Huruma Ya Mungu Ni Chemchemi Ya: Furaha, Msamaha Na Faraja
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sherehe ya Huruma ya Mungu ni shule ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Hapa ni mahali pa kujifunza huruma ya Mungu, ili hatimaye, kuimwilisha katika uhalisia wa maisha ili kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani. Sherehe ya Huruma ya Mungu ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Huruma ya Mungu, Dominika tarehe 24 Aprili 2022 iliyoongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha Uinjilishaji mpya, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amesema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na hatimaye, huruma ya Mungu ni faraja kubwa kwa wasioamini, wanaotaka kugusa Madonda Matakatifu, ili waweze kuamini kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma! Lakini wawe tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka.
Mitume waliokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, kielelezo cha kushindwa kwao; kwa kumsaliti, kumkana na kumkimbia wakati wa Njia ya Msalaba wanaonjeshwa tena huruma ya Mungu inayofumbatwa katika furaha. Mwanzoni walimfuata Kristo Yesu kwa ari na moyo mkuu, lakini wakayeyuka na kutoweka kama umande wa asubuhi. Ni Mitume hawa hawa waliokuwa wanajadiliana ni nani mkuu kati yao, lakini kutokana na hofu, hawakuthubutu kumwangalia, lakini sasa anawatokea na kuwakirimia amani, iliyoibua tena ile furaha ya kweli katika maisha yao, walipomwona Bwana. Akawajalia amani iliyokuwa imetoweka, akawasafisha, akawatakasa na kuwapatia msamaha wake usiokuwa na kifani. Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni chimbuko la amani ya kweli. Huruma ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Hapa ni mahali ambapo mwamini kwa kutubu na kuungama dhambi zake, anapata faraja ya Roho Mtakatifu, amani na furaha ya kweli kwa kukubali dhambi na mapungufu ya kibinadamu, tayari kuambata furaha ya Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Mfufuka aliwakirimia Mitume wake, amani na Roho Mtakatifu na hivyo kuwawezesha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Walipokea nguvu ya Roho Mtakatifu kama zawadi kwa watu waliosamehewa dhambi zao, tayari kuwaondolea watu wa Mungu dhambi zao. Hivyo basi, huruma ya Mungu iwawezeshe waungamishaji kuwa ni wanyenyekevu na vyombo vya huruma na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Ikumbukwe kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu ni ishara ya hamasa ya kimama kwa taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika amana na utajiri wa Fumbo la Imani. Hawa ni Mapadre ambao wamepewa mamlaka ya kuwaondolea waamini dhambi ambazo kwa kawaida zilikuwa zinaondolewa tu na Kiti cha Kitume. Mapadre hawa hasa ni ishara hai ya namna Baba mwenye huruma anavyowapokea wale wanaotafuta huruma na msamaha wake. Hawa ni wamisionari wa huruma ya Mungu kwa sababu wao ni wawezeshaji kwa wote, huku wakiwa wamesheheni ubinadamu, chimbuko la wokovu, uliojaa wajibu katika kushinda vikwazo, tayari kutweka hadi kilindini ili kuanza maisha mapya ya Ubatizo. Baba Mtakatifu anawataka Wamisionari wa huruma ya Mungu, wao wenyewe kuguswa kwanza na huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu; tayari kutoa nafasi kwa wadhambi kusikilizwa na kuondolewa dhambi zao, sanjari na kupewa mashauri bora ya maisha ya kiroho, ili kuanza na hatimaye, kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.
“Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa.” Haya ni maneno ya Kristo Yesu yanayoliwezesha Kanisa kuwa ni Jumuiya ya huruma na chombo cha upatanisho kati ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Ubatizo, inawawezesha Wakristo wote kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, mwaliko kwa waamini wote kuwashirikisha jirani zao, wenye kiu ya huruma ya Mungu katika maisha yao. Huruma ya Mungu imwilishwe katika kuta za familia, maeneo ya kazi na kwenye medani mbalimbali za maisha kiasi kwamba, kila mwamini ajisikie kuwa na wajibu wa kutangaza na kushuhudia amani na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Mfufuka aliwakirimia Mitume wake amani iliyowaimarisha katika imani, baada ya “kuvurugwa na Kashfa” ya Fumbo la Msalaba. Mtume Toma, kielelezo cha wale wasioamini, akapewa fursa ya kuona na kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu Mfufuka. Ni maneno yaliyobubujika huruma ya Mungu kiasi kwamba, Toma, akageuka, akaamini na kukiri akisema: “Bwana wangu na Mungu wangu.” Haya ni maneno yanayoweza kutumiwa na mwamini wakati wowote anapotembea katika uvuli wa mashaka na wasiwasi katika maisha. Toma Mtume, ni kielelezo na mfano wa waamini wanaotindikiwa imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Watu wanaotaka kuona ishara, ili waweze kuamini.
Wote hawa wanafarijika kwa kuona na kugusa Madonda yake Matakatifu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Watambue kwamba, katika kimya kikuu, kuna watu wanaoteseka sana, na hawa ndio wanaohitaji kufarijiwa. Waamini wawe na ujasiri wa kuona na kugusa madonda ya jirani zao: kiroho na kimwili; wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Waamini watenge muda wa kusikiliza, kuwasindikiza na hatimaye, kuwafariji wale wanaoteseka. Kwa kufikiri na kutenda hivi, wataweza kukutana na Kristo Yesu Mfufuka, anayewatazama kwa jicho la matumaini, wale wote waliokata tamaa, ili hatimaye, kuwaonjesha huruma na kuwakirimia amani! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa anayeadhimishwa Jumatatu, baada ya Sherehe ya Pentekoste. Kumbe, Jumatatu baada ya Sherehe ya Huruma ya Mungu, waamini wanaalikwa kumtafakari Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu, anayeliombea Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika kutangaza na kushuhudia Huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Itakumbukwa kwamba, chemchemi ya huruma ya Mungu inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Ibada ya huruma ya Mungu inakolezwa kwa kwa njia ya Novena ya Huruma ya Mungu inayoanza Ijumaa kuu, Siku ile Kristo Yesu alipoteswa na kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuhitimishwa katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Kuna Saa kuu la Huruma ya Mungu, huu ni mwaliko kwa waamini kujizamisha katika huruma ya Mungu, ili kuiabudu, kuitukuza na kusifu uweza mkuu wa Mungu katika kuwahurumia na kuwakomboa wadhambi. Huruma ya Mungu imeshinda haki! Waamini wanahamasishwa kukuza na kudumisha Ibada na uchaji wa Mungu wanapoadhimisha Sakramenti za Huruma ya Mungu yaani: Ekaristi Takatifu na Upatanisho, chemchemi ya utakatifu na mchakato katika uinjilishaji mpya unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Rozari ya Huruma ya Mungu ni chombo cha Ibada kinachowaunganisha waamini wote kuomba huruma ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu mzima. Kristo Yesu ni mwokozi Mwenye Huruma isiyokuwa na kifani. Rozari ya Huruma ya Mungu inawasaidia waamini kutekeleza dhamana na wajibu wao wa Kikuhani, waliojitwalia wakati walipobatizwa. Kwa njia hii, wanapyaishwa na kuwa ni sadaka safi inayounganishwa na Sadaka ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, haki, upendo na huruma!