Kardinali Javier Lozano Barragán Shuhuda wa Ufufuko 1933- 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.
Kardinali Javier Lozano Barragán alizaliwa tarehe 26 Januari 1933 huko Mexico City na kufariki dunia tarehe 20 Aprili 2022, baada ya kukutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa kuu, tarehe 15 Aprili 2022, aliyeshiriki pia katika Ibada ya Buriani “Ultima commendatio et valedictio” Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ya Misa Takatifu, Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 imeongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko kuongoza Ibada ya Buriani. Hayati Kardinali Javier Lozano Barragán alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 30 Oktoba 1955. Tarehe 5 Juni 1979 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Mexico City na kuwekwa wakfu tarehe 15 Agosti 1979. Tarehe 28 Oktoba, 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Zacatecas. Tarehe 20 Agosti 1996 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Kichungaji Kwa Wafanyakazi Katika Sekta ya Afya na hivyo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu.
Tarehe 21 Oktoba 2003 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Tarehe 18 Aprili 2009 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaridhia ombi lake la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Hatimaye, tarehe 20 Aprili 2022 akiwa na umri wa miaka 89 akafariki dunia. Kimsingi amewatumikia watu wa Mungu kama Padre kwa muda wa miaka 66.4. Akapewa dhamana ya kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kama Askofu kwa muda wa miaka 42.6 na kama Kardinali, kati ya Washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa muda wa miaka 18.4. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali amemtaja Hayati Kardinali Javier Lozano Barragán kuwa ni shuhuda wa ufufuko “Testis resurrectionis”, kauli mbiu ya Kiaskofu aliyeimwilisha katika maisha, utume na vipaumbele vyake katika huduma kama shuhuda wa ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu kwa binadamu. Alionesha upendo wa dhati kabisa kwa Mama Kanisa katika huduma na utume tangu ujana wake kama Jalimu na Mchungaji mkuu.
Ni kiongozi aliyesimika maisha yake katika mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Alikuwa na kipaji cha kuongoza majadiliano na kusikiliza kwa makini. Alionesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa na maskini katika shida na mahangaiko yao, akawa kweli ni kielelezo cha huruma na upendo katika shughuli za kichungaji na kitume. Alikuwa na ibada kubwa kwa Bikira Maria. Hayati Kardinali Javier Lozano Barragán alikuwa ni kiongozi mwenye imani thabiti, mwaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake “Sensus Ecclesiae” pamoja na upendo kwa roho za watu wa Mungu. Mama Kanisa anapenda kumsindikiza Kardinali Javier Lozano Barragán shuhuda wa ufufuko “Testis resurrectionis” kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kwa kufunuliwa wokovu katika Kristo Yesu kwa kusema, “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.” 1Pet 1: 3-4.