Tafuta

Baraza la Makardinali Washauri, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Aprili 2022 limekuwa na mkutano wake wa 41 uliongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Makardinali Washauri, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Aprili 2022 limekuwa na mkutano wake wa 41 uliongozwa na Baba Mtakatifu Francisko.  

Baraza la Makardinali Washauri Yaliyojiri Mkutano 41: Ushuhuda wa Injili Kwa Mataifa

Huu ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kuchapishwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Hii imekuwa ni fursa ya kuchambua kwa kina madhara ya vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine: kisiasa, kiuchumi, kikanisa na kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali Washauri, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Aprili 2022 limekuwa na mkutano wake wa 41 uliongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kuchapishwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Hii imekuwa ni fursa ya kuchambua kwa kina madhara ya vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine: kisiasa, kiuchumi, kikanisa na kiekumene. Baba Mtakatifu amewaelezea Makardinali washauri jitihada mbalimbali zilizofanywa na Sekretarieti kuu ya Vatican ili kujibu changamoto hizi, ili hatimaye, kurejesha amani na utulivu. Wajumbe, wamemtia shime Baba Mtakatifu Francisko kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umekuwa ni mwanya kwa Makardinali washauri kutoa muhtasari wa hali ya amani, afya, mapambano dhidi ya umaskini, hali ya kisiasa, changamoto, fursa na matatizo ya shughuli za kichungaji katika maeneo wanamotoka. Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe12 Novemba 2021 ilifanya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland.

Makardinali Washauri wamezungumzia mkutano wa COP26
Makardinali Washauri wamezungumzia mkutano wa COP26

Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Baba Mtakatifu aliwaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusikiliza na kujibu kwa makini kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini, ili kuweza kutoa majibu muafaka yatakayokuwa ni chimbuko la matumaini kwa vizazi vijavyo! Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kwa sababu hawa ndio waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali Washauri wamepembua changamoto za Mkutano huo mintarafu nchi maskini kutoka, Barani Asia, Afrika, Amerika ya Kusini na Oceania. Imekuwa ni fursa ya kujadili kuhusu dhamana na wajibu wa mwanamke katika Kanisa, mada iliyowasilishwa na Sr. Laura Vicuna kutoka Brazil. Makardinali washauri wamegusia pia huduma ya kidiplomasia inayotolewa na Mabalozi wa Vatican sehemu mbalimbali za dunia.

Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, amepitisha Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba itaanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Itakumbukwa kwamba, Katiba ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uliofanyika mwaka 2013.

Katiba Mpya ni matunda ya maelekezo ya Baraza la Makardinali 2013
Katiba Mpya ni matunda ya maelekezo ya Baraza la Makardinali 2013

Haya ni matunda ya kazi kubwa iliyotekelezwa na Baraza la Makardinali Washauri kuanzia mwezi Oktoba 2013 hadi Februari 2022 na hatimaye, kuchapishwa tarehe 19 Machi 2022 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko bila kusahau mchango uliotolewa na Makanisa mahalia kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katiba hii kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka tisa ya uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kuna baadhi ya Mabaraza ya Kipapa yameunganishwa ili kuongeza tija, ubora na ufanisi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu, sanjari na kuunda Mabaraza mapya ya Kipapa. Sekretarieti kuu ya Vatican inayojulikana kama “Curia Romana” inaundwa na Sekretarieti ya mji wa Vatican, Mabaraza ya Kipapa na Ofisi mbalimbali zenye haki sawa katika utendaji wake. Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, lililokuwa linajulikana kama “Apostolic Elemosineria” yaani “Idara ya Sadaka ya Kitume” limeanzishwa ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali washauri wamejielekeza zaidi katika mchakato wa utekelezaji wake, hatua zilizokwisha kuchukuliwa pamoja na changamoto zake katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Makardinali Washauri linatarajia kufanya tena mkutano wake wa 42 mwezi Juni 2022. Katiba ya Kitume “Hubirini Injili” inayagawanya Mabaraza ya Kipapa katika makundi makuu matatu: Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Uinjilishaji. Pili, Mabaraza ya Kipapa kwa Ajili ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Tatu ni Mabaraza ya Kipapa kwa Ajili ya Huduma ya Upendo.

Mabadiliko mengine makubwa ni kuhusu Tume ya Kipapa kwa Ajili ya Ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia ambayo kwa sasa itakuwa chini ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zake pamoja na kuwa na Rais na Katibu wake. Sehemu kubwa ya Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inajikita katika sheria, kanuni na taratibu na kwamba, kila Mkristo kwa Ubatizo wake ni Mtume mmisionari anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema. Ni katika muktadha huu, hata waamini walei wenye sifa zinazohitajika wanaweza kuteuliwa kuchukua nafasi za uongozi kwenye Sekretarieti kuu kadiri ya Mamlaka aliyokabidhiwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katiba ya Kitume inabainisha vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa ili Mkristo aweze kuteuliwa kutoa huduma katika “Curia Romana.” Hii ni huduma kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro inayomwajibisha mwamini kujenga na kudumisha ushirika sanjari na kutoa huduma kwa utume wa Maaskofu, Makanisa Mahalia, Mabaraza ya Maaskofu na Miundombinu ya Makanisa ya Mashariki.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inaendelea kufanyiwa kazi.
Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inaendelea kufanyiwa kazi.

Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa inapewa kipaumbele cha pekee. Sekretarieti kuu ya Vatican sanjari na dhana ya Mtume mmisionari ni hata kwa wale ambao wameteuliwa kufanya kazi kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Haya ni mambo makuu mawili yanayopaswa kuendelea kumwilishwa mintarafu Katiba ya Kitume ya “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili.” Hawa ni waamini wanaopaswa kuwa na tasaufi imara, maadili, ujuzi na weledi; mwenye uwezo wa kushirikiana na kwamba, uteuzi wa wafanyakazi wa Sekretarieti kuu, ni utambulisho wa Ukatoliki wa Kanisa na kwamba hauna budi kujidhihirisha bila shaka. Wakleri na watawa wataweza kutoa huduma yao kwa muda wa miaka mitano na mkataba huu, unaweza kurudiwa tena katika kipindi cha miaka mitano, baada ya hapo, mhusika atapaswa kurejea Jimboni au Shirikani mwake. Katiba hii mpya inaweka mkazo kwamba, hii ni “Sekretarieti ya Kipapa”. Kumbe, kuna uwezekano mkubwa kwa wafanyakazi wa Sekretarieri kuu ya Vatican kuhamishiwa kutoka Idara moja kwenda Idara nyingine, kadiri ya mahitaji na ufafanuzi kutoka kwenye Sekretarieti ya Uchumi, SPE au maelekezo yatakayotolewa na Msimamizi wa Urithi na Mali ya Kitume, APSA.

Baraza Makardinali
30 April 2022, 14:53