Maadhimisho Ya Juma Kuu Ni Kiini Cha Liturujia ya Mama Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Dominika ya Matawi, tarehe 10 Aprili 2022 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa katika majonzi makubwa, linasubiria ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka! Maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Bado kuna maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kumbe, Maaskofu mahalia wanapaswa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu muhimu katika maadhimisho haya. Ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu ulimwenguni.
Tarehe 10 Aprili 2022 DOMINIKA YA MATAWI itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 Asubuhi kwa saa za Ulaya sawa na saa 5: 00 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki. Baba Mtakatifu Francisko atabariki matawi na baadaye kuongoza maandamano kuelekea katika maadhimisho ya Misa ya Mateso ya Bwana. Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kana kwamba, alikua anawania madaraka ya kisiasa, yaani, kuwa ni mfalme wa Wayahudi!
Ni kutokana na wasi wasi huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pilato alimuuliza Yesu mara mbili, ikiwa kama kweli Yeye ni mfalme. Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Juma Kuu Mji wa Yerusalemu kimsingi ni kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, tarehe 30 Machi 2019 pamoja na Mfalme Mohammed VI wa Morocco walitia saini kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu Kuwa ni Mahali Pa Kuwakutanisha watu! Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Huu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu. Ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano. Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na udugu wa kibinadamu ulimwenguni.
Tarehe 14 Aprili 2022 ALHAMISI KUU: Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu. Ibada hii itaadhimshwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 4:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Baba Mtakatifu atabariki Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbu kumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!
Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hadi Kristo Yesu atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha na Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakitenda kwa nafsi ya Kristo, wakitangaza fumbo lake pamoja na kuyaunganisha maombi ya waamini pamoja na sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa katika Ibada ya Misa Takatifu.
Tarehe 15 Aprili 2022 IJUMAA KUU: Kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuanzia saa 11:00 jioni majira ya Ulaya sawa na Saa 12: 00 za Jioni kwa Saa za Afrika Mashariki kuongoza Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, Sawa na Saa 4:15 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Njia ya Msalaba, mwishoni atatoa neno na kuwapatia waamini baraka yake ya kitume. Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo yatajikita katika Wosia wake wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia.” Huu ni mwaka utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu”. Furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1. Hizi ni tafakari zinazoandaliwa na vyama vya utume wa familia.
Tarehe 16 Aprili 2022 JUMAMOSI KUU majira ya saa 2:30 Usiku kwa Saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza “Kesha la Pasaka” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Atabariki moto wa Pasaka na kuongoza maandamano kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na baadaye itaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu. DOMINIKA YA PASAKA YA BWANA tarehe 17 Aprili 2022 saa 4:00 asubuhi majira ya saa za Ulaya, Sawa na Saa 5: 00 za Asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye atatoa baraka zake za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini kama: “Urbi et Orbi.”