Papa asikitika kwa kifo cha rafiki Barragán:Maisha yake katika huduma ya Mungu na Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko amemkubuka Kardinali wa Zacatecas, Mexico Javier Lozano Barragán, Rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Wahudumu wa Kiafya (Kwa ajili ya uchungaji wa kiafya) la wakati huo na leo hii ni Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu, aliyeaga dunia, Jumatano asubuhi tarehe 20 Aprili 2022, akiwa na umri wa miaka 89, jijini Roma. Katika telegramu ya rambi rambi aliyomtumia Askofu wa Zamora jimbo lake asili, Askofu Javier Navarro Rodríguez Papa amesema marehemu alikuwa mwaminifu na alimpa heshima ya kuwa na urafiki tangu 1980 na kwamba kwa miaka hiyo na uaminifu wake alitoa maisha yake kwa ajili ya huduma ya Mungu na Kanisa lote la ulimwengu. Papa Francisko anatoa salamu za rambi rambi kwa askofu wa jimbo, maaskofu, watawa na waamini walei wa Kanisa mahalia wa Zamora pia kwa watoto wa ndugu zake na ndugu wa Marehemu Lozano Barragán, na Makanisa ya Mexico na Zacatenas mahali ambapo aliweza kuhudumia kama mchungaji. Papa Francisko ameandika akimwombea ili roho ya rafiki yake iweze kupumzika kwa amani, na Bwana Yesu amvishe taji la utukufu ambalo halinyauki. Kufuatia na Kifo cha Kardinali huyo, Baraza la Makardinali kwa sasa linaundwa na makardinali 210 ambapo 117 wanaweza kuchagua na 93 hawawezi kuchaguliwa.
Kardinali Lozano Barragán, alizaliwa mnamo tarehe 26 Januari 1933 huko Toluca, Mexico. Majiundo yake ya kikuhani katika seminari ya kijimbo ya Zamora na kupewa daraja la upadre tarehe 30 Oktoba 1955. Baadaye aliendelea na masomo katika chuo Kikuu cha Gregoriana, Roma, kwa kuhitimisha na shahada na Udaktari wa Taalimungu ya Kidogmatiki na kurudi nchini kwao Mexico na miaka sitini akaendelea na shughuli kama rais wa Jamii wa Chama cha Kitaalimungu huko Mexoco, kwa maana hiyo taasisi ya Kitaalimungu kichungaji ya Baraza la Maaskofukofu barani Amerika Kusini Celam). Aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi mnamo mwaka 1979 hadi 1984 kwa kujikita katika shughuli za kichungaji Jimbo Kuu la Mexico na katika miaka hiyo ni mmoja wa waanzilishi wa Taasisi ya Kipapa ya Chuo Kikuu cha Mexico kwa kujikita na shughuli ukatibu mkuu wa Sinodi kuhusu familia 1980. Upyaishaji wa wakleri, miundo ya jimbo, mazungumzo na utamaduni ndio kitovu cha huduma yake katika miaka hiyo akiwa mkuu wa jimbo la Zacatecas (1985-1997). Katika kipindi hiki, ahadi katika huduma ya Kitakatifu iliongezeka. Kunako mwaka 1988 akawa mjumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano na Wasioamini, ambalo baadaye lilikuja kuwa Baraza la Kipapa la Utamaduni, ambapo kunako mwaka 1989 alikuwa sehemu ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na mwaka 1997 akawa Mshauri wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Bara la Amerika Kusini, hadi 2000 alipokuwa mjumbe wa Baraza la Kipapa la Maaskofu.
Mwaka 1996 Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa rais wa Baraza la Kipapa la Wafanyakazi wa Huduma za Afya, nafasi ambayo ikamfanya aliteuliwa kuwa askofu mkuu. Mtakatifu Yohane Paulo II pia alimtangaza kuwa Kardinali katika baraza Makardinali mnamo tarehe 21 Oktoba 2003 na Aprili 2005 alishiriki katika mkutano uliomchagua Papa Benedikto XVI. Alistafu utumishi wake mwaka 2009, wakati Kardinali anakuwa rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Wafanyakazi wa Afya la wakati huo ambalo baadaye lilibadilishwa. Miaka michacheiliyopita, mnamo Agosti 2019, Kadinali Lozano Barragán alisherehekea miaka yake 40 ya huduma ya kiaskofu huko Mexico, pamoja na marafiki na familia. Alikuwa ameongoza Misa katika Madhabahu ya Mama Yetu wa Guadalupe, katika Jimbo la Zamora, na katika jimbo la Michoacán, ambako alitokea. Akitafakari juu ya miaka iliyopita na hatua zilizowatofautisha, alijumlisha kila kitu, mwishoni mwa hotuba yake, na neno zawadi: “Kila kitu kilikuwa zawadi hadi sina kitu cha kujivunia tena. Na sasa ninaitoa. Nimekuwa nikijaribu kwa miaka 9 kutoa kila kitu ambacho Bwana alinipatia hapo awali. Alinipa, na sasa sina budi kuitoa, nikiandika, nikishiriki uzoefu uliojengwa juu ya misingi ya kile kilichokuwa na ni jimbo langu pendwa la asili, la Zamora”.