Mtakatifu George Mshindi Shuhuda Wa Ukweli Uliotundikwa Msalabani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, tazama inavyopendeza Mama Kanisa kupita katika barabara za ulimwengu, akiwa na ari na shauku ya kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili kwa kila mtu. Huu ndio utume ambao waamini wanaitwa na kutumwa kuutekeleza, yaani kuviringisha jiwe kutoka kwenye kaburi ambalo mara nyingi limemzingira Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Mama Kanisa tarehe 23 Aprili ya kila mwaka, anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu George sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu somo wa Papa Jorge Mario Bergoglio, yaani Baba Mtakatifu Francisko. Mtakatifu George Mshindi, Shahidi na Shujaa jasiri wa Kristo Yesu alipinga waziwazi mpango wa Mfalme Diocletian aliyewatesa, kuwadhulumu na kuwanyanyasa Wakristo kunako mwaka 303. Akatangaza na kushuhudia mwenyewe kuwa ni Mkristo na akatoa wito kwa kila mtu kutambua imani ya kweli katika Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Alisema "Mimi ni mtumishi wa Kristo, Mungu wangu, na kwa kumtumaini yeye, nilionekana kati yenu hiari yako mwenyewe kuishuhudia Kweli." "Ukweli ni nini?" mmoja wa wakuu alirudia swali la Pontio Pilato siku ile ya Ijumaa kuu "Kweli ni Kristo mwenyewe, anayeteswa na wewe," Mtakatifu George alijibu kwa ushupavu! Baada ya siku nane za mateso na machungu makali alikatwa kichwa tarehe 23 Aprili 303.
Hata katika madhulumu, nyanyaso na mateso makali Mtakatifu George Mshindi, Shahidi na Shujaa jasiri alisimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia imani yake kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Alitoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii na kuitaka jamii ya waamini kusimamia na kutangaza Ukweli. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Ijumaa kuu kwa Mwaka 2022 imeongozwa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ambaye alipembua kwa kina na mapana mahojiano kati ya Kristo Yesu na Pontio Pilato kuhusu ukweli ambao umetundikwa juu ya Msalaba! Pilato alijaribu kumuuliza Yesu maswali kadhaa ikiwa kama Kristo Yesu alikuwa ni Mfalme na kwamba Ukweli ni kitu gani? Kristo Yesu alitaka kumdhihirishia Pontio Pilato kwamba, maswali aliyokuwa anauliza yalikuwa ni mazito kiasi kwamba, yalihitaji majibu ya kina. Alimjibu kwamba, Ufalme wake si wa ulimwengu huu. Ufalme wake unasimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kristo Yesu alitoa majibu yote haya bila ya kuogopa kifo kilichokuwa mbele ya macho yake, kwa sababu alikuja ulimwenguni ili kuushuhudia Ukweli.
Kristo Yesu alimwona Pontio Pilato kuwa ni kiongozi aliyehitaji mwanga na ukweli, kwa ajili ya hatima ya maisha ya mwanadamu, ili hatimaye kuyaangalia matukio ya dunia kwa mwanga na maelekeo mapya. Mahojiano kati ya Pontio Pilato na Kristo Yesu yalimshtua sana Pilato, kiasi cha kukatisha mahojiano yao na kuamua kuingia tena ndani ya Praitorio, huku akiwa na hofu kuu ambayo iliathiri hata hukumu yake baadaye. Yesu alimwambia bila kupepesa pepesa macho kwamba alizaliwa kwa ajili ya haya na alikuja ulimwenguni ili aishuhudie kweli na kila aliye wa hiyo kweli huisikia sauti yake. Rej. Yn 14:6. Katika midahalo mingi kuhusu masuala ya kidini, si rahisi sana kumtaja Kristo Yesu katika ukweli alioutangaza na kuushuhudia kwa maisha na utume wake. Umefika wakati wa kutangaza na kushuhudia ukweli juu ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa waja wake. Huu ndio ukweli wa Kiinjili ambao hauna mbadala. Huu ni Ukweli kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika shida na mahangaiko ya watu kutokana na ujinga, maradhi na umaskini, Kristo Yesu alikuwa mstari wa mbele katika kusikiliza na kujibu kilio cha mahitaji msingi ya binadamu wa nyakati zake.
Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anakaza kusema hata kama katika ulimwengu mamboleo kuna uvunjifu mkubwa na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kuna dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu, lakini mambo yote haya hayawezi kuondoa uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Imani ya kweli inawezesha ukweli kutamalaki katika maisha ya binadamu. Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anakaza kusema, mahojiano kati ya Kristo Yesu na Pontio Pilato yaliingia katika hatua tete alipoulizwa: “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Walatini wanasema “Gens tua et pontifices tradiderunt te mihi” Yn 18:35. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutangaza na kushuhudia ukweli kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kw asura na mfano wa Mung una kukombolewa na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni wakati muafaka wa kuambata ukweli kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuambata na kuchuchumilia mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa maneno machache, hivi ni vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko katika ulimwengu mambo leo. Radio Vatican inamtakia pia kheri na baraka katika maisha na utume wake kwa maneno yafuatayo: "Dominus conservet et vivificet eum."