Tafuta

Katekesi Kuhusu Maana Na Thamani Ya Uzee: Uzee Ni Amana

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu maana na thamani ya uzee amefafanua sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, Nyakati za Mwisho, kadiri ya Mafundisho ya Kristo Yesu, Uharibifu wa mazingira nyumba ya wote na Mzee Nuhu ni mfano bora wa kuigwa katika maadili na utu wema. Rushwa, vita na ukosefu wa haki msingi yasiwe ni mambo ya kawaida hata kidogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, Jumatano tarehe 16 Machi 2022 ameongozwa na tema kuhusu: Uzee kama rasilimali kwa vijana wasiokuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha. Sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonogesha Katekesi hii ni kutoka katika Kitabu cha Mwanzo 6:5-8: “BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.” Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, amefafanua sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, Nyakati za Mwisho, kadiri ya Mafundisho ya Kristo Yesu, Uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, Hekima ya wazee na Mzee Nuhu kama mfano bora wa kuigwa katika maadili na utu wema. Baba Mtakatifu katika ufafanuzi wake amesema, Mwenyezi Mungu alikasirishwa sana na maovu ya mwanadamu yaliyozagaa kwenye uso wa dunia yaani: rushwa, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Hali ambayo inajitokeza hata katika nyakati hizi.

Uzee ni amana na utajiri wa jamii
Uzee ni amana na utajiri wa jamii

Lakini si mambo yote ni mabaya kwani huduma bora za afya zimesaidia sana kurefusha maisha, hata kama kuna vita inayotishia kufuta maendeleo makubwa yaliyofikiwa na mwanadamu katika karne hii. Dhana ya gharika kushuka na kuwaangamiza watu wote inaonekana kutawala kwa nyakati hizi za wasi wasi na hofu kuu kuhusu hatima ya maisha ya mwanadamu. Mkazo hapa ni uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kristo Yesu anasema: “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.” Lk 17:26-27. Kimsingi hii ilikuwa ni sehemu ya maisha ya kawaida, lakini Kristo Yesu anaonya kwa vile mazoea haya yaliwatumbukiza wanadamu katika maovu kiasi kwamba, rushwa, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu zikaonekana kana kwamba, ni mambo ya kawaida tu na sehemu ya maisha na hivyo kupekenyua na hata kusigina tunu msingi za maisha ya kiroho na matokeo yake ni pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote.

Wazee ni manabii wa maadili na utu wema.
Wazee ni manabii wa maadili na utu wema.

Hiki ni kiini cha dhambi jamii inayosimikwa katika uchoyo na ubinafsi; uchu wa mali, utajiri wa haraka haraka na madaraka. Matokeo yake ni vita, utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine pamoja na utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uzee wenye kutukuka unafumbata maisha na sadaka yake; uzuri, utakatifu na ukweli wake; haki, amani, upendo na mshikamano. Haya ni mambo yanayogeuka kuwa ni wito wa wengi. Hekima na ushauri wa wazee unahitajika ili kupambana na mawimbi ya rushwa, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Neema na baraka za Mwenyezi Mungu zikatoa upendeleo wa pekee kwa Nuhu, Nabii dhidi ya rushwa na mmong’onyoko wa maadili na utu wema; kielelezo cha waja wa Mungu wanaomtegemea na kujiaminisha kwake. Lakini pia kwenye Maandiko Matakatifu kuna mifano ya wazee waliokengeuka, wakazama na kutopea katika tamaa za mwili. Hata wazee wa baraza waliotoa hukumu kwa Suzana mwanamke asiyekuwa na hatia, walikuwa ni wala rushwa wakubwa, lakini kwa nje walijifanya kuwa ni watetezi wa haki. Rej. Dan 13:1-30.

Hii ni changamoto anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa wazee kuwa ni mfano bora wa unabii kwa vijana wa kizazi kipya katika maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wazee wanapaswa kuwa ni divai njema inayoleta faraja na furaha kwa vijana wa kizazi kipya; wawe ni wajumbe wa habari njema na wala si kinyume chake. Wazee waheshimiwe na kuthaminiwa na jamii na kamwe wasibezwe na kutwezwa. Kwa hakika, ulimwengu unawahitaji vijana shupavu na wenye nguvu pamoja na wazee wenye hekima na busara katika maisha.

Uzee ni amana

 

16 March 2022, 15:55

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >