Tafuta

2022.03.19 Papa  alitembelea Hospitali ya Bambino Gesù kuwaona watoto wa Ukraine waliolazwa kutokana na majeraha makali. 2022.03.19 Papa alitembelea Hospitali ya Bambino Gesù kuwaona watoto wa Ukraine waliolazwa kutokana na majeraha makali. 

Papa:vita vya uchokozi dhidi ya Ukraine ni vya kinyama na vya kufuru

Baba Mtakatifu Francisko amepyaishwa wito kwa mamlaka kutafuta suluhisho la Vita nchini Ukraine.Amekumbusha ziara yake aliyowatembelea watoto wa Ukraine waliojeruhiwa ambao wamelazwa katika Hospitali ya Bambino Gesù na akasisitiza mwaliko wake wa kujumuika pamoja katika sala ya kuwekwa wakfu kwa nchi ya Ukraine na Urussi kwa Moyo Safi wa Bikira Maria siku ya Ijumaa ijayo 25 Machi 2022.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 20 Machi 2022, Baba Mtakatifu Francisko amerudia kutazama hali halisi ya vita vinavyoendelea nchini ukraine ambapo ametumia maneno mazito sana kama vurugu la shambulio, mauaji ya kinyama, ya kuchukiza na hatimaye kusema vita visivyo vya kibinadamu na vya kufuru. Baba Mtakatifu akianza kuwaleza waamini na mahujaji waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro na walikuwa ni wengi sana amesema:  “Kwa bahati mbaya, uchokozi mkali dhidi ya Ukraine haukomi, mauaji yasiyo na maana ambapo uharibifu na ukatili unarudiwa kila siku. Hakuna uhalali kwa hili! Ninawasihi wahusika wote katika jumuiya ya kimataifa kujitoa kiukweli kukomesha vita hivi vya kuchukiza. Pia Juma hili makombora na mabomu yaliwakumba raia, wazee, watoto na akina mama wajawazito", alibainisha Papa.

Wito wa Papa Francisko wa kusitisha mauaji na vita nchini Ukraine

 

Papa akiendelea aliongeza kusema:"Nilienda kuwatembelea watoto waliojeruhiwa ambao wako hapa Roma. Mmoja wao amekatwa mkono, mwingine amejeruhiwa kichwani ... Watoto wasio na hatia. Ninawaza mamilioni ya wakimbizi wa Ukraine ambao wanapaswa kukimbia na kuacha kila kitu nyuma na ninahisi uchungu mkubwa kwa wale ambao hawana hata uwezekano wa kutoroka. Babu na bibi wengi, wagonjwa na maskini, waliotenganishwa na familia zao, watoto wengi na watu dhaifu wanabakia kufa chini ya mabomu, bila kupata msaada na bila kupata usalama hata katika makao ya kujikinga na  mashambulizi ya anga”.

Baba Mtakatifu Francisko amesema “Hii yote ni unyama! Hakika, pia ni kufuru, kwa sababu inaenda kinyume na utakatifu wa maisha ya mwanadamu, hasa dhidi ya maisha ya mwanadamu yasiyo na ulinzi, ambayo lazima yaheshimiwe na kulindwa, sio kuondolewa, na ambayo yanahesimiwa  kabla ya mkakati wowote ule! Tusisahau: ni ukatili, unyama na wa kufuru! Tuwaombee kwa ukimya wale wanaoteseka…. Katika wakati huo, kimya imetanda ya sala katika uwanja wa Mtakatifu Petro. Mara baada ya sala hiyo ya kimya, Papa Francisko ameongeza kusema “Nimefarijika kujua kwamba watu ambao wamesalia chini ya mabomu hawakosi ukaribu wa Wachungaji, ambao katika siku hizi za huzuni wanaishi Injili ya upendo na udugu. Siku za hivi karibuni nimesikia baadhi yao kwenye simu jinsi walivyo karibu na watu wa Mungu, asanteni ndugu wapendwa kwa ushuhuda huu na msaada madhubuti ambao mnatoa kwa ujasiri kwa watu wengi waliokata tamaa !  Baba Mtakatifu Francisko aidha amesema “ Pia namfikiria Balozi  wa Kitume, ambaye amepewa jukumu hilo hivi karibuni Askofu Mkuu Visvaldas Kulbokas, ambaye amebaki Kiev pamoja na wahudumu wake tangu mwanzo wa vita na uwepo wake unanifanya kuwa karibu kila siku na watu wa Ukraine wanaoteswa”.

Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022

Tuwalinde dhidi ya tai wala mizoga ya kijamii

Tuwe karibu na watu hawa, tuwakumbatie kwa upendo, kwa kujitoa madhubuti na kwa maombi. Na tafadhali tusizoee vita na vurugu! Tusichoke kukaribisha kwa ukarimu, kama tunavyofanya: sio tu sasa, katika hali ya dharura, lakini pia katika juma na miezi ijayo. Kwa sababu ninyi mnatambua kwamba mara ya kwanza, sisi sote hufanya tuwezavyo kuwakaribisha, lakini baadaye mazoea hayo uanza kupooza mioyo yetu kidogo na kusahau. Tuwafikirie wanawake hawa, watoto hawa ambao baada ya muda, bila kazi, wakitenganishwa na waume zao, watatafutwa na 'Tai au wala mizoga wa jamii' Tafadhali tuwalinde”, amesisitiza kwa nguvu Papa Francisko.

Mwaliko wa Papa wa kusali tarehe 25 Machi 2022

Baba Mtakatifu akikumbuka mwito wake wa sala amesema “Ninatoa mwaliko kwa kila jumuiya na kila waamini kujumuika nami siku ya Ijumaa tarehe 25 Machi, katika Maadhimisho Kupashwa Habari Bikira Maria  ili  kutekeleza tendo zito la kuwekwa wakfu kwa ubinadamu, hasa Urussi na Ukraine, kwa Moyo Safi wa Bikira Maria, ili yeye Malkia wa amani aweze kuleta amani kwa ulimwengu".

Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022

Salamu kwa mahujaji na waamini”

Kwa kuhitimisha amewageukia waliokusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro na Kusema: “Nawasalimu ninyi nyote, Warumi na mahujaji kutoka Italia na kutoka nchi mbalimbali. Hasa, ninawasalimu waamini wa Madrid, kikundi cha kimataifa “Agora ya wakazi wa dunia”, madaktari na waokoaji wa Huduma ya Dharura ya 118, Upyaji wa Karismatiki wa Kikatoliki “Charis”,  ambayo ndiyo pekee inayotambuliwa rasmi,  “Charis”, sio wengine na wanachama wa Harakati ya Wafokolari. Ninawasalimu Kwaya Ndogo ya Antoniano kutoka Bologna pamoja na bendi ya Polisi ya Jimbo, Kwaya ya “Ensemble Vox Cordis” ya Fornovo ya Mtakatifu Giovanni, Kwaya ya Mtakatifu Vincenzo Grossi ya Pizzighettone, vijana wa taaluma ya imani kutoka Angera, Sesto Calende na Ternate, katika hija ya Jimbo katoliki la Asti na waamini wa Venezia na Sassari". Mwisho amewatakia Dominika njema, na wasisahau kusali kwa ajili yake.

Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022
Sala ya Malaika wa Bwana 20 Machi 2022
WITO WA PAPA KUSITISHA VITA NA KUOMBEA UKRAINE
20 March 2022, 13:31