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kazi kwa sababu ya sifa yake ya kiutu, mtu yuko juu kabisa ya rasilimali zote nyingine zinazohusika katika uzalishaji; na kanuni hii inahusu hasa mtaji. Kumbe, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa kwa upande wake, Mei Mosi linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi. Kanisa linatambua na kuthamini umuhimu wa kazi kama wajibu na utimilifu wa maisha ya mwanadamu sanjari na ushiriki wa mwanadamu katika kuitiisha dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Utu wa mwanadamu ndicho kipimo cha heshima ya kazi. Kazi ni kwa ajili ya mwanadamu na wala si mwanadamu kwa ajili ya Kazi na kwamba, kazi ni sehemu ya utambulisho wa mwanadamu. Huu ni mwendelezo wa ushiriki wa mwanadamu katika kazi ya uumbaji na mchango katika kazi ya ukombozi. Kutokana na ugumu wa dhambi ya asili, Kristo Yesu alitoa mwelekeo mpya wa kazi, kuwa ni kielelezo cha ukombozi; utu na heshima ya binadamu.
Kielelezo cha kazi na utume huu, ni mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, sehemu mbalimbali za dunia, Papa Pio XII kunako Mei Mosi, 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani, atakayewasaidia kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao ili kujenga na kudumisha utu, heshima, haki msingi, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Kwa vile Sikukuu hii iligubikwa sana na kilio cha wafanyakazi, machafuko, kinzani na misigano, hasa kwenye Karne ya XIX, Mama Kanisa akataka Mtakatifu Yosefu kuwa ni kielelezo makini cha mapambano ya kudai haki msingi za wafanyakazi, utu na heshima yao pamoja na kutoa hadhi kwa kazi kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa kazi ya uumbaji na ukombozi ambayo hata Kristo Yesu mwenyewe aliishiriki kiasi hata cha watu kumsema “Huyu si yule seremala…” Mk. 6:3. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa: bidii, juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; kwa kutambua na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao.
Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa kuwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika kutafuta fursa za kazi! Kanisa ni Mama na Mwalimu, daima anapenda kushikamana na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utu, heshima na haki msingi za binadamu hazina budi kupewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, kazi iliyotekelezwa na Mtakatifu Yosefu, ni kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu aliyemuumba mwanadamu, anathamini sana kazi ya uumbaji aliyoitekeleza kwa muda wa siku sita na siku ya saba akapumzika. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa wafanyakazi, aendelee kuwakumbuka na kuwaombea watu wote, ili asiyewepo kijana, familia au mtu awaye yote asiyekuwa na fursa ya kazi. Hii iwe ni dhamana inayowawajibisha watu wote. Mei Mosi ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na kuwaua wafanyakazi wanne.