Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa UNITALSI Lombardia: Huruma na upendo kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa UNITALSI Lombardia: Huruma na upendo kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. 

Jubilei ya Miaka 100 UNITALSI Lombardia: Huruma na Upendo

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kusikiliza na kujibu kilio na mahitaji msingi ya wazazi na watoto wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali na vituo mbalimbali vya afya huko Milano. Wazazi wengi ni wale wanaotoka kwenye familia zisizojiweza kutokana na kusiginwa na umaskini. Waamini wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Kitaifa wa Usafiri wa Wagonjwa wa Italia Lourdes na Madhabahu ya Kimataifa, UNITALSI “Unione Nazionale Italiana Trasporto Ammalati a Lourdes e Santuari Internazionali, UNITALSI” ulianzishwa na Kijana Giovanni Battista Tomassi, kunako mwaka 1903. Huo ukawa ni mwanzo wa historia ya upendo, mshikamano wa udugu na huduma inayotekelezwa na UNITALSI kama chombo na wajumbe wa faraja na matumaini kwa wagonjwa. UNITALSI Lombardia, Kaskazini mwa Italia, inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei hii, imeamua kujenga nyumba itakayowahudumia wazazi na watoto wachanga wanaohudumiwa katika hospitali za Milano, Kaskazini mwa Italia. Hiki ni kielelezo cha ujirani mwema, huruma na upendo kwa wagonjwa unaotekelezwa na UNITALSI si tu kwa kuwasafirisha wagonjwa kwenye Madhabahu ya Lourdes, bali pia kutoa huduma kwa wazazi na watoto wao wachanga, kwa kuwajengea nyumba ya huduma. Hiki ni kielelezo cha matendo ya huruma. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani.

Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwa njia hii Mwenyezi Mungu ameshuka na kukaa pamoja na waja wake. Huruma ni sheria ya msingi ambayo imechorwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu inayomwezesha kumwangalia kila mwanadamu anayekutana naye kwa unyofu. Huruma ni daraja inayo muunganisha Mwenyezi Mungu na binadamu na hivyo kuufungulia moyo mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha ya mwanadamu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 29 Machi 2022 amewatumia ujumbe wanachama wa Umoja wa Kitaifa wa Usafiri wa Wagonjwa wa Italia Lourdes na Madhabahu ya Kimataifa, UNITALSI, Lombardia kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Amewapatia pia jiwe la msingi kutoka katika matofali ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Waraka wake wa Kitume “Uso wa huruma: Misericordiae vultus” wa tarehe 13 Machi 2015 na yakazinduliwa rasmi tarehe 29 Novemba 2015 na hatimaye, kuhitimishwa tarehe 20 Novemba 2016.

UNITALSI: Huruma na upendo ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya waja wake.
UNITALSI: Huruma na upendo ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Kristo Yesu kwa kuyaona yale makundi ya watu waliomfuata aligundua kwamba, walikuwa wamechoka na kuishiwa nguvu, wamepotea na bila kiongozi, na akasikia huruma sana kwa ajili yao. Rej. Mt 15: 37. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kilichomsukuma Kristo Yesu katika mazingira haya yote si kingine ila huruma, iliyomwezesha kusoma nyoyo za wale aliokutana nao na kuwatimizia mahitaji yao ya kina. Rej. Misericordia vultus, 8. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kusikiliza na kujibu kilio na mahitaji msingi ya wazazi na watoto wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali na vituo mbalimbali vya afya huko Milano. Wazazi wengi ni wale wanaotoka kwenye familia zisizojiweza kutokana na kusiginwa na umaskini. Huduma hii, iwe ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume.

Hili ni tukio ambalo limewakusanya viongozi wakuu wa Kanisa na Serikali. Ujenzi wa nyumba hii ni mchango kutoka kwa watu mbalimbali walioguswa na kusukumwa na huruma na upendo wa Mungu kwanza kabisa katika maisha yao. Hii ni huduma inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa ufupi kabisa, UNITALSI Lombardia inasema, nyumba hii ni zawadi ya uhai, imani, familia, urafiki na Maandiko Matakatifu yanayomwilishwa katika huduma ya upendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Hii ni zawadi ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika mchakato wa ujenzi wa urafiki na ushuhuda wa furaha ya kweli. Nyumba hii inajengwa kwa heshima ya Fabrizio Frizzi ambaye katika maisha na utume wake, alikuwa ni rafiki na shuhuda wa huruma ya Mungu.

UNITALSI Lombardia

 

29 March 2022, 15:15