Tafuta

Kipaumbele cha kwanza ni kwa Sakramenti ya huruma na furaha ili kuonja upendo na faraja unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kipaumbele cha kwanza ni kwa Sakramenti ya huruma na furaha ili kuonja upendo na faraja unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. 

Sakramenti Ya Kitubio Ni Chemchemi ya Toba Na Neema ya Upatanisho

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kuomba neema ya upatanisho inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya furaha. Bikira Maria anawafunda waamini kutoogopa na badala yake kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu pamoja na kupokea mapaji ya Roho Mtakatifu, ili hatimaye, kuuweka wakfu ulimwengu kwa Moyo Safi wa Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 25 Machi 2022 Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kuwa atakuwa Mama wa Mungu ameadhimisha Ibada ya Toba na Maondoleo ya Dhambi sanjari na kuiweka Urussi na Ukraine wakfu kwa maombezi ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Wakati huo huo, Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka Mkuu wa Kipapa, kwa niaba ya Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada kama hiyo kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno. Ibada ya kuiweka wakfu Urussi na Ukraine kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, imeadhimishwa sehemu mbalimbali za dunia kama kielelezo cha ushirika wa Kanisa katika shida na mahangaiko ya watu mbalimbali kutokana na kufumuka kwa vita. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kuomba neema ya upatanisho inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya furaha. Bikira Maria anawafunda waamini kutoogopa na badala yake kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu pamoja na kupokea mapaji ya Roho Mtakatifu, ili hatimaye, kuuweka wakfu ulimwengu kwa Moyo Safi wa Bikira Maria. Sababu kubwa ya Bikira Maria kufurahi ni kwa sababu Mwenyezi Mungu yu pamoja naye, kama ilivyo pia kwa waamini wanaomwendea Mwenyezi Mungu kwa toba na unyenyekevu ili kuomba msamaha na maondoleo ya dhambi zao, tayari kukirimiwa nguvu ya kusimama tena na kufurahia maisha.

Mapadre waungamishaji wawe ni chemchemi ya furaha kwa waamini wao.
Mapadre waungamishaji wawe ni chemchemi ya furaha kwa waamini wao.

Kiini cha maadhimisho yote ya Sakramenti ya furaha na huruma ya Mungu ni dhambi za mwanadamu, lakini kubwa zaidi ni msamaha na maondoleo ya dhambi. Hii ni fursa kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie neema ya kutambua nguvu ya upatanisho inayowaambata na kuwashangaza. Kumbe, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Sakramenti ya huruma na furaha, ili kuonja upendo, huruma na faraja inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa Mapadre waungamishi wanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, ili kuonja upendo wa Mchungaji mwema anayewabeba Kondoo wake mabegani pake. Watambue kwamba, wao ni mifereji ya neema inayomwagilia jangwa na ugumu wa nyoyo za waamini; ni mifereji ya maji hai ya huruma ya Baba wa milele. Usiogope ni ujumbe wa matumaini ambao umesikika katika Maandiko Matakatifu tangu kwa Mzee Abrahamu, Baba wa imani, Isaka na Yakobo hadi kwa Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki na hatimaye kwa Bikira Maria. Mwenyezi Mungu anatambua udhaifu, mapungufu na dhambi za mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini ni kumwendea Mwenyezi Mungu, ili kumshirikisha mapungufu haya yanayowaandama waja wake naye kwa huruma na upendo wake, atayageuza na kuyapatia ufufuko. Jambo la msingi anasema Mwenyezi Mungu; Msiogope!

Bikira Maria alipopashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu, alipata mahangaiko makubwa ndani mwake kutokana na mazingira, tamaduni, mapokeo na Sheria ya Musa. Aliogopa kuhusu mahusiano yake na Mtakatifu Yosefu mtu wa haki, watu wa kijijini kwake bila kuwasahau watu wake. Bikira Maria hakuweka kipingamizi na badala yake akajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha kwanza kwa imani mbele ya Mwenyezi Mungu na mengine yote watayapata kwa ziada. Mwenyezi Mungu ni chemchemi dhidi ya woga na hofu. Waamini wanapaswa kuthubutu kuamka na kumwendea Mungu ili aweze kuwafufua, kuishi ndani mwake na kuendelea kutenda mema. Katika siku za hivi karibuni, watu wengi wameteseka kutokana na utamaduni wa kifo kuingia kwa kasi katika maisha ya wa watu, kutokana na mashambulizi makali ya silaha kiasi kwamba, watu wanajiona kana kwamba, “si mali kitu.” Kwa hakika wanayo matumaini ya kusikia tena wakiambiwa “Usiogope” kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Huu ni uwepo unaotakasa na kuwaondolea watu dhambi zao, huku akiwajalia amani na utulivu wa ndani. Huu ni mwaliko wa kumrudia Mwenyezi Mungu ili kuonja msamaha wake.

Msamaha na maondoleo ya dhambi ni kiini cha Sakramenti ya Upatanisho.
Msamaha na maondoleo ya dhambi ni kiini cha Sakramenti ya Upatanisho.

Bikira Maria alikirimiwa nguvu ya Mungu katika maisha yake kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hata mwanadamu katika ulimwengu mamboleo kwa nguvu zake mwenyewe “hawezi kufua dafu.” Kumbe, anahitaji nguvu za Roho Mtakatifu zinazosimikwa katika haki na unyenyekevu wa Mungu. Watu wana kiu ya upendo wa Roho Mtakatifu unaozima moto na ari ya kutaka kulipiza kisasi, chuki na hasira, wivu na tabia ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Injili ya upendo ndiyo zawadi kubwa inayoweza kutolewa na Mama Kanisa. Upendo ndio utambulisho wa maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kuchota nguvu ya upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika msamaha, kama ambavyo Roho Mtakatifu alipomshukia Bikira Maria. Mageuzi ya kweli anasema Baba Mtakatifu Francisko yanapata chimbuko lake kutoka katika moyo wa mwadamu. Bikira Maria alipewa upendeleo wa pekee kwa kukirimiwa neema iliyomkinga na kila aina ya doa na dhambi, iliyomwezesha Mwenyezi Mungu kuanzisha historia ya mwanadamu kwa njia ya Bikira Maria. Hii ni historia ya wokovu na chemchemi wokovu na amani. Ni kwa njia hii Mwenyezi Mungu akabadilisha historia ya mwanadamu kwa kubisha kwenye Mlango wa Moyo Safi wa Bikira Maria.

Hata leo hii baada ya kupyaishwa kwa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, hata Baba Mtakatifu akiwa ameungana na Maaskofu pamoja na waamini wao kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanapenda sasa kuliweka wakfu Kanisa kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, lakini zaidi wananchi wa Urussi na Ukraine, wanaomheshimu na kumtukuza Bikira Maria kama Mama, kielelezo cha Ibada inayopata chimbuko lake kutoka katika maisha ya kiroho. Hiki ni kitendo cha watoto kumtumainia Bikira Maria katika nyakati hizi za maafa makubwa ya mpambano ya kivita yanayotishia amani. Watoto wanakimbilia kwa Bikira Maria, ili kumshirikisha hofu, woga na machungu pamoja na wao wenyewe kujikabidhi kwa Bikira Maria. Katika Moyo Safi wa Bikira Maria; Moyo usiokuwa na doa, mng’ao wa Baba wa milele, waamini wanataka kuweka humo amana n ana tunu za udugu wa kibinadamu, amani na yale yote waliyo nayo, ili kwa njia ya Bikira Maria, aweze kuwalinda na kuwatunza. Watu wanahitaji kuona miradi ya amani ikishamiri na wala si woga na ubaya wa moyo. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, ashiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani kwa matumaini kwamba, kwa hakika atawajibu kwa wakati muafaka kama ilivyokuwa siku ile aliposikia kwamba, Binamu yake Elizabeth alikuwa mja mzito, akaondoka kwa haraka. Bikira Maria asaidie na kuwaongoza katika udugu wa kibinadamu, majadiliano na njia ya amani.

Sakramenti ya Furaha
26 March 2022, 10:03