Tafuta

Papa Francisko ukarimu wa Poland kwa wananchi wa Ukraine ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Papa Francisko ukarimu wa Poland kwa wananchi wa Ukraine ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.  

Siku ya Kufunga Ili Kuombea Amani Ukraine: Huduma ya Upendo

Papa Francisko asema, watu wa Mungu nchini Poland wamekuwa ni mashuhuda na kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ni huduma inayopania kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jumatano ya Majivu, iwe ni fursa ya kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa amekianza Kipindi cha Kwaresima tarehe 2 Machi 2022 kwa maadhimisho ya Jumatano ya Majivu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2022 unanogeshwa na kauli mbiu “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.” Gal 6:9-10. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na machungu pamoja na masikitiko makubwa sana moyoni mwake kutokana na Urussi kuivamia kijeshi Ukraine, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine bila kusahau maeneo mbalimbali ambako bado mtutu wa bunduki unaendelea kurindima.

Poland imeonesha mfano bora wa huduma kwa wakimbizi kutoka Ukraine
Poland imeonesha mfano bora wa huduma kwa wakimbizi kutoka Ukraine

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 2 Machi 2022 wakati wa Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Maana na Thamani ya Uzee, ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Poland, kwa kuwa nchi ya kwanza kufungua mipaka yake ili kuwapokea na hatimaye, kuwahudumia wakimbizi wa vita kutoka nchini Ukraine. Hiki ni kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ni huduma inayopania kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Jumatano ya Majivu, iwe ni fursa ya kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inapata chimbuko lake katika toba na wongofu wa mtu binafsi, tayari kumfuasa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, kwa kushirikiana na Mashirika ya Misaada kutoka Bulgaria, "Caritas Bulgaria" yanaendelea kujipanga vyema zaidi ili kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi wa kivita kutoka Ukraine. Familia mbalimbali ziko tayari kuwapokea na kuwapatia hifadhi watu wenye uhitaji mkubwa zaidi, kila familia kadiri ya uwezo na nafasi yake. Watu wa Mungu nchini Ukraine wanahitaji kuonjeshwa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kulinda: utu, heshima na haki zao msingi. Ni fursa ya kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa, wakavunjika na kupondeka moyo!

Watu wanateseka sana kwa vita
Watu wanateseka sana kwa vita

Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hungaria, "Caritas Hungary," tangu kuvamiwa kwa Ukraine limekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi hasa kuhusiana na afya, chakula na makazi ya muda. Kadiri vita hii inavyoendelea kuchukua kasi na muda mrefu zaidi kuliko ilivyotarajiwa, watu wengi wanaweza kuanza kupoteza maisha kutokana na baa la njaa. Hali ya maisha inazidi kudidimia wakati gharama ya maisha inazidi kucharuka zaidi. Wakati huo huo, Caritas Ambrosiana kutoka Jimbo kuu la Milano, Italia limejiunga katika mtandao wa Caritas Internationali kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi sanjari na kusali pamoja nao, kwani faraja ya maisha ya kiroho ni kati ya huduma msingi zinazoweza kutolewa kwa watu wanaoteseka na kusononeka kwa ajili ya vita.

Kufunga na Kusali

 

02 March 2022, 15:14