Tafuta

Papa Francisko Injili Ya Baba Mwenye Huruma: Sherehe Ni Muhimu!

Mwana mkubwa alidhani kwamba, amebaki nyumbani kwa muda wote lakini hakufanyiwa sherehe. Huu ni mwanzo wa mgogoro mkubwa kati ya Baba na Mwanaye mkubwa anayepima mahusiano yao kwa utekelezaji wa nyajibu. Hii inawezekana pia ikawa ni changamoto hata kwa waamini wanaoona dini kama sehemu ya utekelezaji wa sheria na taratibu pasi na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima inabeba ujumbe wa furaha ya Baba mwenye huruma anayewapenda, kuwajali na kuwasubiri watoto wake ili waweze kutubu na kumwongokea. Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima pia huitwa "Domenica Laetare" au “dominika ya furaha” hii ni furaha ya toba na wongofu wa ndani tayari kumrudia Mwenyezi Mungu. Ni furaha na amani ya ndani, baada ya mwamini kujipatanisha na nafsi yake, Mwenyezi Mungu, jirani na mazingira nyumba ya wote. Rej. Lk 15:1-3, 11-32. Sehemu hii ya Injili kwa wengi inajulikana kama Injili ya Mwana Mpotevu. Lakini inapaswa kuitwa Injili ya Baba Mwenye Huruma kwani ndiye mhusika mkuu anayewangojea watoto wake wawili, waweze kutubu na kurejea tena nyumbani, ili aweze kuwafanyia sherehe. Baba Mwenye huruma ni kielelezo cha Mungu Baba Mwenyezi anayesamehe daima, yuko tayari kuwapokea na kuwafanyia watoto wake sherehe, hata kama wametenda dhambi kubwa kiasi gani. Jambo la msingi ni kutubu na kumwongokea Mungu. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 27 Machi 2022 wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amegusia kuhusu mahusiano kati ya Mwana mpotevu, Mwana mkubwa na Baba mwenye huruma mintarafu utekelezaji wa sheria; Umuhimu wa kufanya sherehe kama kielelezo cha ujirani mwema na ukaribu wa Mungu anayetamani kuwaona watoto wake wote wakitubu na kumwongokea, tayari kuanza safari ya mwelekeo mpya wa maisha.

Toba na wongofu wa ndani ni mwanzo wa maisha mapya
Toba na wongofu wa ndani ni mwanzo wa maisha mapya

Baba Mtakatifu anasema, kwa waamini wengi, ndani mwao kuna chembe cha maisha ya mwana mkubwa aliyedhani kwamba, amebaki nyumbani ili kumtumikia Baba yake. Alisikitishwa sana na kile kitendo cha Baba yake kufurahi na kumfanyia sherehe Mwana mpotevu, “aliyeponda nchi pamoja na makahaba” akamchinjia ndama aliyenona. Lakini mwana mkubwa aliyedhani kwamba, amebaki nyumbani kwa muda wote huo, akitekeleza Amri za Baba yake, lakini hakuwahi kumpata mwana mbuzi ili afanye sherehe pamoja na rafiki zake. Huu ni mwanzo wa mgogoro mkubwa kati ya Baba Mwenye huruma na Mwanaye mkubwa anayepima mahusiano yao kwa utekelezaji wa dhamana na nyajibu. Hii inawezekana pia ikawa ni changamoto hata kwa waamini katika ulimwengu mamboleo, wanaoona dini kama sehemu ya utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu. Matokeo yake ni baadhi ya waamini kuwa na “shingo ngumu” kiasi cha kushindwa kuwatambua jirani zao kama ndugu wamoja na matokeo yake ni kuonesha kiburi, hasira na kukataa kuingia ndani.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mwenye Huruma akatoka nje na kumwambia “Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo nanvyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Lk 15: 31-32. Baba Mwenye huruma alikuwa anajitahidi kumfafanulia kijana wake mkubwa kwamba, alikuwa anawathamini wote kama “mboni ya jicho lake.” Wazazi wanafahamu sana changamoto ya malezi na makuzi iliyoko mbele yao. Baba Mwenye huruma anakazia mambo msingi yaliyoko moyoni mwake na wala si utekelezaji wa Amri tu. Hii ni fursa kwa waamini kujichunguza kutoka katika undani wa nyoyo kama wanajisikia kufanyiwa sherehe ili wapate kufurahi. Kufanya sherehe ni mchakato wa ujenzi udugu na ujirani mwema, ili kushinda woga na tabia ya kujikatia tamaa, kama sehemu ya kumbukizi ya makosa yalitotendwa huko nyuma katika maisha. Mwenyezi Mungu anasamehe dhambi na kufanya sherehe kwa sababu ya toba na wongofu wa ndani. Mwenyezi Mungu anasehekea watoto wake wanaporejea tena nyumbani.

Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli.
Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli.

Kwa mtu aliyekengeuka na kutenda dhambi, mara nyingi husutwa na dhamiri nyofu na maneno makali anayorushiwa, lakini Baba Mtakatifu anasema yote haya hayasaidii kitu. Jambo la msingi ni kuonesha ukarimu na kumtia mtu shime, ili aweze kusonga mbele. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga hata na waamini katika ulimwengu mamboleo, kwa kujifunua na kujiweka wazi; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kwa kuonesha tabasamu la “kukata na shoka” na wala si kutaka tena kumdidimiza mtu katika mateso yake. Kadiri ya matakwa ya Baba mwenye huruma anakaza kusema, “tena kufanya furaha na shangwe ilipasa”. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake wa ajabu anavyotenda kwa kuona mdhambi akitubu na kumwongokea. Waamini wajifunze kufurahia matendo mema yanayotekelezwa na jirani zao, kwa sababu ni kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha tafakari yake kwa kuwauliza waamini ikiwa kama wanaweza kuwaangalia na kufurahia matendo mema ya jirani zao? Je, wanaweza kuonesha furaha kwa ajili ya wengine? Bikira Maria awafunde jinsi ya kupokea huruma ya Mungu katika maisha yao, ili huruma hii iweze kuwa ni jicho la kuwaangalia jirani zao.

Baba Mwenye Huruma
27 March 2022, 14:53

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >