Mkutano Wa Baraza La Kikatoliki La Utume Kwa Wahispania Wanaoishi Marekani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kikatoliki la Utume Kwa Wahispania, NCCHM, ni chombo kinachounganisha Taasisi kuu zinazotoa huduma kwa waamini wa Kanisa Katoliki kutoka nchini Hispania, wanaoishi Marekani. Mkutano wa VI Kitaifa umefunguliwa tarehe 26 Aprili 2022 na unatarajiwa kufungwa tarehe 30 Aprili 2022. “Nacional Católico de Pastoral Hispana “Raíces y Alas 2022” (Congresso Nazionale della Leadership Cattolica del Ministero Ispano 2022 "Radici e Ali") - Washington D.C., 26-30 April 2022.” Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Sauti za Kinabii ni Madaraja kwa Enzi Mpya.” Mkutano huu unatoa kipaumbele cha kwanza kwa: tunu msingi za maisha ya kifamilia; utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya; haki, amani, malezi sanjari na majiundo ya shughuli za kichungaji. Mkutano unapania kutoa mang’amuzi ya pamoja kuhusu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kadiri ya vipaumbele ambavvyo tayari vimekwisha kubainishwa. Maamuzi yatakayofikiwa kwenye Mkutano huu, yatapelekwa kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB kwa maamuzi na utekelezaji wake. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video ndio uliofungua mkutano huu. Amegusia janga la UVIKO-19, madhara ya vita na umuhimu wa Wakristo kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa madaraja ya amani na udugu wa kibinadamu.
Baba Mtakatifu anasema, mada inayonogesha maadhimisho ya mkutano huu ni muafaka kwa mazingira ya nyakati hizi, hasa baada ya maambukizi makubwa ya Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19. Janga hili limekuwa ni sababu ya maafa, mateso na huzuni kubwa na kwa wakati huu, athari hizi zinaendelea kukuzwa na vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine. Ikumbukwe kwamba, vita ni matokeo ya dhuluma inayoweza kupata chimbuko lake ndani ya familia na jumuiya. Hivi ni vita inayopiganwa kimya kimya kutokana na dhuluma katika mazingira kama haya. Mawazo na mipango ya amani, inaonekana kana kwamba, si vipaumbele katika mawazo ya mwanadamu kwa nyakati hizi na matokeo yake, mawazo ya vita yamepewa msukumo mpya. Hii ni changamoto ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kuwasaidia watu kubadilisha fikra zao ndani ya familia, jumuiya, watu wa Mataifa na hatimaye, dunia nzima iweze kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani, udugu na mshikamano. Baba Mtakatifu anawahamasisha Wakristo kushiriki kikamilifu katika mchakato wa mabadiliko ili kuunda madaraja katika sekta mbali mbali za kijamii, ili kudumisha umoja, udugu na mshikamano katika ngazi mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Jumuiya ya KImataifa inahitaji amani ya kweli, ili kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa amani duniani.