Tafuta

Papa Dominika ya Matawi Juma Kuu: Huruma Na Msamaha

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi katika sehemu ya Injili inayoonesha Kristo Yesu akisulubiwa Msalabani: “Kama wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.” Yesu alijibu shutuma zote hizi kwa kusema: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Rej Lk 23:33. Juma Kuu ni Wakati wa kuona huruma na msamaha wa dhambi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Matawi, tarehe 10 Aprili 2022 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amebariki matawi na baadaye kuongoza maandamano kuelekea katika maadhimisho ya Misa ya Mateso ya Bwana. Kwa hakika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulipambwa kwa mafuriko ya waamini na watu wenye mapenzi mema. Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amejikita zaidi katika sehemu ya Injili inayoonesha Kristo Yesu akisulubiwa Msalabani: “Kama wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.” Lakini Kristo Yesu alijibu shutuma zote hizi kwa kusema: “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Rej Lk 23:33. Watesi wa Yesu walimtaka azame zaidi katika uchoyo na ubinafsi kwa kujali afya yake, mafanikio, mafao binafsi, madaraka na hata mwonekano wake. Haya ni mambo msingi ya kuyafanyia tafakari ya kina wakati huu Mama Kanisa anapoanza kuadhimisha Juma Kuu, kiini cha Liturujia yote ya Kanisa. Mawazo ya kumtaka Kristo Yesu ajiokoe mwenyewe kwa kuzama katika ubinafsi ni kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu. Katika sehemu hii ya Injili Kristo Yesu anajibizana na wale walioteswa pamoja, kwa kumwombea na kumsamehe yule mhalifu aliyekuwa amesulubishwa pamoja naye. Badala ya kujiokoa mwenyewe, Kristo Yesu anawaombea wote msamaha kwa sababu hawajui watendalo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ulikuwa ni muda wa mateso makali wakati Kristo Yesu alipokuwa anasikia kabisa misumari ikiingia mwilini, lakini bado aliwaombea watu msamaha. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu ni tofauti kabisa na Simulizi nyingine za Kibiblia zinazoonesha maongozi ya Mungu katika madhulumu.

Dominika ya Matawi Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Dominika ya Matawi Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mashuhuda wa Agano la Kale, waliwakaripia watesi wao kwa maneno makali, lakini Kristo Yesu, anasali na kuwaombea kwa Baba yake wa mbinguni. Rej. 2 Mk 7:18-19. Akiwa ametundika Msalabani, kielelezo cha sadaka yake kuu, anakuwa pia ni chemchemi ya huruma na msamaha. Huu ni mwaliko kwa waamini hata katika mateso na mahangaiko makali kujifunza kusamehe na kusahau. Msalaba wa Kristo uwe ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha shukrani, huruma, upendo na msamaha. Ni fursa ya kujifunza kupenda na kusamehe na hasa zaidi kuwapenda na kuwasamehe adui, kama sehemu ya utekelezaji wa Amri ya Kristo Yesu ya kuwapemda na kuwaombea adui. Baba Mtakatifu anakiri kabisa kwamba, hii ni Amri ngumu sana kuweza kutekelezwa, hasa kutokana na madonda, makovu na ubaya ambao wametendewa. Kristo Yesu anawaalika waamini kupiga moyo konde na hivyo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu, kwani Mwenyezi Mungu anawatambua watu wote kuwa ni watoto wake, wala hakuna tofauti kati yao yaani wema na wabaya, wote ni “mali na watoto wapendwa wa Mungu, anawapenda upeo na kuwakumbatia; na anataka kuwasamehe. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza ikiwa kama wanafuata kikamilifu nyayo za Kristo Yesu, Mwalimu wao au wanafuata hisia zao wenyewe? Waamini watambue kwamba, wanapendwa na kusamehewa!

Kwa njia ya mateso na kifo cha Kristo Msalabani, ameweza kuwakirimia wanadamu msamaha na maondoleo ya dhambi na kwamba, kamwe Mwenyezi Mungu hachoki kusamehe na kusahau. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu amewaletea waja wake msamaha wa dhambi na kuwataka kwenda ulimwenguni kote kuwahubiria watu Habari Njema ya Wokovu, toba na ondoleo la dhambi. Rej. Lk 24:47. Waamini, kamwe wasichoke kupokea msamaha wa Mungu katika maisha yao, utume unaotekelezwa na Mapadre kwa waamini, wanaopokea na hatimaye kuutolea ushuhuda katika uhalisia wa maisha yao. Kristo Yesu anawaombea watesi wake msamaha kwa sababu hawajui watendalo na hivyo kugeuka kuwa wakili na mtetezi wa wadhambi. Kwa wale wanaowatenda wengine jeuri na ukatili wana tabia ya kumsahau Mwenyezi Mungu na kwamba, hao wanaowatesa ni ndugu zao. Haya ndiyo yanayotendeka wakati wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, vitendo vinavyoendeleza mateso na dhuluma dhidi ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu anaendelea kutundikwa Msalabani, kwa wanawake wanaowalilia watoto wao wanaoendelea kuuwawa kutokana na vita na ushuhuda wa imani unaotolewa na watoto wao. Kristo Yesu anateseka kati ya wakimbizi na wahamiaji; kati ya akina mama wanaolazimika kuyakimbia makazi yao huku wakiwa wamewabeba watoto wao wadogo. Kristo Yesu anateseka miongoni mwa wazee waliotelekezwa katika upweke hasi, kiasi cha kufariki dunia katika hali ya upweke. Kristo Yesu anateseka kati ya vijana wa kizazi kipya waliopokwa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kristo Yesu anateseka miongoni mwa wanajeshi wanaotumwa kwenda kuwauwa ndugu zao.

Dominika ya Matawi: Huruma, Upendo na Msamaha wa Mungu
Dominika ya Matawi: Huruma, Upendo na Msamaha wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuiga mfano wa yule mhalifu aliyeguswa na maneno na huruma ya Kristo Yesu pale juu Msalabani, kiasi hata cha kuchipua ndani mwake matumaini mapya yaliyomwezesha kusema: “Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.” Lk 23: 42-43. Hiki ndicho kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu inayomwongoa yule aliyekuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, kuandika historia ya kwanza kwa kutangazwa kuwa ni Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini katika maadhimisho ya Juma Kuu kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anaweza kusamehe kila ubaya na dhambi na hivyo kumwezesha mwamini kumtukuza, kumsifu na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Rej. Zab 30: 12. Waamini wakumbuke kwamba, katika maisha na utume wa Kristo Yesu, kila mtu anayo nafasi yake, Yeye ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, nyakati zote ni zake na wala hakuna kuchelewa. Kwa kumtumainia Mungu, mwanadamu anaweza kupata nafasi ya kufufuka na kuendelea tena kuishi. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatia shime waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea na hija inayoelekea kwenye Sherehe za Pasaka huku wakiwa na ujasiri unaosimikwa katika msamaha wa Kristo Yesu kwani anaweza kuwaokoa wale wote wanaomwendea, kwa maana yu hai siku zote, ili awaombee. Rej. Ebr 7: 25. Kristo Yesu anapouangalia ulimwengu huu uliochoka na kuelemewa na vita, hachoki kusema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.” Rej. Lk 23:33.

Papa Matawi

 

 

10 April 2022, 13:43

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >