Hayati Kardinali Carlos A. Valleyo: Shuhuda Wa Amani Na Upatanisho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Kardinali Carlos Amigo Valleyo, O.F.M, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Sevilla kilichotokea tarehe 27 Aprili 2022, akiwa na umri wa miaka 87. Baba Mtakatifu katika salam za rambirambi alizomwandikia Askofu mkuu Josèp A’ngel Saiz Meneses wa Jimbo kuu la Sevilla, Hispania anamwomba amfikishie salam zake za rambirambi kwa watu wa Mungu Jimboni humo, Ndugu jamaa pamoja na wanashirika wake, bila kuwasahau watu wa Mungu Jimbo kuu Tangeri, nchini Morocco ambako pia huko alihudumu kama Mchungaji mkuu. Hayati Kardinali Carlos Amigo Valleyo, O.F.M, kwa miaka mingi katika maisha na utume wake, alionesha uaminifu mkubwa kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Kanisa.
Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kumwombea, ili roho yake iweze kupumzika kwa amani, ili kwamba, Kristo Yesu kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria wa Montserrat, aweze kumvika taji lisilo chakaa hata kidogo. Kwa njia ya Kristo Yesu Mfufuka, amewapatia wote wanaoomboleza baraka zake za kitume. Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali Carlos Amigo Valleyo, O.F.M, alizaliwa tarehe 23 Agosti 1934, Medina de Rioseco, Jimbo kuu laValladolid nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre na Kitawa, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 17 Agosti 1960. Mtakatifu Paulo VI tarehe 17 Desemba 1973 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tanger nchini Morocco na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 28 Aprili 1974. Tarehe 22 Mei 1982 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sevilla (Seville) na tarehe 29 Juni 1982 akasimikwa rasmi kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Sevilla nchini Hispania.
Tarehe 21 Oktoba 2003 Mtakatifu Yohane Paul II akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali. Tarehe 5 Novemba 2009 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaridhia uamuzi wake wa kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Na ilipogota tarehe 27 Aprili 2022 akiwa na umri wa miaka 87 akaitupa mkono dunia na kuzikwa Jumamosi tarehe 30 Aprili 2022. Kimsingi, Hayati Kardinali Carlos Amigo Valleyo, O.F.M, amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 61; akafundisha, akaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Askofu kwa muda wa miaka 47 na kama Kardinali kwa muda wa miaka 18.5 na sasa anapumzika kwenye usingizi wa amani akiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Katika maisha na utume alitoa kipaumbele cha pekee sana kwa Kanisa Barani Afrika, kiasi cha kujisadaka kwa ajili ya kunogesha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam. Alijielekeza zaidi katika uinjilishaji wa kina uliogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Alisimika maisha yake kwa ajili ya katekesi, akajipambanua kwa kusimama kidete kunogesha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki, amani na maridhiano. Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Ekaristi Takatifu iliyomwilishwa katika Injili ya huduma na upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.
[ Audio Embed Hayati Kardinali Amigo]