Tafuta

Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee tarehe 30 Machi 2022 Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika dhana ya uaminifu machoni pa Mungu kwa kizazi kijacho. Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee tarehe 30 Machi 2022 Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika dhana ya uaminifu machoni pa Mungu kwa kizazi kijacho.   (Vatican Media)

Katekesi Kuhusu Maana Na Thamani Ya Uzee: Uaminifu Machoni Pa Mungu

Leo hii kuliko wakati mwingine wowote katika historia kuna haja ya kuwa na uzee uliojaliwa kuwa na hisia changamfu za kiroho zenye uwezo wa kutambua ishara za Mwenyezi Mungu. Hii ni Ishara ambayo inawapatia watu changamoto kwa sababu ni "ishara inayonenwa" (Lk 2:34), lakini ambayo inawajaza furaha, amani na utulivu wa ndani kutokana na huduma kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tangu Jumatano tarehe 23 Februari 2022 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee. Amekazia muungano thabiti kati ya umri na maisha, ili kutegemeana na kukamilishana katika hija ya maisha, bila ya wazee kuonekana kama mzigo kwa jamii na hivyo kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Wazee wanapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya imani na mang’amuzi ya maisha. Anasema inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Wazee wana ndoto, na vijana wana maono. Rej. Yoe 3:1. Utu, heshima na haki msingi za wazee zinapaswa kulindwa na kuendelezwa, kwa kutambua kwamba, uzee ni amana, utajiri na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wazee wana hekima wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya, ili hata wao waweze kukua na kukomaa kwani wao wanayo mizizi ya historia ya watu wao ni kielelezo cha neema na baraka kwa jamii husika.

Uaminifu machoni pa Mwenyezi Mungu
Uaminifu machoni pa Mwenyezi Mungu

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, amekwisha kuchambua kuhusu: Uzee kama rasilimali kwa vijana wasiokuwa na dira wala mwelekeo sahihi wa maisha. Hii ni changamoto kwa wazee kuwa ni mfano bora wa unabii kwa vijana wa kizazi kipya katika maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wazee wanapaswa kuwa ni divai njema inayoleta faraja na furaha kwa vijana wa kizazi kipya; wawe ni wajumbe wa Habari Njema na wala si kinyume chake. Wazee waheshimiwe na kuthaminiwa na jamii na kamwe wasibezwe na kutwezwa. Kwa hakika, ulimwengu unawahitaji vijana shupavu na wenye nguvu pamoja na wazee wenye hekima na busara katika maisha. Baba Mtakatifu amekwisha kudadavua kuhusu wakati wa wazee kuagana na jamii, urithi na utajiri wao; kumbukumbu na ushuhuda wa maisha, imani na utu wema. Uhai wa macho ya Mtumishi wa Mungu, Musa ilikuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliyomwezesha kurithisha uzoefu na mang’amuzi ya muda mrefu wa maisha na imani mambo msingi sana kwa wazee. Kimsingi wazee wanayo macho ya imani thabiti na kwamba, wanaweza kwa uaminifu mkubwa kurithisha historia kwa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 30 Machi 2022 wakati wa Katekesi yake kuhusu: Maana na Thamani ya Uzee amejikita zaidi katika dhana ya uaminifu machoni pa Mungu kwa kizazi kijacho. Sehemu hii ya Katekesi, imenogeshwa na Injili kama ilivyoandikwa na Luka 2: 25-30 kuhusu Yesu kupelekwa Hekaluni: Maaguzi ya Simeoni na Ana. “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako.”

