Tafuta

Papa Francisko tarehe 16 Machi 2022 amefanya mazungumzo kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima kuhusu vita Ukraine. Papa Francisko tarehe 16 Machi 2022 amefanya mazungumzo kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima kuhusu vita Ukraine. 

Papa Francisko Azungumza na Patriaki Cyril wa Urussi: Vita!

Kiini cha mazungumzo haya ni uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Kirussi nchini Ukraine, dhamana na wajibu wa Wakristo na viongozi wao katika kuhamasisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili haki, amani na maridhiano viweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Urussi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, Jumatano jioni tarehe 16 Machi 2022 alipata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii na Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima. Patriaki Cyril alikuwa ameambatana pia na Askofu mkuu Hilarion Alfeyev wa Jimbo kuu la Volokolamsk ambaye pia ni Mjumbe wa Sinodi Takatifu na Mwenyekiti wa Idara ya Mahusiano ya nje ya Kanisa la Kiorthodox la Urussi na Moscow nzima. Kiini cha mazungumzo haya ni uvamizi wa kijeshi uliofanywa na majeshi ya Kirussi nchini Ukraine, dhamana na wajibu wa Wakristo na viongozi wao katika kuhamasisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili haki, amani na maridhiano viweze kushika mkondo wake. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Patriaki Cyril wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima kwa kushiriki katika mazungumzo haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Viongozi wa Makanisa wasimamie haki na amani.
Viongozi wa Makanisa wasimamie haki na amani.

Kama viongozi wa Makanisa wanasukumwa kuonesha dira na mwongozo unaopaswa kufuatwa na waamini wao, katika mchakato wa kutafuta amani; huku wakiendelea kujikita katika kusali na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili hatimaye, vita iweze kukoma na amani kutamalaki. Kanisa linapaswa kutumia lugha ya Kristo Yesu, yaani upendo na wala si lugha ya wanasiasa. Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, wao ni viongozi wa watu wanaomwamini Mungu, Fumbo la Utatu Mtakatifu na Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Ni katika muktadha huu, viongozi wa Makanisa hawana budi kushikamana na kuungana kwa pamoja ili kutafuta amani, kuwasaidia wale wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kuongeza juhudi za kusitisha vita. Viongozi hawa wakuu wa Makanisa wamekazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya kufikia amani ya kweli na ya kudumu. Hii inatokana na ukweli kwamba, wanaoathirika na mashambulizi haya ya kivita ni watu wa kawaida na wanajeshi wa Urussi wanaojikuta wakipoteza maisha yao kutokana na vita.

Makanisa hayana budi kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa sasa kuna uelewa na kiu kubwa ya kutaka amani na watu wamekwisha kujifunza madhara ya vita. Makanisa yanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kuna watoto, wanawake na wazee wasiokuwa na hatia wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na uvamizi wa kivita nchini Ukraine. Roho Mtakatifu anayewaunganisha katika huduma kama viongozi wakuu wa Makanisa anawataka wawasaidie waathirika wa vita.

Makanisa na Ukraine

 

17 March 2022, 16:48