Tafuta

Papa Francisko Maadhimisho Juma Kuu: Mafumbo ya Wokovu Wa Mwanadamu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Juma Kuu ni kipindi maalum cha kujiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Huu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kwa njia ya vita, hakuna kinachoweza kusalia na wala mshindi wa vita, yote ni upotevu mtupu. Huu ni wakati wa kuachana na utamaduni wa kifo na kuambata amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafumbo ya Wokovu wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti yanafumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Huu ni ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na huduma ya upendo. Ni Siku ambayo Wakleri wanarudia tena ahadi zao kwa Maaskofu mahalia. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kielelezo cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika ya Matawi tarehe 10 Aprili 2022 amewakumbusha waamini kwamba, Juma Kuu ni kipindi maalum cha kujiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Huu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kwa njia ya vita, hakuna kinachoweza kusalia na wala hakuna mshindi wa vita, yote ni upotevu mtupu. Baba Mtakatifu anawaalika wale wote wanaosigana kumwavchia nafasi Kristo Yesu ili aweze kupata ushindi. Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Amekufa kifo cha aibu pale Msalabani, ili Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, iweze kusonga mbele; upendo dhidi ya chuki na uhasama viweze kushindwa na hatimaye, amani ya kweli iweze kutawala katika nyoyo za watu.

Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu.
Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu.

Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika misingi ya: Ukweli, haki, upendo na uhuru wa kweli kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani: “Amani Duniani”. Kimsingi, watu wanatofautiana kwa mambo mengi sana, lakini kanuni hizi zinaweza kutumika ili kuheshimu na kuwawajibisha wanasiasa, ili kujizatiti katika kudumisha mafao ya wengi. Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu kudumisha upendo, kwa kukuza majadiliano, mshikamano na matumizi bora zaidi ya nguvu kazi. Amani duniani inahatarishwa sana kutokana na vitisho vya silaha za nyuklia. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, amani siyo tu kutokuwepo kwa vita, bali ni matunda ya haki, maendeleo, mshikamano, utunzaji bora wa mazingira pamoja na kusimamia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Huu ni wakati wa kusitisha vita katika kipindi hiki cha Juma Kuu na hatimaye Sherehe za Pasaka ya Bwana. Huo uwe ni mwisho na ukomo wa vita, kwa kuendelea kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hakuna ushindi unaoweza kusimikwa kwenye “magofu na makaburi ya watu” Baba Mtakatifu Francisko anasema, hakuna lisilowezakana mbele ya Mwenyezi Mungu. Rej. Lk 1:37. Ni Mwenyezi Mungu ambaye ataweza kusimamisha vita inayoendelea huko Ukraine, ambayo kwa sasa inaonkena kana kwamba, inaendelea kushika kasi ya ajabu na madhara yake kusambaaa kama “moto wa nyika.” Ni vita ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuendelea kusali ili kuombea amani duniani.

Hakuna ushindi unaosimikwa kwenye makaburi na vifusi vya majengo.
Hakuna ushindi unaosimikwa kwenye makaburi na vifusi vya majengo.

Alhamisi Kuu, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu endelevu ya siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha ushuhuda wa upendo na uwepo wake, unaobubujika kutoka katika Ekaristi Takatifu. Hii ni kumbukumbu ya uwepo wake kati pamoja na waja wake. Kristo Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeichukua dhambi ya walimwengu. Kwa Mwili na Damu yake Azizi amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu aliteswa na kufa Msalabani kwa sababu ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na sadaka yake Msalabani imekuwa ni chombo cha ukombozi wa binadamu wote!

