Mshikamano Wa Udugu wa Kibinadamu Ni Ushuhuda Wa Imani Tendaji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Majadiliano ya kidini, kitamaduni na kiekumene yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha Imani kutoka kwa waamini wa dini mbalimbali duniani. Vita ni chanzo kikuu cha mateso, mahangaiko na maafa kwa watu na mali zao. Hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha utamaduni wa kifo dhidi ya Injili ya uhai na matumaini. Waamini wanao wajibu na haki ya kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa wale wote wanaopenda vita kwa ajili ya masilahi yao binafsi, ili waweze kutubu na kumwongokea tayari kuambatana majadiliano katika ukweli na haki, ili hatimaye, amani ya kweli iweze kupatikana.
Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia vita sehemu mbalimbali za dunia, uthibitisho kwamba, vita ni kushindwa kwa siasa na ubinadamu, ni kitendo cha kujisalimisha kwa aibu mbele ya nguvu za uovu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mahujaji wanaoshiriki katika hija ya mshikamano wa upendo wa kidugu na watu wa Mungu kutoka Ukraine, hija ambayo imeandaliwa na Taasisi ya “The Elijah Interfaith Institute, kutoka Chernivtsi-Ukraine.” Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kutenda muda wa sala na ujenzi wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali. Hii ni changamoto ya kuendelea kuwekeza katika amani duniani na hatimaye, kuondokana na falsafa ya matumizi ya silaha duniani. Watu wajitahidi kujenga na kudumisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kulinda: Utu, heshima, haki msingi za binadamu na utakatifu wa maisha yake ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu.