Tafuta

Siku ya Sala na Kufunga kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. 2 Machi 2022. Siku ya Sala na Kufunga kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. 2 Machi 2022. 

Siku ya Kufunga Na Kusali Ili Kuombea Amani Nchini Ukraine

Papa Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Ukraine kwa sala na sadaka zao. Kuna maelfu ya watu wanaokimbia vita na sasa wengi wao wanaelekea nchini Poland. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa kweli kutoka moyoni, tayari kumfuasa Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Baba Mtakatifu akiwa na machungu pamoja na masikitiko makubwa sana moyoni mwake kutokana na Urussi kuivamia kijeshi Ukraine na majanga makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Ukraine, aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. Baba Mtakatifu wakati wa mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe 2 Machi 2022, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Ukraine ambao kwa sasa wanashambuliwa kwa mabomu kiasi kwamba, wengi wao wamelazimika kutafuta hifadhi kwa kujificha chini ya maandaki. Kati ya wasomaji wa salam na matashi mema kwa lugha mbalimbali alikuwepo Mkapuchini kutoka Ukraine ambaye amesema kwamba, wazazi wake ambao kwa sasa wako Ukraine wamelazimika kujificha kwenye maandaki, kwa ajili ya usalama wa maisha yao.

Wazazi hawa wako karibu sana na mji mkuu wa Ukraine, Kiev, ambao umezungukwa na wanajeshi kutoka Urussi. Baba Mtakatifu, kwa mara nyingine tena, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Ukraine kwa sala na sadaka zao. Kuna maelfu ya watu wanaokimbia vita na sasa wengi wao wanaelekea nchini Poland ambayo imefungua mipaka yake, kielelezo cha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Lakini, ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa kweli kutoka moyoni, tayari kumfuasa Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Viongozi waandamizi kutoka Vatican wameitumia kikamilifu Jumatano ya Majivu kwa ajili ya kusali, kufunga na kuombea amani nchini Ukraine.

Sala kwa ajili ya kuombea amani na utulivu Ukraine
Sala kwa ajili ya kuombea amani na utulivu Ukraine

Wakati huo huo, Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, akizungumza na waamini kutoka Ukraine wanaoishi nchini Italia, amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Malkia wa Ukraine. Amebahatika kuzungumza kwa njia ya simu na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine ambaye kwa sasa amejificha ili kusalimisha maisha yake, huku akiendelea kusali na kufunga, ili kuomba neema na baraka za Mungu, ili vita hii iweze kukoma. Silaha kubwa ambayo waamini wanayo mikononi mwao ni sala. Watu wa Mungu nchini Ukraine watambue kwamba, Kanisa linawakumbuka na kuwaombea, ili wahusika wakuu wa mgogoro huu wa kivita waweze kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kujielekeza katika njia ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kwa upande wake, Kardinali Michael F. Czerny, S.J. Mwenyekiti wa Muda wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu, amekazia kuhusu Kipindi cha Kwaresima, safari ya maisha ya kiroho ya Siku 40 za: Kufunga, kusali, kusoma na kutafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaopaswa kuwa ni endelevu, ili hatimaye kufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo Yesu. Rej. Efe 4:13. Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayotoa fursa kwa waamini kujipatanisha na Mungu, hatimaye waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu. Kwaresima iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Fumbo la Utatu Mtakatifu, Jirani na kila mmoja na nafsi yake. Jumatano ya Majivu imekuwa ni fursa kwa ajili kufunga na kusali ili kuombea amani nchini Ukraine. Amewaombea watu wa Mungu nchini Ukraine ili waweze kuwa na njaa na kiu ya haki. Jumuiya ya Kimataifa isikilize na kujibu kilio cha mahangaiko ya wananchi wa Ukraine, kwa kujenga na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Waimarishe imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Neno na Sakramenti zake.

Kufunga na Kusali

 

03 March 2022, 15:45