Jamii inahitahi uzee uliosheheni hisia changamfu za maisha ya kiroho
Jamii inahitahi uzee uliosheheni hisia changamfu za maisha ya kiroho

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwinjili Luka anaweka mbele ya macho ya waamini watu wawili mashuhuri yaani Mzee Simeoni na Ana waliobahatika kumwona Kristo wa Bwana huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Ni watu wanaonesha na kushuhudia uaminifu machoni pa Mungu. Daima Mama Kanisa anamwomba Roho Mtakatifu akisema, “Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waamini, Neema yako mioyoni mwao.” Roho Mtakatifu licha ya udhaifu wa mwili na roho, lakini bado anamkirimia mwanadamu heri na mwanga wa kuweza kuona matendo makuu ya Mungu, tayari kuyapokea kwa imani na matumaini makubwa. Leo hii kuliko wakati mwingine wowote anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna haja ya kuwa na uzee uliojaliwa kuwa na hisia changamfu za kiroho zenye uwezo wa kutambua ishara za Mwenyezi Mungu, yaani Ishara ya Mungu, ambaye ni Kristo Yesu. Ishara ambayo inawapatia watu changamoto kwa sababu ni "ishara inayonenwa" (Lk 2:34), lakini ambayo inawajaza furaha, amani na utulivu wa ndani kutokana na huduma kwa Mungu na jirani. Papa anasema, kuna watu wamepigwa ganzi ya hisi za maisha ya kiroho, katika msisimko na kudumaa kwa zile za kimwili, ni ugonjwa ulioenea katika jamii mamboleo inayokuza udanganyifu wa ujana wa milele, na sifa yake hatari zaidi iko katika ukweli kwamba haijulikani.

Watu hawatambui kwamba, tayari wamekwisha kupigwa ganzi. Ni rahisi sana kupoteza hisi za maisha ya kiroho ambazo zinakwenda mbali zaidi ya ufahamu wa Mungu na maisha ya kidini. Baba Mtakatifu anakaza kusema kwamba, hisi za maisha ya kiroho zinafumbatwa katika msingi wa huruma na ibada; aibu na masikitiko moyoni; uaminifu na majitoleo; upendo na heshima, uwajibikaji binafsi pamoja na kuguswa na mateso ya watu wengine. Kwa bahati mbaya, wazee ni wahanga wa kwanza kupoteza hisi za maisha ya kiroho, hasa katika jamii ambayo inasimikwa kwenye msingi wa mafanikio, watu wenye udhaifu ndani ya jamii, hawataweza kupewa msukumo unaohitajika, kwa sabababu “falsafa inayoongoza hapa ni kwamba, mwenye nguvu mpishe.” Ujenzi wa jamii shirikishi na fungamani ni wazo zito miongoni mwa wanasiasa na ni sahihi, lakini bado linaelea kwenye ombwe. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo jamii unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hapa kuna watu wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ulimwengu unawahitaji mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiroho.
Ulimwengu unawahitaji mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiroho.

Simulizi la Maandiko Matakatifu kuhusu Mzee Simeoni na Ana linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kutambua Ishara ya Mungu ambaye ni Kristo Yesu. Hawa si wakareketwa bali mashuhuda wa Ishara ya Mungu ambayo imemwilishwa katika kizazi kipya na hivyo kuwa ni faraja kwao kwa kuweza kuona na kutangaza historia ya kizazi chao. Hiki ni kielelezo cha shukrani kwa kizazi kijacho; shukrani inayobubujika kutoka katika uzee wa maisha ya kiroho na kuwa ni kielelezo cha ushuhuda, unyenyekevu pamoja na mwanga angavu kwa watu wote. Hapa hakuna husuda kati ya kizazi kimoja na kingine, bali neema na baraka za Mungu zinashuka wakati “mshumaa wa maisha” unapokaribia kuzimika. Hisi za maisha ya kiroho miongoni mwa wazee zina nguvu kiasi cha kuvunjilia mbali tabia ya mashindano yasiyokuwa na tija wala mvuto; kinzani na mipasuko kati ya kizazi kimoja na kingine. Yote haya yanawezekana kwa msaada na neema ya Mungu. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu kama hawa.

Papa Katekesi
30 March 2022, 15:29

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >