Tafuta

Katekesi Kuhusu Maana Na Thamani ya Uzee: Mahusiano ya Kifamilia

Ruthu ni ishara ya mahusiano ya kifamilia yanayofumbatwa katika upendo; Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika ushuhuda wa tunu msingi za kifamilia, muungano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee; dhamana ya Naomi mkwewe Ruthu pamoja na wosia wa watu wa ndoa kuwaheshimu na kuwathamini wakwe zao katika uzee wao! Upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tangu Jumatano tarehe 23 Februari 2022 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee. Amekazia muungano thabiti kati ya umri na maisha, ili kutegemeana na kukamilishana katika hija ya maisha, bila ya wazee kuonekana kama mzigo kwa jamii na hivyo kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Wazee wanapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Anasema inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Wazee wana ndoto, na vijana wana maono. Rej. Yoe 3:1. Utu, heshima na haki msingi za wazee zinapaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kutambua kwamba, uzee ni amana, utajiri na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wazee wana hekima wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya, ili hata wao waweze kukua na kukomaa kwani wao wanayo mizizi ya historia ya watu wao na kwamba, wao ni kielelezo cha neema na baraka kwa jamii husika. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, amekwisha kuchambua kuhusu: Uzee kama rasilimali kwa vijana wasiokuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha.

Wanandoa wawaheshimu wakwe zao; wakwe pia wajiheshimu, ili kudumisha amani.
Wanandoa wawaheshimu wakwe zao; wakwe pia wajiheshimu, ili kudumisha amani.

Hii ni changamoto kwa wazee kuwa ni mfano bora wa unabii kwa vijana wa kizazi kipya katika maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wazee wanapaswa kuwa ni divai njema inayoleta faraja na furaha kwa vijana wa kizazi kipya; wawe ni wajumbe wa Habari Njema na wala si kinyume chake. Wazee waheshimiwe na kuthaminiwa na jamii na kamwe wasibezwe na kutwezwa. Kwa hakika, ulimwengu unawahitaji vijana shupavu na wenye nguvu pamoja na wazee wenye hekima na busara katika maisha. Baba Mtakatifu amekwisha kudadavua pia kuhusu wakati wa wazee kuagana na jamii, urithi na utajiri wao; kumbukumbu na ushuhuda wa maisha, imani na utu wema. Uhai wa macho ya Mtumishi wa Mungu, Musa ilikuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliyomwezesha kurithisha uzoefu na mang’amuzi ya muda mrefu wa maisha na imani mambo msingi sana kwa wazee. Kimsingi wazee wanayo macho ya imani thabiti na kwamba, wanaweza kwa uaminifu mkubwa kurithisha historia kwa vijana wa kizazi kipya. Mara ya mwisho Katekesi kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Baba Mtakatifu alijikita zaidi katika dhana ya uaminifu machoni pa Mwenyezi Mungu kwa kizazi kijacho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Ruthu kwa hakika ni uso wa huruma ya Mungu inayojidhihirisha katika huruma na ushiriki. Kitabu cha Ruthu kinachosimikwa katika Sura IV kimesheheni amana na utajiri mkubwa wa imani kwa upendo wa Mungu unaowaambata watu wote. Ni kitabu kinachoonesha ufunuo wa huruma ya Mungu anayetambua undani wa maisha ya mwanadamu katika uaminifu wake, ukweli wa maisha unaomzunguka, ukarimu na matumaini yanayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake anapokabiliana na majaribu magumu ya maisha. Ukarimu ni kielelezo cha haki na ujasiri unaopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Mapadre. Katika Kitabu cha Ruthu, Mwenyezi Mungu hazungumzi kamwe, lakini anamgusa Naomi kwa matendo makuu, kielelezo cha uwepo wake wa daima. Huu ni mwaliko wa kutambua na kukiri uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Hii ni hija yenye ugumu na changamoto nyingi, lakini ni katika safari hii ya maisha, Mwenyezi Mungu anafunua huruma na upendo wake wa daima.

Uzee ni rasilimali kwa vijana
Uzee ni rasilimali kwa vijana

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe 27 Aprili 2022 amezungumzia kuhusu Kitabu cha Ruthu ambacho kimesheheni amana na utajiri mkubwa wa huruma na upendo wa Mungu. Ruthu ni ishara ya mahusiano ya kifamilia yanayofumbatwa katika upendo; Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika ushuhuda wa tunu msingi za kifamilia, muungano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee; dhamana ya Naomi mkwewe Ruthu pamoja na wosia wa watu wa ndoa kuwaheshimu na kuwathamini wakwe zao katika uzee wao kwani wao kwa hakika ni chemchemi ya uhai, wanaoshiriki katika familia zao na kwamba, vijana waendelee kujifunza kutoka kwa wazee. Baba Mtakatifu anakazia mahusiano ya kifamilia yanayosimikwa katika upendo unaounda na kuwafungamanisha watu wa vizazi mbalimbali, kiasi cha kujenga udugu unaoongozwa na uaminifu unaojielekeza katika matumaini kwa sasa na kwa siku za usoni.

Inasikitisha kuona kwamba, mahusiano kati ya watu wa ndoa na wakwe zao katika ulimwengu mamboleo yanasuasua kiasi cha kusababisha mafarakano na mipasuko ya kifamilia. Neno la Mungu ambalo ni chemchemi ya imani linatoa mwelekeo wa ushuhuda unaovunjilia mbali maamuzi mbele katika jumuiya ya mwanadamu. Kitabu cha Ruthu ni amana na utajiri mkubwa katika tafakari za upendo na katekesi kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hiki ni Kitabu kinachoonesha ushirikiano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee; chemchemi ya matumaini kwa vijana walioathirika na kubaki na madonda makubwa katika mahusiano yao ya maisha ya ndoa na familia. Ruthu alionja huruma na upendo wa Mama mkwe wake kama neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akamtia nguvu kutafuta mume mwingine, ili maisha yasonge mbele. Akakutana na Boazi aliyesimama kidete kumlinda na kumtunza dhidi ya mfumo dume na hivyo kuanzisha mchakato wa upatanisho kati ya upendo wa kweli, utu na heshima ya binadamu.

Papa Francisko anawataka wazee na vijana kujenga utamaduni wa majadiliano
Papa Francisko anawataka wazee na vijana kujenga utamaduni wa majadiliano

Baba Mtakatifu Francisko anawaasa watu wa ndoa na familia kuwaheshimu, kuwathamini na kuwatunza wakwe zao, kwani wao ni chemchemi ya Injili ya uhai. Wajitahidi kuhakikisha kwamba, wakwe zao, wanaendelea kuishi kwa furaha na matumaini; kwa kuwapokea jinsi walivyo. Baba Mtakatifu anawashauri wazee wenzake wawe makini na ndimi zao, zisije zikawaponza na hivyo kutenda dhambi. Katika Kitabu hiki, Ruthu anampokea na kumkubali Mama mkwe wakwe, kiasi cha kumkirimia tena maisha mapya. Naomi katika uzee wake, akamwandalia maisha mapya Ruthu kwa kumpatia baraka ya kuolewa na Boazi, wakafunga ndoa na kumzalia mwana. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuendeleza majadiliano na kujifunza kutoka kwa wazee, ili familia nyingi zaidi ziweze kuwa ni viota vya Injili ya furaha. Daraja hili la ujenzi wa mahusiano na mafungamano kati ya vijana na wazee halina budi kulindwa na kudumishwa.

Katekesi wazee
27 April 2022, 14:25

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >