Padre Ni Shuhuda Wa Huruma Na Upendo Wala Si Mtu Wa Mshahara!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi kuu tarehe 14 Aprili 2022 baada ya kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amewazawadia kitabu wakleri waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu. Kitabu hiki kinajulikana kama: “Mashuhuda, na wala si Maafisa, Padre Ndani ya Mabadiliko ya Nyakati. “Testimoni, non funzionari. Il sacerdote Dentro il Cambiamento d’epoca (Libreria Editrice Vaticana, pp. 232, kinauzwa kwa bei ya Euro 16), Kimetungwa na Askofu François-Xavier Bustillo, wa Jimbo Katoliki la Ajaccio lililoko nchini Ufaransa na anatekeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu huko Lourdes, Ufaransa. Katika kitabu hii, Askofu François-Xavier Bustillo anazama zaidi kuhusu Daraja Takatifu ya Upadre, anapembua kwa kina na mapana taalimungu ya Daraja Takatifu ya Upadre pamoja na tasaufi yake.
Askofu François-Xavier Bustillo anamweka Padre na Kuhani wa Bwana, kama shuhuda na Mtumishi wa Mafumbo Matakatifu na wala si kama mtu wa mshahara au afisa kama wanavyojulikana na wengi. Padre ni shuhuda anayejibidiisha katika maisha na utume wake kumtafuta Mwenyezi Mungu. Mtunzi wa Kitabu hiki, anakitajirisha na tafakari makini kuhusu Daraja takatifu ya Upadre zilizowahi kutolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko, kwa kubainisha amana na utajiri wa kitaalimungu wa Daraja takatifu ya Upadre katika ulimwengu mamboleo unaoonekana kutaka kukita mizizi yake katika malimwengu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewakumbusha Wakleri kwamba, Upadre ni neema inayowawezesha kuwatumikia watu wa Mungu kwa kufundisha, kuongoza na kutakatifuza. Damu Azizi ya Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo na msamaha wake usiokuwa na masharti, changamoto na mwaliko wa kuwa waaminifu kwa Agano na kuendelea kukaza macho yao kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Baba Mtakatifu amewataka Mapadre kujiepusha kumezwa na malimwengu ya maisha ya kiroho; kuabudu namba au mwonekano wa nje na kamwe wasitekeleze utume wao kama watu wa mshahara na kutaka kujimwambafai na kujikweza. Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao kama Mapadre. Amana na utajiri wa mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu ya Kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu umebubujika kutoka katika Liturujia ya Neno la Mungu. Kwa mara ya kwanza kitabu hiki kilichapishwa kunako mwaka 2021 na Kampuni ya “Nouvelle Cité na kupewa jina “La vocation du prête face au crises. La fidélité créatrice.”