Tafuta

Jubilei ya Miaka 50 ya huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s University, Belfast.” Jubilei ya Miaka 50 ya huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s University, Belfast.”  

Jubilei ya Miaka 50 ya Huduma ya Maisha ya Kiroho & Kiutu Chuo Kikuu Cha Belfast

Jubilei ya Miaka 50 ya huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s. Ni fursa ya kuendelea kuthamini mchango unaotolewa na Kanisa katika majiundo na malezi ya wanafunzi: kiroho na kiakili mintarafu Mapokeo ya Kanisa. Ni nafasi ya k kuendeleza mwamko wa Kiinjili unaosimikwa katika utamaduni wa watu kukutana, ili kushirikisha kweli za Kiinjili kama alivyofanya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s University, Belfast” kilichoko nchini Ireland, “The Catholic Chaplaincy at Queen's University, Belfast” kwa mwaka 2022 kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Kuheshimu mafanikio yaliyopita na kufirikia siku zijazo kwa ujasiri.” Jubilei ya Miaka 50 ya huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s University, Belfast.” Hii ni fursa ya kuendelea kuthamini mchango unaotolewa na Mama Kanisa katika majiundo na malezi ya wanafunzi: kiroho na kiakili mintarafu Mapokeo ya Kanisa. Ni nafasi ya kuendelea kujenga na kudumisha ari na mwamko wa Kiinjili unaosimikwa katika utamaduni wa watu kukutana, ili kushirikisha kweli za Kiinjili kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake.

Wasomi wajenge utamaduni wa kukutana na kushirikishana tunu injili za kiimani
Wasomi wajenge utamaduni wa kukutana na kushirikishana tunu injili za kiimani

Kama binadamu, lakini zaidi kama waamini wanahamasishwa kutafuta na kuambata ukweli, huku wakiendelea kuwa ni mashuhuda wa ukweli kwa njia ya maisha yao. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 25 Aprili 2022 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Huduma ya maisha ya kiroho Chuo Kikuu cha “Queen’s University, Belfast” kilichoko nchini Ireland, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya huduma hii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana kwa ajili ya Ufalme wa Mungu ni jambo tete kabisa. Huu ni mchakato unaokita mizizi yake katika kutazama na kusikiliza kwa makini; kusimama na kushirikishana mema ya nchi kwa nyoyo safi, bila kosa.

Ni wito na mwaliko wa kukubali mahusiano mapya yanayoletwa na Kristo Yesu kwa: Kushirikishana na kushikamana na wengine katika hija ya kutafuta na kuambata ukweli; kujenga na kudumisha mitandao ya mahusiano na mafungamano ya kijamii katika umoja. Haya ni mang’amuzi ya ukweli wa udugu wa kibinadamu, msafara wa mshikamano na hija takatifu. Rej. Evangelii Gaudium, 87. Baba Mtakatifu anawahimiza mahuaji hawa wote, kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake ajitahidi kuwa ni mhamasishaji mkuu wa utamaduni wa watu kukutana katika mazingira ya Chuo Kikuu, ili kuendelea kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ireland inayosimikwa katika utamaduni wa ukarimu, upatanisho, uaminifu wa Injili pamoja na kuambata utakatifu wa maisha. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewakabidhi ili waendelee kuitafakari na hatimaye, akawazamisha chini ya ulinzi na tunza ya Mama Bikira Maria, ili waendelee kuwa ni Jumuiya ya Imani na Urafiki katika mazingira ya Chuo Kikuu.

Jubilei huduma

 

 

25 April 2022, 15:35