Makardinali 9 Waliopandishwa Daraja: Makardinali Mapadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema lengo la kuwa na Makardinali wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia ni kuweza kushuhudia ukatoliki wa Kanisa; kuendeleza ushirika wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wanasema, kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika. Kwa maana Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote “plenam, supremama et universalem potestatem.”
Ni urithi wa Mitume katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27. Makardinali wamegawanyika katika madaraja makuu matatu: Makardinali Mashemasi, Makardinali Mapadre na Makardinali Maaskofu. Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano wa kawaida wa Makardinali, Ijumaa tarehe 4 Machi 2022 amewapandisha madaraja Makardinali 9 kutoka katika Daraja la Makardinali Mashemasi na kuingia katika Daraja la Mashemasi Mapadre. Waliopandishwa daraja ni: Kardinali Manuel Monteiro de Castro, Kardinali Santos Abril y Castelló, Kardinali Antonio Maria Vegliò, Kardinali Giuseppe Bertello, Kardinali Francesco Coccopalmerio, Kardinali João Braz de Aviz, Kardinali Edwin Frederick O’Brien, Kardinali Domenico Calcagno pamoja na Kardinali Giuseppe Versaldi. Mkutano huu umehudhuriwa na Makardinali 42 chini ya uongozi wa Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali.