Papa Francisko Atia Nia Kutembelea Kazakhstan Mwezi Septemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 26 Oktoba 1986, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa aliwakutanisha viongozi wa dini mbalimbali huko mjini Assisi, nchini Italia, kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani! Mkutano huu, ukawa ni chachu ya kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kudumisha amani duniani. Sala na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku ni nyenzo msingi ya ujenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Miaka 25 baadaye, aliwataka waamini wa dini mbalimbali duniani kuendeleza roho na moyo wa sala kutoka Assisi kwa kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na maridhiano. Alikazia umuhimu wa vijana kufundwa utamaduni wa haki na amani na kwamba, majadiliano ya kidugu ni muhimu sana katika kukuza haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ametia nia ya kushiriki katika Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani litakaloadhimishwa mjini Kaza, Nur Sultan huko nchini Kazakhstan mwezi Septemba 2022. Kongamano hili linanogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Mapokeo katika mchakato wa maendeleo kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hayo yamethibitishwa na Dr Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican mara baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza kwa njia video na Rais Kassym-Jomart Tokayev wa Kazakhstan, Jumatatu tarehe 11 Aprili 2022. Kongamano la Kwanza la Viongozi wa Dini Duniani liliadhimishwa kunako Januari 2002 mjini Assisi, Italia, kwa mwaliko wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Lengo lilikuwa ni kuendelea kuimarisha mchango wa dini mbalimbali katika kukuza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa njia ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Hii ni kutokana na kinzani kubwa zilizoibuka miongoni mwa waamini wa dini mbalimbali duniani, baada ya shambulizi la kigaidi lililofanyika nchini Marekani tarehe 11 Septemba 2001.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” uliozinduliwa rasmi tarehe 4 Oktoba 2020, unagusia magonjwa jamii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; mshikamano wa udugu wa kibibadamu; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waraka huu umekuwa ni rejea makini katika mchakato wa kuganga na kuponyesha madonda yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Ujenzi wa ulimwengu mpya ni mchakato wa watu wote wa Mungu unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani duniani. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yasaidie kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Amani ya kweli inajengwa katika msingi wa maendeleo fungamani ya binadamu: kiroho na kimwili; kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni sehemu ya hali halisi ya maisha ya binadamu yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa kujikita katika kanuni maadili, sheria za kimataifa sanjari na ujenzi wa siasa ya amani duniani inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani; upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, majadiliano pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; uhuru pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa iwekeze katika uchumi fungamani unaojali na kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, utu na heshima yake!