Papa Francesko: Kwaresima Ni Kipindi Cha Toba na Wongofu wa Ndani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Kwaresima ni kipindi cha safari ya Siku 40 katika jangwa la maisha ya kiroho, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani tayari kuadhimisha kiini cha Fumbo la Wokovu wa mwanadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu yaani Fumbo la Pasaka. Hiki ni kipindi kinachosimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 anakazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa kupanda na kuvuna mema katika familia ya binadamu kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Waamini wasichoke katika kutenda mema maana watavuna kwa wakati wake. Wasichoke kusali, kung’oa maovu kutoka katika maisha yao sanjari na kuwatendea mema jirani. Baba Mtakatifu wakati wa salam kwa mahujaji waliohudhuria Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, amewataka waamini kukianza Kipindi hiki cha Kwaresima kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwaresima kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; kufunga na kusali; kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni wakati muafaka wa kuwasaidia maskini na wahitaji zaidi, bila kuchoka kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Toba hii ifanywe kwa moyo wa furaha na shukrani, ili hatimaye, waamini waweze kusherehekea vyema Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Waamini wajiandae kusherehekea Pasaka ya Bwana, huku wakiwa na nyoyo zilizotakaswa na kupyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Kwa ari na moyo wa toba na wongofu wa ndani, waamini wajikite zaidi katika kusali na kuombea amani, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia waja wake huruma na upendo wa daima, wale wote wanaoendelea kuathirika kutokana na vita sehemu mbalimbali za dunia.