Tafuta

Papa Francisko: Sitisheni mauaji ya kinyama nchini Ukraine kabla ya miji hii kugeuka kuwa ni kumbukumbu ya makaburi ya kivita. Papa Francisko: Sitisheni mauaji ya kinyama nchini Ukraine kabla ya miji hii kugeuka kuwa ni kumbukumbu ya makaburi ya kivita. 

Papa Francisko: Sitisheni Mauaji ya Kinyama Nchini Ukraine

Kumekuwepo na mauaji ya watoto, watu wasiokuwa na hatia, wala hawana uwezo wa kujihami dhidi ya mashambulio ya Warussi. Papa anakaza kusema, hakuna sababu msingi inayoweza kukubaliwa ili kuhalalisha mauaji haya. Jambo kubwa la kuzingatia kwa wakati huu ni kusitisha mashambulizi ya kijeshi kabla ya mji wa Mariupol kugeuka na kuwa ni Mji wa Makaburi ya Vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 13 Machi 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametoa mwaliko wa kusitisha vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine. Katika siku za hivi karibuni mji wa Mariupol umegeuka kuwa ni mji wa mashuhuda wa vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine. Kumekuwepo na mauaji makubwa ya watoto, watu wasiokuwa na hatia na wala hawana uwezo wa kujihami dhidi ya mashambulio ya Warussi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hakuna sababu msingi inayoweza kukubaliwa ili kuhalalisha mauaji haya. Jambo kubwa la kuzingatia kwa wakati huu ni kusitisha mashambulizi ya kijeshi kabla ya mji wa Mariupol kugeuka na kuwa ni Mji wa Makaburi ya Vita.

Mwaliko wa kusitisha vita nchini Ukraine
Mwaliko wa kusitisha vita nchini Ukraine

Baba Mtakatifu Francisko akiwa na majonzi mazito moyoni mwake anapenda kuungana na watu wa kawaida kusali na kuombea ili vita iweze kukoma. Kwa jina la Mungu Baba mwingi wa huruma na mapendo, wasikilize kilio cha wale wanaoteseka, ili mabomu pamoja na mashambulizi yakome tayari kuanza kujielekeza katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kutengeneza njia ya msaada wa kiutu ambayo ni salama na inatekelezeka. Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu amewaomba Urussi na Ukraine kusitisha mapigano mara moja. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuonesha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwapokea na kuwapatia hifadhi. Amewasifu wale wote wanaoendelea kujenga na kuimarisha mtandao wa upendo na mshikamano na wakimbizi kutoka Ukraine.

Kwa mara nyingine tena Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika ujumla wao, kuungana pamoja naye kwa ajili ya kufunga na kusali, ili kuombea amani na utulivu nchini Ukraine. Hizi ni silaha madhubuti dhidi ya hali tete ya vita inayoendelea kwa sasa nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu ni Mungu wa amani na wala si Mungu wa vita; ni Baba wa wote na wala si kwa baadhi ya watu. Mwenyezi Mungu anataka watu wajenge umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu na wala si kujiundia maadui. Kamwe, Mwenyezi Mungu hawezi kuunga mkono mashambulizi ya kijeshi. Toba na wongofu wa ndani ndiyo silaha madhubuti dhidi ya vita inayoendelea huko nchini Ukraine.

Papa Vita Ukraine
14 March 2022, 15:43