Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la “Mshikamano wa Kimataifa wa Utatu Mtakatifu” Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la “Mshikamano wa Kimataifa wa Utatu Mtakatifu”  

Lindeni Utu Na Haki Msingi Za Wanaotumbukizwa Katika Utumwa mamboleo!

Papa amelishukuru Shirika kwa kusimama kidete kwa vitendo kulinda uhuru wa kidini; amekazia umuhimu wa utume wao mintarafu Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa pamoja na kuendelea kumwilisha Karama ya Shirika kwa kusoma alama za nyakati na pale inapowezekana washirikiane na Taasisi nyingine. Wasithubutu kuchakachua Karama ya mwanzilishi wa Shirika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitangaza “declarat” kwamba, binadamu anayo haki ya uhuru wa dini. Uhuru huo ndio huu, kwamba, kila binadamu lazima akingiwe na shurutisho la mtu mmoja mmoja, la makundi ya kijamii, au la mamlaka yoyote ya kibinadamu. Hivyo kwamba, katika mambo ya dini mtu yeyote asishurutishwe kutenda dhidi ya dhamiri yake, wala asizuiliwe, katika mipaka inayokubalika kutenda kulingana na dhamiri yake binafsi au hadharani, peke yake au katika muungano na wengine. Haki ya uhuru wa dini msingi wake ni hadhi ya binadamu ijulikanayo kwa njia ya Neno la Mungu lililofunuliwa na ya akili. Haki hii ya binadamu ya uhuru wa dini yatakiwa kuzingatiwa katika sheria za jamii ili iwe haki ya raia. Rej. DH 2. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulizingatia hasa: mema ya kiroho kwa kila mtu; ukweli na haki; Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa. Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kanisa linawajibu wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, linahimiza umuhimu wa kulinda dhamiri nyofu pamoja na wajibu wa kimaadili.

Simameni kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu
Simameni kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba: wanaendeleza Mafundisho ya Kanisa kuhusu haki msingi za binadamu zisizoondosheka na katika sheria za muundo wa jamii. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufunda dhamiri za watu, ili kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. DH.1. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 amekutana na kuzungumza na washiriki wa Kongamano la “Mshikamano wa Kimataifa wa Utatu Mtakatifu” lililoandaliwa na Shirika la Utatu Mtakatifu, O.SS.T. “L'Ordine della Santissima Trinità” kwa Kilatini: Ordo Sanctissimae Trinitatis” lililoanzishwa kunako mwaka 1193 na Mtakatifu Giovanni de Matha (1154-1213) na kuidhinishwa na Papa Innocent III tarehe 17 Desemba 1198 kwa waraka wake wa “Operante Divine Dispositionis.”

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amelishukuru Shirika kwa kusimama kidete kwa vitendo kulinda uhuru wa kidini; umuhimu wa utume wao katika ulimwengu mamboleo mintarafu Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa pamoja na kuendelea kumwilisha Karama ya Shirika kwa kusoma alama za nyakati na pale inapowezekana washirikiane na Taasisi nyingine, lakini kamwe wasithubutu kuchakachua Karama ya mwanzilishi wa Shirika. Baba Mtakatifu analipongeza Shirika ambalo limeendelea kusimama kidete kwa matendo, kwa kuwahudumia watu wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao. Shirika limekuwa mstari wa mbele kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa uhuru wa kidini, kiasi hata cha Mtakatifu Giovanni de Matha (1154-1213) kutambuliwa na kupewa heshima kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Toma wa Akwino, maarufu kama Angelicum kilichoko mjini Roma. Karama ya Mtakatifu Giovanni de Matha ni zawadi ya Roho Mtakatifu iliyomwezesha kuwa shuhuda, ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kwenye Karne ya Nane, nyakati za Mtakatifu Francisko wa Assisi. Akajitosa kushiriki katika mchakato wa ukombozi wa watu waliokuwa wametumbukizwa katika biashara ya utumwa mkongwe. Akaanzisha Shirika ambalo lingeweza kutekeleza dhamana na utume wake, sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuwaokoa watu waliokuwa wametumbukizwa kwenye biashara ya utumwa.

Karama ya Mwanzilishi wa Shirika Idumishwe daima isichakachuliwe hata kidogo
Karama ya Mwanzilishi wa Shirika Idumishwe daima isichakachuliwe hata kidogo

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukombozi ni kati ya shughuli zilizotekelezwa na Kristo Yesu katika hatua zile za mwanzo za maisha yake ya hadhara. Alianza kwa kusema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Lk 4: 18-19. Huu ni utume unaotekelezwa katika ushiriki mkamilifu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayelitakatifuza Kanisa. Shirika hili kwa maisha na utume wake, limewaokoa watu waliokuwa wanakandamizwa kwa kongwa la utumwa. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, utumwa mkongwe umekomeshwa duniani, lakini leo hii, kumeibuka tena utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anaangalisha juu ya mabadiliko makubwa ambayo yamejitokeza katika historia ya mwanadamu kwa kutambua utu na heshima ya binadamu na kwamba, utumwa ni kitendo kinachodhalilisha na kufisha utu na heshima ya binadamu; jambo ambalo limepelekea utumwa kupigwa marufu kutoka katika uso wa dunia na kwamba, ni marufuku mtu kuingizwa katika utumwa, sheria ambao bado inaacha maswali mengi bila ya kuwa na majibu muafaka. Baba Mtakatifu anasema hata leo hii, kuna watu wanalazimika kuishi katika mazingira ya utumwa, kwani kuna mifano hai inayoonesha kwamba, kuna watu wanafanyishwa kazi za kitumwa; wahamiaji wananyimwa haki zao msingi.

Kuna watu wanadhulumiwa na kunyanyaswa; wanawekwa kizuizini katika mazingira hatarishi; wananyanyaswa na kudhulumiwa na waajiri kwa kudhibiti mikataba na vibali vya kuishi ugenini. Kuna wanawake, wasichana na watoto ambao wametumbukizwa katika biashara haramu ya ngono; wengine wanauzwa kama biadhaa na kulazimishwa kufunga ndoa za shuruti. Kuna baadhi ya watu wanatumbukizwa katika biashara haramu ya viungo vya binadamu; watoto wanapelekwa mstari wa mbele kama chambo katika mapigano ya kivita; kuna baadhi ya watoto wanaolazimishwa kuuza dawa haramu za kulevya na wengine wanaasiliwa kinyume cha sheria za kimataifa. Kuna baadhi ya watu wametekwa nyara na kufungwa na vikundi vya kigaidi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba kuna ukatili unaoendelea kushika kasi sehemu mbalimbali za dunia. Ni wajibu na dhamana yao kama wanashirika kushirikiana na Taasisi mbalimbali kulinda na kutetea uhuru wa kuabudu lakini kamwe wasithubutu kuchakachua Karama ya mwanzilishi wa Shirika, bali waendelee kujikita katika mchakato wa ujenzi wa “Mshikamano wa Kimataifa wa Utatu Mtakatifu.”

Utumwa mamboleo
27 April 2022, 14:15