Tafuta

Papa Francisko tarehe 13 Machi 2022 amefanya kumbukizi la miaka 9 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Papa Francisko tarehe 13 Machi 2022 amefanya kumbukizi la miaka 9 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. 

Papa Francisko Kumbukizi la Miaka 9 ya Maisha na Utume Wake: 2013-2022

Papa Francisko 13 Machi 2013 alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Na tarehe 19 Machi 2013 alianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petroo. Na kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko pia ni Askofu wa Jimbo la Roma, Kanisa ambalo ni kielelezo cha upendo na mshikamano na Makanisa mengine yote yaliyoenea duniani kote. Yaani: Umoja, Ushiriki na Utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Machi 2013 alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Na tarehe 19 Machi 2013 alianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko pia ni Askofu wa Jimbo la Roma, Kanisa ambalo ni kielelezo cha upendo na mshikamano na Makanisa mengine yote yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya na utamadunisho unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu ameendelea kuhimiza utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamtakia heri na baraka Papa Francisko.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamtakia heri na baraka Papa Francisko.

Baba Mtakatifu anapenda kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa ndiyo maana kamwe hachoki kuombea amani duniani, hata kama amani yenyewe inaonekana kutopatikana kwa urahisi. Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha pia mwanadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko anapofanya kumbukizi la miaka tisa tangu kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki, linasikitika kusema kwamba, kumbukizi hili limeangukia katika nyakati ambapo giza la vita na maafa makubwa kwa watu wa Mungu yametanda kwenye uso wa dunia. Upepo wa vita unaendelea kutishia malango ya Bara la Ulaya, kiasi cha kubeba ndani mwake utamaduni wa kifo na maangamizi makubwa ya watu na mali zao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kusali na kuombea amani duniani; ili mtutu wa bunduki uweze kunyamaza na majadiliano katika ukweli na uwazi yaanze kushika kasi. Huu ndio utume wa Kanisa unaopania kuwasha tena moto wa furaha ya Injili, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na Mama Dunia. Kumbukizi hii pia imeangukia katika maadhimisho ya Miaka 400 tangu Mama Kanisa alipowatangaza watakatifu wafuatao: Mtakatifu Isidori Mkulima, Inyasi wa Loyola, Francisko Xsaveri, Theresa wa Yesu pamoja na Mtakatifu Filippo Neri. Ni katika muktadha huu, Familia ya Mungu nchini Italia, inataka kusali ili kuleta mabadiliko duniani kwa kujizatiti katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa ajili ya amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Maaskofu Katoliki Italia wanapenda kuonesha uwepo wao wa karibu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Mwishoni, wanamweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani.

Papa Miaka 9

 

14 March 2022, 14:41