Papa Francisko Asikitishwa na Maafa ya Kimbunga Cha Megi Nchini Ufilippini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Taarifa kutoka nchini Ufilippini zinaonesha kwamba, Kimbunga cha Megi kinachojulikana pia kama Agaton, kilicho ikumbuka nchi ya Ufilippini, Jumatano tarehe 13 Aprili 2022 kimesababisha watu zaidi 123 kufariki dunia baada ya kufukiwa na maporomoko ya udongo na kwamba, idadi hii, inahofiwa kuongeza maradufu. Watu 236 wamejeruhiwa vibaya na kwamba, kuna idadi ya watu kadhaa ambao hawajulikani mahali walipo. Serikali inasema kwamba, sekta ya kilimo imeharibiwa vibaya sana na mafuriko na kwamba, hadi sasa hasara inakadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 8. Maeneno yaliyoathirika vibaya ni pamoja na mikoa ya Magharibi ya Visayas na ile ya Mashariki ni Visayas na Caraga.
Kuna vijiji ambavyo vimefutika kabisa baada ya kukumbukwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya udongo. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa viongozi wa Serikali na Kanisa nchini Ufilippini kutokana na maafa makubwa yaliyosabishwa na Kimbunga cha Megi kinachojulikana pia kama Agaton. Katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikisha uwepo wake wa karibu wale wote waliofikwa na maafa haya. Anawaombea wale waliofariki dunia, wapate rehema na wapumzike kwa amani. Majeruhi waweze kupona haraka ili hatimaye, waweze kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Mwishoni, anawaombea nguvu na amani, watu wote wa Mungu nchini Ufilippini walioguswa na kutikiswa na kimbunga hiki.