Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, amempongeza Askofu Msaidizi Methodius Kyabonaki Kilaini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, amempongeza Askofu Msaidizi Methodius Kyabonaki Kilaini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre.  

Papa Francisko Ampongeza Askofu Msaidizi Kilaini, Miaka 50 ya Daraja Ya Upadre

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, amempongeza Askofu Msaidizi Methodius Kyabonaki Kilaini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu amesema, katika maisha na utume wake, Askofu Msaidizi Kilaini amejitoa bila ya kujibakiza katika huduma kwa Mungu na jirani kama Padre na Askofu, kama inavyoshuhudiwa na watu wa Mungu Tanzania.

Na Remigius Mmavele, -Bukoba, Tanzania.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja takatifu ya Upadre ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka ya kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, amempongeza Askofu Msaidizi Methodius Kyabonaki Kilaini kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Baba Mtakatifu amesema, katika maisha na utume wake, Askofu Msaidizi Kilaini amejitoa bila ya kujibakiza katika huduma kwa Mungu na jirani kama Padre na Askofu, kama inavyoshuhudiwa na watu wa Mungu nchini Tanzania. Baba Mtakatifu amemtakia heri na baraka tele katika maisha na utume wake, ili kuendeleza kazi ya ukombozi. Salam na matashi mema yaliyosomwa na Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 19 Machi 2022 sanjari na Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria.

Shukrani kwa Jubilei ya Miaka 50 ya Daeaja Takatifu ya Upadre.
Shukrani kwa Jubilei ya Miaka 50 ya Daeaja Takatifu ya Upadre.

Katika maadhimisho haya, Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, akishirikiana na familia ya Mungu nchini Tanzania na kwa namna ya pekee Jimbo Katoliki la Bukoba, amempongeza Askofu Msaidizi Kilaini kwa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre na kwamba, anatambua pia utume wake wa Kiaskofu. Maadhimisho haya ni sehemu ya kumbukumbu endelevu ya matukio mbalimbali yaliyopita katika maisha na utume wake katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita. Anamtaka awe na moyo wa shukrani kwa kila jambo na kwamba, ataendelea kumkumbuka na kumwombea, ili Mwenyezi Mungu azidi kumwiimarisha katika maisha na utume wake na Bikira Maria amsimamie katika utekelezaji wa shughuli zake za kichungaji. Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba, alimpongeza sana Askofu Msaidizi Methodius Kilaini kwa maisha na utume wake. Ni Askofu ambaye ameonesha Ibada kwa Bikira Maria na hivyo kutumia karama na mapaji yake kwa ajili ya kumtangaza na kumweneza kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii ndani na nje ya Tanzania. Amesaidia kuboresha elimu na utume wa Mapadre Jimboni Bukoba. Kwa ufupi, ni Askofu ambaye anaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Bukoba: kiroho, kimwili na kiutu.

Askofu Msaidizi Methodius Kilaini amewasihi watu wa Mungu mkoa wa Kagera kudumisha umoja, mshikamano na upendo, ili kunogesha ustawi, maendeleo na mafanikio ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Ni mwaliko wa kuondokana na chuki, mtimanyongo na mafarakano yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa watu wa Mungu mkoani Kagera. Ibada ya Masifu iliadhimishwa katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma na kuongozwa na Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo Katoliki Bunda huku yakihudhuriwa na Maaskofu Katoliki, Mapadre naWatawa wa kike na Kiume waliojumuika na Majandokasisi kutoka Seminari kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba pamoja na waamini na watu wenye mapenzi mema. Mgeni rasmi katika Jubilei hii alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango aliyeambata na mke wake Mama Mbonimpaye Mpango pamoja na baadhi ya viongozi wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kushukuru kwa mchango wa Askofu Kilaini katika Kanisa na pia kwa jamii ya Watanzania. Amemtaja Askofu Kilaini kama   miongoni mwa waanzilishi wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini (1994) ambayo imeimarisha maridhiano miongoni mwa waamini wa dini na madhehebu mbalimbali hapa nchini Tanzania. Aidha amelipongeza na kulishukuru Kanisa Katoliki kwa kuunga mkono juhudi za Serikali na kwa kutoa mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya Watanzania: kiroho, kiuchumi na kijamii. Amesema Kanisa limeweza kufikisha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo yale ambayo Serikali bado haijaweza kufikisha huduma hususani vijijini na maeneo wanakoishi watu wa hali ya chini mijini.

Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 22 ya Uaskofu, matendo makuu ya Mungu
Miaka 50 ya Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 22 ya Uaskofu, matendo makuu ya Mungu

Aidha Makamu wa Rais amelipongeza Kanisa kwa kuendelea kuhudumia yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Makamu wa Rais amesema serikali imejielekeza katika kuboresha na kujenga miundombinu ya usafiri na usafirishaji, miundombinu ya Elimu, Afya na Maji katika mkoa wa Kagera ili kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na uchimbaji wa madini kama mgodi wa Nikel Kabanga na kufungua fursa za biashara na ajira hivyo kuwaasa wananchi wa Kagera kutumia fursa hizo kukuza uchumi wao. Dkt. Mpango ameliasa Kanisa kufundisha na kulea vijana katika maadili na utu wema sanjari na kuthamini kufanya kazi halali kwa juhudi na maarifa. Amesema katika nyakati hizi, kuna ongezeko la mmong’onyoko mkubwa wa maadili katika jamii ikiwemo ulevi, vitendo vya rushwa, uvivu, wizi na ufisadi, mauaji ya kutisha na idadi kubwa ya ndoa kuvunjika na kuongezeka kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Pia Makamu wa Rais amewaasa viongozi wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine yote ya kidini kupaza sauti kuhamasisha usafi, ulinzi na uhifadhi bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kwa upande wake Askofu Msaidizi Methodius Kilaini ameishukuru serikali kwa ushirikiano iliyompatia kwa kipindi chote cha miaka hamsini ya utumishi wake. Aidha amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mwaka mmoja wa uongozi wake wenye mafanikio makubwa na kazi nzuri alioifanya. Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan taifa limeongozwa kwa utu, amani na mshikamano wa udugu pamoja na hatua mbalimbali za maendeleo fungamani kwa wananchi wa Tanzania. Askofu Kilaini amewashukuru watu wa Mungu Mkoa wa Kagera kwa kushirikiana naye wakati wote wa utumishi wake na kuwaombea kuendelea kuimarisha: umoja, upendo na kuendelea kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa, ili kunogesha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu mkoani Kagera.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba, alizaliwa tarehe 30 Machi 1948 huko Katoma, Bukoba. Ni Mtoto wa Ta Paulo Mutegeki na Ma Asteria Kokutona Balilonda wa Katoma Kyamtwara Jimboni Bukoba. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 18 Machi 1972 akiwa na umri wa miaka 24 akapewa daraja Takatifu ya Upadre na Kardinali Agnelo Rossi. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 22 Desemba 1999 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu tarehe 18 Machi 2000 na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisaidiana na Hayati Askofu Nestorius Timanywa wa Jimbo Katoliki la Bukoba pamoja na Hayati Askofu Justin T. Samba wa Jimbo Katoliki la Musoma. Tarehe 5 Desemba 2009, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Kumbe, Askofu Msaidizi Methodius Kilaini anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, anamshukuru Mungu kwa miaka 22 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu Msaidizi.

Askofu Kilaini
04 April 2022, 14:36