Papa amekutana na Waziri Mkuu wa Hungary:wametazama suala la wakimbizi wa Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Francisko Alhamisi tarehe 21 Aprili 2022 ametumia dakika kama 40 hivi na Bwana Viktor Orbán, Waziri Mkuu wa Hungary, ambaye alikutana naye mjini Vatican. Waziri Mkuu aliwasili Vatican muda mfupi kabla ya saa 5.00 asubuhi, akifuatana na mkewe na wasaidizi wake na hakukutana na mamlaka nyingine za Vatican kutokana na hali ya faragha ya ziara yake. Waziri Orbán yuko katika safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuchaguliwa tena kama mkuu wa serikali yake mnamo tarehe 3 Aprili 2022. Kabla ya kuja Roma Waziri Orbán mwenyewe alikuwa ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba: “Safari yangu ya kwanza rasmi baada ya uchaguzi itanipeleka jijini Vatican, kwa Papa Francisko”.
Katika mazungumzo yao kati ya viongozi hao wawili Papa Franciko na Waziri Mkuu katika Maktaba ya Kitume yalifanyika mbele ya mkalimani, lakini akizungumza kwa Kiingereza, Papa alimbariki Bwana Orbán, familia yake, na nchi nzima ya Hungary, ambayo kwa sasa inajishughulisha na kutoa hifadhi kwa watu wa Ukraine jirani wanaokimbia vita. Waziri Mkuu alijibu kwa Kiingereza na maneno haya: “Tunakusubiri,” akimaanisha kumpa mwaliko Papa kutembelea nchi ya Hungaria. Na akiwa kando ya mkutano wao, msemaji wake, Zoltan Kovacs, alisema Orbán alimwomba Papa Francisko kuunga mkono juhudi zao za kuleta amani.
Zawadi
Zawadi kadhaa zilitolewa na Waziri Orbán kwa Papa: vitabu viwili, na Béla Bartók, mtunzi wa Hungaria na mtaalamu wa muziki. “Ikiwa unataka sikiliza”, alisema kiongozi huyo wa kisiasa. Baadaye akamkabidhi mkusanyo wa rekodi za muziki wa liriki na juzuu ya 1750 ya Ofisi ya Masifu ya Wiki Takatifu kwa lugha ya Kiingereza na Kilatini. Kwa upande wa Baba Mtakatifu amewapa zawadi ya mchoro wa shaba unaoonesha Mtakatifu Martin wa Tours, ambaye ni mzaliwa wa Pannonia, Hungaria ya sasa, katika kitendo na ishara ya kuwalinda maskini ambapo mtakatiu huyo alikata nusu ya sehemu ya vazi lake na kumfunika maskini. Na akimpatia zawadi hiyo Papa alitoa maoni yake kwamba: “Nilikuchagulia wewe, Mtakatifu Martin ambaye ni Hungaria, na nilifikiri kwamba ninyi Wahungaria mnapokea wakimbizi hawa wote hivi sasa”. Papa pia alitoa hati za kipapa kama kawaida yake: Ujumbe kwa Siku ya Amani ya Duniani mwaka huu, Hati juu ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini mnamo 2019 huko Abu Dhabi, na kitabu kilichochapishwa na LEV kwenye Statio Orbis mnamo tarehe 27 Machi 2020.