Tafuta

Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa moyo wa upendo wa kibaba na ubunifu wa kishujaa miongoni mwa mapadre na watawa ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yosefu awe ni mfano bora wa moyo wa upendo wa kibaba na ubunifu wa kishujaa miongoni mwa mapadre na watawa ndani ya Kanisa. 

Mtakatifu Yosefu Awe Ni Mfano wa Moyo Ubaba na Ubunifu wa Kishujaa

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Shirika. Mt. Yosefu awe ni mfano wa Ubaba wa maisha ya kiroho na kielelezo bora cha ubunifu wa kishujaa. Maadhimisho ya Mkutano Mkuu ni kipindi cha neema kinachokita mizizi yake katika mchakato wa upyaisho na umwilishaji wa karama ya Shirika kwa kusoma alama za nyakati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Waaugustiani wa Recolletti “Ordo Augustinianorum Recollectorum, OAR” lilianzishwa tarehe 6 Juni 1621 kwa kibali cha Papa Gregory wa XV katika Waraka wake wa Kitume “Militantes ecclesiae.” Hili ni Shirika ambalo limejikita zaidi katika tafakuri na maisha ya kijumuiya; linatekeleza utume wake katika nchi 20 sehemu mbalimbali za dunia. Kuanzia tarehe 1 Machi 2022 linaadhimisha Mkutano wake mkuu wa 56 unaonogeshwa na kauli mbiu “Tunatembea kwa pamoja: Mimi nalikuja ili wawe na uzima.” Rej. Yn 10:10. Alhamisi tarehe 17 Machi 2022 wajumbe wa mkutano mkuu wa 56 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Shirika. Mtakatifu Yosefu awe ni mfano wa Ubaba wa maisha ya kiroho na kielelezo bora cha ubunifu wa kishujaa. Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Mkutano Mkuu ni kipindi cha neema kinachokita mizizi yake katika mchakato wa upyaisho na umwilishaji wa karama ya Shirika kwa kusoma alama za nyakati. Wanashirika wamejiandaa kuadhimisha mkutano huu kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tunatembea kwa pamoja: Mimi nalikuja ili wawe na uzima.” Rej. Yn 10:10.

Ni muda wa kumwilisha dhana ya sinodi katika maisha ya Shirika.
Ni muda wa kumwilisha dhana ya sinodi katika maisha ya Shirika.

Huu ni muda wa kutembea kwa pamoja kama Shirika, huku macho na mioyo yao, ikiwa inamkazia Kristo Yesu, kielelezo cha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujikita katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Itakumbukwa kwamba, Shirika hili liko chini ya ulinzi na maombezi ya Mtakatifu Yosefu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ameamua kukazia mambo makuu mawili: Mtakatifu Yosefu awe ni mfano wa Ubaba wa maisha ya kiroho na kielelezo bora cha ubunifu wa kishujaa. Huu ni mwaliko kwa Mapadre na watawa kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu kwa kuwa na moyo wa kibaba unaobubujika mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao katika hija ya maisha yao, wameshindwa kuonja upendo wa kibaba. Watu hawa wataendelea kuteseka hadi pale watakakapofikishwa mbele ya Mwenyezi Mungu, kama kielelezo cha utimilifu wa maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu anapenda sana kuwasikiliza waja wake, anatambua mahitaji yaliyomo mioyoni mwao na kadiri ya wema, huruma na upendo wake anawaonesha njia ya kupitia.

Mtakatifu Yosefu ni mfano na kielelezo bora cha ubunifu wa kishujaa, katika kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtakatifu Yosefu wakati wa nyakati zake. Lakini alijifunza kumtumainia Mungu ambaye aligeuka na kumwamini Yosefu, kiasi hata cha kumkirimia baraka na neema za kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake. Huu ni mwaliko kwa wanashirika hawa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa Kristo Yes una Kanisa lake kwa kujiweka wakfu na hivyo kumruhusu Kristo Yesu aweze kuwaletea mageuzi makubwa katika maisha na kuwageuza kuwa ni: dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompenda Mungu. Rej. Rum 12:1. Baada ya sadaka na majitoleo haya, wawe na ujasiri wa kutoka kwenda kutekeleza utume, kwa ari na moyo mkuu; kwa kujiamini na kwa ubunifu mkubwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu daima yuko pamoja na anatembea pamoja nao hatua kwa hatua na kuwasaidia kufanya maamuzi. Baba Mtakatifu amependa kuwatia shime kusonga mbele, kwa kujiaminisha katika ahadi za Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza vyema utume wa Mama Kanisa.

Mtakatifu Yosefu
17 March 2022, 16:21