Ijumaa Kuu ni siku ya toba, kufunga, kusali na kutafakari Maandiko Matakatifu, ili kushiriki Njia ya Msalaba na hatimaye, kusimama chini Msalaba ili kuadhimisha: mateso na kifo cha Kristo Msalabani kinacholeta wokovu kwa binadamu. Ni siku ya kumwabudu Kristo aliyeteswa na hatimaye kulazwa Msalabani kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Ni siku ya kuonesha mshikamano wa udugu wa upendo kwa: wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa na kutelekezwa pembezoni mwa jamii. Ni siku ya kuwakumbuka wahanga wa vita, ghasia na watoto waliotolewa mimba. Mbele ya Msalaba wa Kristo Yesu, waamini wanahimizwa kuwakumbuka na kuwaombea, wale wote wanaoelemewa ni Misalaba ya maisha, ili waweze kuonja huruma na faraja kutoka kwa Kristo Yesu. Mateso, Madonda Matakatifu na kifo cha Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma ya upendo wa Mungu unaomwagilia na kulainisha “majangwa ya nyoyo za binadamu”. Ni mwanga unaofukuzia mbali giza katika maisha ya waamini. Hili ni giza la vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia.

Ni giza la watoto wanaoteseka na kufariki dunia kwa baa la njaa na utapiamlo; kwa kukosa fursa za elimu na tiba. Ni giza la watu wanaoteseka kutokana na mashambulizi pamoja na vitendo vya kigaidi; watu wanaotumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, inayokumbatia utamaduni wa kifo! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, amekuwa ni chemchemi ya toba, msamaha wa dhambi na mwanzo wa maisha mapya kwa kutambua kwamba, binadamu anapendwa na kuthaminiwa na Mungu. “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa”. 1 Pet 2:24. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, asiwepo tena mtu anayetembea katika giza la mauti na kifo. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi katika nyoyo zao, ili aweze kuwaongoza.

Jumamosi Kuu, ni siku ya kimya kikuu na majonzi! Mitume waliokuwa wameweka matumaini yao kwa Kristo Yesu, walipoona jinsi alivyoteswa, akasulubiwa na kufa Msalabani, walivunjika moyo na kutawanyika. Wakajisikia kuwa ni watoto yatima na kuona kana kwamba, hata Mwenyezi Mungu “amewageuzia kisogo”. Jumamosi kuu ni Siku ya kuomboleza na Bikira Maria, lakini mwingi wa upendo na ujasiri, kiasi cha kuthubutu kufuata Njia ya Msalaba hadi kusimama chini ya Msalaba na hatimaye, kupokea maiti ya Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Hapa dunia inaonekana kusimama na kifo kushika mkondo wake! Lakini, Bikira Maria aliendelea kukesha kwa imani, matumaini na mapendo makuuu. Bikira Maria aliyegubikwa kwa giza nene la kifo cha Mwanaye, akageuka kuwa ni Mama wa waamini na Mama wa Kanisa, alama ya matumaini. Ushuhuda wake ni nguzo thabiti, pale waamini wanapoelemewa na Msalaba wa maisha.

Kesha la Pasaka ni Mama ya Mikesha Yote ya Kanisa.
Kesha la Pasaka ni Mama ya Mikesha Yote ya Kanisa.

Mkesha wa Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Kanisa. Huu ni Usiku ambamo Sifa za Mshumaa zinatangazwa wakati wa Mbiu ya Pasaka.  Wimbo wa Aleluiya Kuu unasikika, kielelezo cha imani ya waamini wanaokutana na Kristo Mfufuka. Waamini wataendelea kumshangilia Kristo Mfufuka kwa muda wa Siku 50, hadi Sherehe ya Pentekoste. Kristo Mfufuka anapenda kuwahakikishia waja wake kwamba, uzuri utashinda ubaya; maisha “yatapeta” dhidi ya utamaduni wa kifo! Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Mtakatifu Maria Magdalena alikuwa ni mfuasi wa kwanza wa Yesu kuona na kushuhudia kwamba, amefufuka kwa wafu. Baba Mtakatifu Francisko hapa anauliza swali la “kizushi kidogo”, Je, wale askari waliokuwa wameambiwa kulinda kaburi, kweli hawakumwona Kristo Mfufuka? Lakini, wakaamua kukaa kimya, kwa sababu walikula rushwa, wakafumbwa midomo na fedha kiasi cha kubadili ukweli wa mambo. Hata leo hii, rushwa inaendelea ili kunyamazisha ukweli, lakini iko siku ukweli huu utajulikana tu!

Papa Mafumbo ya Wokovu
12 April 2022, 15:41

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >