Papa Francisko Kuwaasili Watoto Ni Kitendo Cha Huruma na Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kuasili watoto ni mchakato wa kisheria ambao huhamisha uwajibikaji wa mzazi kutoka kwa wazazi wa kuzaliwa kwa mtoto kwenda kwa wazazi wao wa kuwalea, mchakato ambao unapaswa kutekelezwa kisheria. Mradi wa Agata Smeralda “Progetto Agata Smeralda” ulianzishwa rasmi Jimbo kuu la Firenze, nchini Italia kunako mwezi Mei 1999 na Profesa Mauro Barsi, akishirikiana kwa karibu na Kardinali Lucas Moreira Neves, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la São Salvador da Bahia nchini Brazil, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa Kwa Amerika ya Kusini. Ndoto kuu la Mradi wa Agata Smeralda ni kulinda, maisha, utu, heshima na haki msingi za watoto wenye uhitaji mkubwa sehemu mbalimbali za dunia. Mradi wa Agata Smeralda una jumla ya miradi 150 inayoendeshwa katika nchi 15 duniani, kwa kuwasaidia na kuwahudumia watoto zaidi ya elfu saba. Huu ni mradi unaowahusisha wakleri, watawa pamoja na waamini walei, jambo ambalo limemvutia sana Baba Mtakatifu Francisko kielelezo cha umoja, ushiriki na utume wa Kanisa kwa wahitaji zaidi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, watoto wanaoasiliwa wanapata mahitaji yao msingi ikiwa ni chakula, malazi, elimu na afya, ili wakisha kuwa watu wazima, waweze kusaidia mchakato wa kuleta mabadilio katika nchi zao, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za watoto.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 5 Machi 2022 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Mradi wa Agata Smeralda “Progetto Agata Smeralda” ili kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kushirikiana na Jimbo kuu la São Salvador da Bahia nchini Brazil. Katika hotuba yake, amekazia umuhimu wa kuwaasili watoto kama kielelezo cha upendo na ukarimu unaobubujika kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na ushiriki mkamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Watambue kwamba, wao ni washiriki wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Papa Francisko katika Katekesi kuhusu Mtakatifu Yosefu alibainisha kuwa, Mtakatifu Yosefu anaonesha kwamba, kitendo cha kuasili watoto ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa kibaba na kimama. Leo hii kuna mamilioni ya watoto wanaosubiri kuasiliwa na pia kuna wazazi wengi ambao wangependa kuasili watoto lakini hawawezi kutoka na sababu mbalimbali. Wazazi wengine, pamoja na kubahatika kupata watoto, wakati mwingine, bado wanaonesha ukarimu na upendo kwa kuwaasili watoto wengine zaidi.
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuthubutu kuonesha ukarimu kwa kuwaasili watoto, kama njia ya kupambana na ubinafsi pamoja na uchoyo, ili watoto hawa waweze kupata mahitaji yao msingi na kuendelea kukua vyema. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa kushiriki katika kueneza huruma na upendo wa Mungu Baba kwa watoto hawa, zawadi kubwa ambayo Kristo Yesu, amewaachia waja wake, kwa kuwashirika huruma na upendo wa Baba yake wa milele. Huyu ndiye Neno wa Mungu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, akateswa, akafa Msalabani na kufufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili wapate kupokea hali ya kuwa wana. Rej. Gal 4:5. Mapinduzi ya kweli yanaletwa na watu wenye huruma na upendo wa Mungu, bila hata ya watu kutaka kujimwambafai. Kwa sababu watoto wadogo, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ndio wale wanaonyanyaswa, kuteswa na kudhulumiwa: utu na haki zao msingi.
Kwa huruma na upendo wa dhati, watu hawa wanaweza kusimama tena na kuendelea na safari ya maisha. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika huruma na upendo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Serikali pamoja na Taasisi mbalimbali, zitatunga sheria na sera zitakazo wasaidia wazazi kutekeleza wajibu wao wa malezi na makuzi kwa watoto wao. Wawe makini ili watu wasitumbukie kwenye kashfa za kuwaasili watoto kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi. Mwishoni amewatia shime, kusonga mbele kwa imani na matumaini, wakitambua kwamba, wanazo baraka zake za kitume.