Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Watu Wanataka Amani Na Wala Si Vita! Wanasiasa Sikilizeni Hili!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu inayomwajibisha mwanadamu kudumisha mahusiano mema na Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na kazi ya uumbaji. Kwa njia hii, binadamu anaweza kupata amani ya kweli na inayodumu, lakini amani hii inaweza kutoweka kama ndoto ya mchana ikiwa kama hakuna mahusiano mema na Mwenyezi Mungu na hapa ni mwanzo wa kinzani na migogoro ya kijamii. Amani ni zawadi ambayo ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na imetekelezwa licha ya binadamu kuendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi na mauti kwa kumkirimia zawadi ya Ukombozi ambayo maandalizi yake yanajionesha kwa namna ya pekee tangu Agano la Kale na kupata utimilifu wake katika Agano Jipya linalojikita katika amani. Hili ni Agano Jipya na la milele, Agano la amani linalowaelekea watu wote. Hii ni amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa wale wote anaowapenda. Mitume walipokuwa wamejifungia kwa hofu na wasi wasi mkubwa wa Wayahudi Kristo Yesu akawatokea na kuwaambia, "Shalom" yaani: Amani iwe kwenu! Huu ni muhtasari wa kazi ya ukombozi, ndiyo maana Mama Kanisa kamwe hawezi kuchoka kutangaza amani duniani kwa kutambua kwamba, amani ni tunda la Msalaba wa Yesu, kwani wakishahesabiwa haki itokayo katika imani, waweze kuwa na amani kwa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
Mateso na Kifo cha Yesu Kristo kimeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadanu, kwani amekombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Msalaba ni kielelezo cha msamaha na upatanisho kati ya Mungu, mwanadamu na mazingira anamoishi, kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye. Amani ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo Yesu Kristo mfufuka aliwapatia wafuasi wake, jioni ile walipokuwa wamejifungia ndani kwa woga wa Wayahudi; kumbe, amani ni zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu; kwani Mungu ni amani, upendo na neema inayotolewa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, mwaliko kwa waamini kujipatanisha na Mungu, jirani na mazingira kwa njia ya Kristo Yesu. Ni katika muktadha huu, wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Huruma ya Mungu kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 24 Aprili 2022, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia heri na baraka Wakristo wote wa Kanisa la Kiorthodox ambao wameadhimisha Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 24 Aprili 2022. Kristo Mfufuka awe ni chemchemi ya matumaini mapya, chimbuko la amani ya kweli na mwisho wa vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine.
Imegota miezi miwili tangu Urussi ilipoivamia Ukraine kijeshi, badala ya vita kukoma, imeendelea kuwaka moto na hivyo kusababisha mateso makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Kipindi hiki cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, iwe ni fursa ya kusikiliza kengele za shangwe na furaha badala ya kuendelea kusikiliza mirindimo ya risasi na mabomu. Inasikitisha kuona kwamba, matumizi ya silaha za kivita yanazidi kupamba moto badala ya mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu ametoa wito wa kusitisha vita kati ya Urussi na Ukraine wakati huu wa Kipindi cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana, ili kuwahudumia walioathirika kwa vita; maneno ya Kristo Yesu, amani iwe kwenu, yasikike na kuzama katika akili na nyoyo za watu wenye dhamana ya kusitisha vita. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani kwa kutambuua na kushuhudia kwamba, amani ya kweli inaweza kupatikana. Viongozi wa kisiasa wasikilize na kujibu kilio cha watu wa Mungu wanaohitaji amani na wala si vita inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo!