Juma Kuu Ni Kiini Cha Liturujia ya Kanisa: Mafumbo Ya Wokovu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 13 Aprili 2022, kama sehemu ya maandalizi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2022 amejikita katika kufafanua maana ya Amani inayotolewa na Kristo Yesu wakati wa Sherehe ya Pasaka. Anasema, hii ni amani ambayo ni kinyume kabisa cha matumizi ya nguvu, wala ushindi wa kulazimisha. Amani ya Kristo Yesu inajikita katika njia ya upole, Msalaba na huduma. Kwa hakika Kristo Yesu amechukua, maovu, dhambi na kifo cha mwanadamu. Amani ya Kristo ni kielelezo cha sadaka na majitoleo yake binafsi. Ni amani ambayo inakita mizizi yake katika upole na ujasiri, lakini ni amani ambayo si rahisi kupokeleka na walimwengu. Baba Mtakatifu anasema, Pasaka kiwe ni kipindi cha neema na upyaisho unaopata chimbuko lake kutoka katika undani wa maisha ya watu. Maadhimisho ya Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Mkesha wa Pasaka ya Bwana, iwe ni hija ya maisha ya kiroho inayosimikwa katika upendo na sadaka ya mtu binafsi, ili kuweza kuambata amani ya kweli inayobubujika kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.
Juma kuu ni kiini cha Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika kipindi cha mwaka mzima wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kufuatilia kwa makini ili kuweza kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya. Ni mwaliko kwa wazee, wagonjwa, wanandoa wapya pamoja na vijana wa kizazi kipya, kuonesha ushuhuda wa imani yao kwa kuungana na Kristo Yesu katika mateso, kifo na hatimaye, ufufuko wake kwa wafu, chemchemi ya matumaini ambayo hayadanganyi kamwe. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Poland ambao wanaadhimisha Pasaka ya Bwana, wakiwa na wageni na jirani zao wakimbizi wa vita kutoka Ukraine. Huu ni wakati wa kutafakari Fumbo la Msalaba katika maisha yao, huku wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Waendelee kuombea amani na utulivu nchini Ukraine. Sala na sadaka za waamini ziwaendee na kuwaambata wale wote wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia. Waamini wasisite kumkimbilia Kristo Yesu, katika shida na mahangaiko yao, ili aweze kuwafariji na kuwalinda.