Tafuta

Kumbukizi la Miaka 8 tangu Yohane Paulo II kutangazwa kuwa ni Mtakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014 Kumbukizi la Miaka 8 tangu Yohane Paulo II kutangazwa kuwa ni Mtakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014 

Mtakatifu Yohane Paulo II: Miaka 8 Tangu Atangazwe Kuwa Mtakatifu

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa tarehe 27 Aprili 2022 anafanya kumbukizi ya miaka nane tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu. Mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa Yesu na Kanisa lake; kwa kutangaza na kushuhudia upendo wenye huruma ulimwenguni, katika maisha ya kifamilia na maeneo ya kazi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kunako mwaka 2020, Mama Kanisa ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Yohane Paulo II alipozaliwa. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Ametekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alifariki dunia hapo tarehe 2 Aprili, 2005.

Papa Mstaafu Benedikto XVI tarehe 1 Mei 2011 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri
Papa Mstaafu Benedikto XVI tarehe 1 Mei 2011 akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Mei Mosi, 2011 akamtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbu kumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wengi na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Ni katika kumbukizi hii, tarehe 27 Aprili 2022 wakati wa katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa, mwaka huu, anafanya kumbukizi ya miaka nane tangu Papa Yohane Paulo II alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kutangaza na kushuhudia upendo wenye huruma ulimwenguni, katika maisha ya kifamilia na maeneo ya kazi. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake. Neema hii ikamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kufanya hija za kitume 104 nje ya Italia. Akabarikiwa kufanya hija za kichungaji 142 nchini Italia, daima maneno yake yaliambatana na vitendo; akagusa na kufariji mamilioni ya watu duniani, huku akitangaza na kushuhudia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama kiini cha haki msingi za binadamu! Matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989. Kanisa likatoka kifua mbele na kusimama kidedea ili kupinga sera za kibaguzi zilizoigawa dunia, kati ya Kaskazini na Kusini: likaimarisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kujikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kama kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hija za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, zilikuwa ni sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa kimisionari katika kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wanawake ndani na nje ya Kanisa.

Papa Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI walifanya utume wao kwa ukaribu
Papa Yohane Paulo II na Papa Mstaafu Benedikto XVI walifanya utume wao kwa ukaribu

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai”; kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha.

Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Huduma shufaa itolewe kwa kuzingatia maboresho katika huduma ya afya. Injili ya uhai ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Wanasiasa wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.  Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata dira na mwongozo wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akaimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kiasi hata cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini sana mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake, mambo yanayojionesha hata katika Nyaraka zake za kichungaji “Mulieris dignitatem” yaani “Utu na wito wa mwanamke”. Alikazia sana umuhimu wa utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuthubutu kuwatangaza watakatifu wapya 482 na wenyeheri 1319, mwaliko na changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu kama chemchemi ya utakatifu na utimilifu wa maisha ya Kikristo.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa msamaha, huruma na upendo wa Mungu
Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa msamaha, huruma na upendo wa Mungu

Mtakatifu Yohane Paulo wa II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata nyakati hizi. Majadiliano kati ya Mtakatifu Yohane Paulo II na vijana wa kizazi kipya, waliompenda upeo, ni ushuhuda unaojionesha hadi wakati huu kutokana na maadhimisho ya Siku za vijana kitaifa na kimataifa. Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata dakika zake za mwisho katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Yohane Paulo II
27 April 2022, 14:00