Serikali ya Nicaragua Yamfukuza Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vatican imesikitishwa sana na uamuzi wa Serikali ya Nicaragua ya kumfukuza Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag, Balozi wa Vatican nchini Nicaragua na kumtaka kuwa ameondoka nchini humo katika kipindi cha saa 24 kama “Persona non grata.” Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag amekuwa akitoa huduma yake ya kidiplomasia nchini Nicaragua tangu mwaka 2018 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko. Vatican inasema, imeshindwa kuuelewa uamuzi huu dhidi ya Balozi wa Vatican nchini Nicaragua, ambaye amekuwa akitekeleza dhamana na utume wake kwa sadaka na majitoleo makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Nicaragua, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Amejitahidi kujenga na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Nicaragua.
Ni vyema, ikakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag, amekuwa akishiriki kama shuhuda na msindikizaji wa Majadiliano kati ya Serikali ya Nicaragua na Wapinzani wa Serikali kisiasa, kama sehemu ya mchakato wa upatanisho na ujenzi wa Umoja wa Kitaifa sanjari na Serikali kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa. Vatican katika tamko lake, inasema, wakati ambapo kumefanyika kosa hili kubwa na lisiloweza kuhalalishwa kwa sababu halitoi taswira sahihi ya watu wa Mungu nchini Nicaragua ambao kimsingi ni Wakristo wa dhati, Vatican itaendelea kuwa na imani na Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag, kama Balozi wa Vatican.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018, aliungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua ili kuonesha masikitiko yake kutokana na machafuko pamoja na ghasia zilizokuwa zinaendelea nchini humo ambazo tayari zilipelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa vibaya. Kikundi cha watu wenye silaha kinachounga mkono serikali iliyoko madarakani kimeamua kuanzisha mashambulizi ya silaha ili kupambana na raia wanaopinga mchakato wa mageuzi unaofanywa na serikali ya Nicaragua. Baba Mtakatifu aliwakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na mashambulizi haya. Alisema, Kanisa daima litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, yanayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika matendo kwa kuheshimu uhuru wa watu, lakini zaidi kwa kuheshimu maisha ya watu! Baba Mtakatifu aliiombea nchi ya Nicaragua, ili iweze kusitisha ghasia na hatimaye, kuwa na uhakika wa kuanza tena majadiliano katika ukweli na uwazi!
Tangu tarehe 18 Aprili 2018 kumekuwepo na maandamano makubwa ya kupinga mchakato wa mageuzi ya masuala ya pensheni kwa kupunguza kiasi cha asilimia 5%, mchakato ambao ulikuwa umeridhiwa na Rais Daniel Ortega wa Nicaragua. Baada ya mshike mshike na patashika nguo kuchanika, Rais Daniel Ortega, akanyoosha mikono juu na kuondoa muswada wa mageuzi! Lakini, wananchi wakaendeleza mapambano kwani walisema, Rais Daniel Ortega, ndiye aliyekuwa “mzigo kwa Serikali” baada ya kuongoza Nicaragua kwa muda wa miaka 30. Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu, likaamua kuingilia kati ili kuanzisha mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na raia wake, ombi lililokuwa limetolewa na Rais Daniel Ortega. Lakini Rais Ortega alifutilia mbali mchakato wa majadiliano na kuamua “kutembeza mkong’oto.” Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua katika tamko lake, lilisikitika na kulaani mashambulizi dhidi ya raia na kwamba, hivi ni vitendo vilivyokuwa vinakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Maaskofu walikaza kusema, raia wanao uhuru wa kuandamana kikatiba, lakini Serikali imeamua kuwashughulikia bila huruma, kiasi hata cha kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa dunia.