Ijumaa Kuu: Ukweli Umetundikwa Juu Ya Msalaba: Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa kuu tarehe 15 Aprili 2022 ameongoza Ibada ya Ijumaa kuu. Mwanzoni kabisa mwa Ibada, Baba Mtakatifu alijilaza kifudifudi, kielelezo cha anguko la kwanza la mwanadamu kupitia kwa Adam na Eva. Dhambi ya asili ni sababu ya mwanadamu kuendelea kuanguka dhambini kila wakati. Kulala kifudifudi ni ishara ya fedheha ya mwanadamu aliyoipata baada ya kuanguka dhambini. Hii ni ishara ya huzuni na mateso ya Kanisa kuu ya madhara ya dhambi ambazo zinaendelea kumsulubisha Kristo Yesu hadi sasa. Ni alama ya kifo cha Kristo Yesu. Ibada ya Ijumaa kuu imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Yaani Liturujia ya Neno inayohitimishwa kwa maombi kwa ajili ya watu wote. Pili ni Ibada ya Kuabudu Msalaba, ambao juu yake ukweli wote umetundikwa juu yake, yaani, Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu. Tatu ni Komunyo takatifu. Katika chemchemi ya ufunuo wa hekima, upendo na huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu aliingia katika mateso na kifo kwa kudhamiria lile Fumbo kuu la Upendo ambalo angelikamilisha pale juu Msalabani. Akiwa pale Msalabani, Askari mmoja wapo akamchoma ubavuni kwa mkuki, mara ikatoka Damu na Maji, alama za Sakramenti za Kanisa.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Ijumaa kuu imeongozwa na Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ambaye amepembua kwa kina na mapana mahojiano kati ya Kristo Yesu na Pontio Pilato kuhusu ukweli ambao umetundikwa juu ya Msalaba! Pilato alijaribu kumuuliza Yesu maswali kadhaa ikiwa kama Kristo Yesu alikuwa ni Mfalme na kwamba Ukweli ni kitu gani? Kristo Yesu alitaka kumdhihirishia Pontio Pilato kwamba, maswali aliyokuwa anauliza yalikuwa ni mazito kiasi kwamba, yalihitaji majibu ya kina. Alimjibu kwamba, Ufalme wake si wa ulimwengu huu. Ufalme wake unasimikwa katika kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kristo Yesu alitoa majibu yote haya bila ya kuogopa kifo kilichokuwa mbele ya macho yake, kwa sababu alikuja ulimwenguni ili kuutolea ukweli ushuhuda. Kristo Yesu alimwona Pontio Pilato kuwa ni kiongozi aliyehitaji mwanga na ukweli, kwa ajili ya hatima ya maisha ya mwanadamu na kuyaangalia matukio ya dunia kwa mwanga mpya wa mawazo.
Mahojiano kati ya Pontio Pilato na Kristo Yesu yalimshtua sana Pilato, kiasi cha kukatisha mahojiano yao na kuamua kuingia tena ndani ya Praitorio, huku akiwa na hofu kuu ambayo iliathiri hata hukumu yake baadaye. Yesu alimwambia bila kupepesa pepesa macho kwamba alizaliwa kwa ajili ya haya na alikuja ulimwenguni ili aishuhudie kweli na kila aliye wa hiyo kweli huisikia sauti yake. Rej. Yn 14:6. Katika midahalo mingi kuhusu masuala ya kidini, si rahisi sana kumtaja Kristo Yesu katika ukweli alioutangaza na kuushuhudia kwa maisha na utume wake. Umefika wakati wa kutangaza na kushuhudia ukweli juu ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu Baba kwa waja wake. Huu ndio ukweli wa Kiinjili ambao hauna mbadala. Huu ni kweli kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika shida na mahangaiko ya watu kutokana na ujinga, maradhi na umaskini, Kristo Yesu alikuwa mstari wa mbele katika kujibu kilio cha mahitaji msingi ya binadamu. Hata kama katika ulimwengu mamboleo kuna uvunjifu mkubwa na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kuna dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu, lakini mambo yote haya hayawezi kuondoa uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Imani ya kweli inawezesha ukweli kutamalaki katika maisha ya binadamu.
Kardinali Raniero Cantalamessa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa anakaza kusema, mahojiano kati ya Kristo Yesu na Pontio Pilato yaliingia katika hatua tete alipoulizwa: “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Walatini wanasema “Gens tua et pontifices tradiderunt te mihi” Yn 18:35. Kwa maneno machache Pontio Pilato anamuuliza Kristo Yesu katika muktadha wa ulimwengu mamboleo akisema, waamini wa Kanisa lako, Mapadre wako, wamekutosa na kukukimbia, wamekosa imani na wewe, Je, bado unataka sisi tukuamini? Imani na upendo kwa Mama Kanisa vinaweza kupungua na hata kufishwa, lakini mwamini mwenye Imani thabiti hawezi kuteteleka. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Kanisa na hata waamini walei wameguswa na kupapaswa na kashfa mbalimbali. Lakini, ikumbukwe kwamba, hii ni sehemu ya maisha tangu awali kabisa, hata kabla ya Pasaka ya kwanza ya Bwana. Yuda Iskariote, aliyetunza hazina, alimsaliti Kristo Yesu kwa busu. Mtakatifu Petro, Mwamba wa Kanisa alimkana Kristo Yesu mara tatu kabla ya kuwika jogoo! Petro, akagugumia na kuangua kilio! Ushupavu wake umetoweka kama umande wa asubuhi, kwa kukaziwa macho na Mjakazi! Ni rahisi sana kuwanyooshea kidole Mitume wa Yesu kwa mapungufu na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini Kardinali Raniero Cantalamessa anasema, hata waamini katika nyakati hizi, hawana budi kububujika machozi kutokana na dhambi na makosa wanayoendelea kutenda: kwa mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu. Leo hii, Mama Kanisa anasrehekea Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kwa kukikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuambata na kuchuchumilia ukweli, uadilifu na utakatifu wa maisha. Ninawaambia anasema Kristo Yesu, msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Rej. Lk 13: 5.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pasaka ni Sherehe ya kweli ya Mungu na mwanadamu, kwa sababu, hii ni Pasaka ambayo Kristo Yesu ameitolea sadaka kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu. Ndiyo maana ile Siku ya kwanza ya Juma alipowatokea wafuasi wake aliwaambia “Amani iwe kwenu” Yn 20: 20.21. Pasaka katika asili yake maana yake kwa Lugha la Kilatini: Pasqua, Pascha, "Kupita juu” Kwa lugha ya Kigiriki πάσχα (pascha), na kwa Kiharamayo פסח (pesach). Huu ni mwaliko wa pekee kwa Pasaka ya Mwaka 2022 kupita juu ya miungu wa dunia hii na kumwendea Mungu wa kweli; ni mwaliko wa kutoka katika chuki na uhasama ni kuanza kujikita katika upendo unaowaweka huru; badala ya kutegemea amani inayofumbatwa kwenye mtutu wa bunduki, watu wa Mungu waanze kujielekeza katika ushuhuda wa amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika waaamini kusimama mbele ya Msalaba, chemchemi ya amani na wamwombe Kristo Yesu aweze kuwakirimia amani katika nyoyo zao, amani kwa ajili ya ulimwengu. Itakumbukwa kwamba, Tafakari za Njia ya Msalaba Kuzunguka Magofu ya Colosseo inajikita katika Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia.” Huu ni mwaka utakaohitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya X ya Familia Duniani. Kilele cha maadhimisho haya mjini Roma ni tarehe 26 Juni, 2022 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Furaha inayopata chimbuko lake ndani ya familia ni furaha ya Kanisa pia na kwamba, tamko la Kikristo kuhusu familia ni Habari Njema kweli! Rej. AL 1. Hizi ni tafakari zilizoandaliwa na vyama vya utume wa familia.