Tafuta

Papa Francisko: Mfumo mpya wa uchumi kimataifa unapaswa kusimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu. Papa Francisko: Mfumo mpya wa uchumi kimataifa unapaswa kusimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu.  (Vatican Media)

Mfumo Mpya Wa Uchumi Unasimikwa Katika Utu, Haki Na Heshima Ya Binadamu

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujikita katika malengo yao, kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; ujenzi wa mfumo mpya wa uchumi unaofumbatwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kusahau kurutubisha maisha yao ya kiroho, ushauri anaowapatia kama Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Maadili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la “Anima per il sociale nei valori d’impresa” lilianzishwa kunako mwaka 2001, likipania kukoleza kanuni maadili katika ushirika. Ni Shirikisho linalowaunganisha wakurugenzi, wamiliki wa viwanda na wataalam ambao wanapenda kushirikisha: weledi, ujuzi na utaalam wao kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu katika sekta ya uchumi, jamii na mazingira. Ni katika muktadha wa kumbukizi la miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, wajumbe wa Shirikisho hili, Jumatatu tarehe 14 Machi 2022 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican ambaye amewapongeza kwa kuwekeza katika kanuni maadili na ujenzi wa jamii. Huu ni muda muafaka kwa viongozi kupima mafanikio, changamoto na matumaini kwa siku za mbeleni. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujikita katika malengo yao, kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; ujenzi wa mfumo mpya wa uchumi unaofumbatwa katika: utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kusahau kurutubisha maisha yao ya kiroho, ushauri anaowapatia kama Askofu mwenye dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Mfumo mpya wa uchumi unajikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu
Mfumo mpya wa uchumi unajikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Shirikisho hili kujikita katika kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna uhusiano mkubwa baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya azma ya binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mtikisiko wa uchumi kimataifa kati yam waka 2007 hadi mwaka 2008 ulitoa fursa ya kujenga mfumo mpya wa uchumi, unaozingatia kanuni za kimaadili na njia mpya za kudhibiti biashara ya fedha na utajiri usio halali. Kumbe, kuna haja ya kuangalia vigezo vilivyopitwa na wakati vinavyoendelea kuiathiri dunia kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Mfumo bora wa uchumi usaidie kuboresha uzalishaji na hivyo kuzisaidia kampuni kufanya kazi zao vyema pamoja na kusaidia biashara ndogo ndogo na za kati kuendelea kutengeneza fursa za ajira. Rej. Laudato si, 189. Bado kuna vitisho vya nguvu za kijeshi kikanda kama inavyojionesha huko Ukraine, kielelezo kwamba, kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao hawajajifunza madhara ya vita yaliyojitokeza kwenye Karne ya Ishirini. Katika muktadha kama huu, kuna changamoto kubwa kuweza kutengeneza fursa za ajira kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema sanjari na kujikita katika uwajibikaji wa kijamii.

Jambo hili linawezekana ikiwa kama uchumi utazingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu; uchumi unaosimikwa katika kipaji cha ubunifu sanjari na ikolojia fungamani. Mchakato wa utandawazi unapaswa kuratibiwa na kanuni maadili. Huu ni mwaliko wa ujenzi wa mfumo bora wa uchumi unaozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuendeleza mawasiliano na ushiriki mkamilifu kutokana na mang’amuzi haya, ili hatimaye, kuunda mtandao utakaoweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa kuwapatia ushauri wa Kiaskofu, kwa kutambua kwamba, Askofu anayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza wa Mungu. Wanachama wa Shirikisho hili wajithidi kuboresha maisha yao ya kiroho, kwa kutafuta daima kile kilicho chema, kizuri na cha kweli. Kwa njia hii, makampuni ya Italia yaliweza kuimarika na kupata faida kubwa, na hatimaye kuboresha maisha ya watu na ajira, mambo yanayotekelezwa katika uhuru na ugunduzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, dhamiri zao zilikuwa zimeangazwa na mwanga wa Injili.

Mfumo Mpya wa Uchumi

 

 

14 March 2022, 16:25